004-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Haifai Kuapa Kila Wakati

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

04- Haifai Kuapa Kila Wakati

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

[At-Tafsiyr Al-Kabiyr ya Ar-Raaziy (6/75), 30/83) na Al-Mabsuwtw (8/127)]

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ"

 

“Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili”.  [Al-Qalam (68:10)].

 

الحَلَّافُ  kwa mujibu wa walivyomwelezea baadhi ya Mufassiruna, ni mwingi wa kuapa katika haki na baatwil, na kwa tabia hiyo ya kuapa ovyo ovyo, inatosha kuwa alama ya kujiweka mbali na mtu huyo.  Na Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema:

 

"وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ"

 

“Na hifadhini yamini zenu”.  [Al-Maaidah (5:89)].

 

Muradi wa Aayah hii ni jizuieni kuapa apa – kwa mujibu wa kauli ya mmoja wa Mufassiruna-, kwani linalotazamiwa baada ya kuapa ni kuhifadhi jema lililoapiwa, au kwa maana ya jizuieni msiape bila sababu yoyote.

 

Waarabu walikuwa wakimsifu mtu kutokana na uchache wa kuapa kwake kama alivyosema Kathiyr:

 

                 قَلِيْلُ الأَلَايَا حَافِظٌ لِيَمِيْنِهِ                  فَإِنْ سَبَقَتْ مِنْهُ الأَلِيَّة ُ بَرَّتِ 

 

“Ni mchache mno wa kuapa, alindaye kiapo chake, na kama kiapo chake kimemtangulia, basi hukiheshimu akakitekeleza”.

 

Na hikma ya watu kuamuriwa kuapa kwa ufinyu iwezekanavyo, ni kuwa mtu anayeapa kwa Allaah kwa kila kichache na kingi, basi ulimi wake utazoea hilo, na kiapo hakitakuwa na uzito wala thamani kwenye moyo wake, na hatokuwa na muamana wa kuthubutu kuapa kiapo cha uongo.  Na hapo lengo asili la kiapo litapoteza mwelekeo.  Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amekirihisha kuapa katika kuuza na kununua kwa kusema:

 

"الْحَلِفُ مَنْفَقَةٌ لِلسِّلْعَةِ مَمْحَقَةٌ لِلرِّبْحِ"

 

Kiapo ni chuuzo la bidhaa, futo la baraka ya faida”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2087) na Muslim (1606)].

 

 

 

Share