014-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Kuapa Kwa Asiye Allaah Ni Shirki

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

014- Kuapa Kwa Asiye Allaah Ni Shirki

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Toka kwa Ibn ‘Umar kwamba alimsikia mtu mmoja akisema:  Laa, naapa kwa Al-Ka’abah.  Ibn ‘Umar akamwambia: Haapiwi asiye Allaah, kwani hakika mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"مَنْ حَلَفَ بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ أَشْرَكَ"

 

“Mwenye kuapa kwa asiye Allaah, basi hakika amefanya shirki”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1535) na Abu Daawuwd (3251)].

 

Inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Qutaylah –Mwanamke toka Juhaynah- :

 

"أَنَّ يَهُودِيًّا، أَتَى النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ إِنَّكُمْ تُنَدِّدُونَ وَإِنَّكُمْ تُشْرِكُونَ تَقُولُونَ مَا شَاءَ اللَّهُ وَشِئْتَ وَتَقُولُونَ وَالْكَعْبَةِ ‏.‏ فَأَمَرَهُمُ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا أَرَادُوا أَنْ يَحْلِفُوا أَنْ يَقُولُوا ‏"‏ وَرَبِّ الْكَعْبَةِ ‏"‏ ‏.‏ وَيَقُولُونَ ‏"‏ مَا شَاءَ اللَّهُ ثُمَّ شِئْتَ "

 

“Kwamba Myahudi mmoja alikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Hakika nyinyi mnamfanyia Allaah ulinganishi na viumbe, na hakika nyinyi mnamfanyia washirika.  Mnasema:  Alitakalo Allaah na ulitakalo [mnafanya sawa Matashi ya Allaah na matashi ya binadamu].  Na mnasema:  Naapa kwa Al-Ka’abah.  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaamuru [Maswahaba] waseme wanapotaka kuapa: Naapa kwa Mola wa Al-Ka’abah, na waseme:  Alitakalo Allaah, kisha ulitakalo”.  [Matashi ya mja yaje baada ya Matashi ya Allaah].  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/6) na Ahmad (6/371)].

 

Katazo la kuapa kwa asiye Allaah limekuja katika Hadiyth kadhaa.  Kati ya Hadiyth hizo ni:

 

 

1-  Hadiyth ya Abu Hurayrah.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا تَحْلِفُوا بِآبَائِكُمْ وَلَا بِأُمَّهَاتِكُمْ وَلَا بِالْأَنْدَادِ وَلَا تَحْلِفُوا إلا بِاللَّهِ، وَلَا تَحْلِفُوا إِلَّا وَأَنْتُمْ صَادِقُونَ"

 

“Msiape kwa baba zenu, wala kwa mama zenu, wala kwa viumbe wanaolinganishwa na Allaah.  Na wala msiape isipokuwa kwa Allaah, na wala msiape isipokuwa mnasema kweli”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3248) na An-Nasaaiy (7/5)].

 

2-  Toka kwa ‘Abdur Rahmaan bin Samurah amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

" لَا تَحْلِفُوا بِالطَّوَاغِي وَلَا بِآبَائِكُمْ"

 

“Msiape kwa masanamu wala kwa baba zenu”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1648), An-Nasaaiy (7/7) na Ibn Maajah (2095)].

 

3-  Toka kwa Ibn Az Zubayr:

 

"أَنَّ عُمَرَ  لَمَّا كَانَ بِالْمَخْمَصِ مِنْ عُسْفَانَ اسْتَبَقَ النَّاسُ فَسَبَقَهُمْ عُمَرُ ، فقَالَ ابْنُ الزُّبَيْرِ : فَانَتهَزْتُ فَسَبَقْتُهُ ، فَقُلْتُ : سَبَقْتُه وَالْكَعْبَةِ، ثُمَّ انتهَزَ فَسَبَقَنِي ، فَقَالَ : سَبَقْتُه وَاللَّهِ ، ثُمَّ أَنَاخَ فَقَالَ : أَرَأَيْتَ حَلِفَكَ بِالْكَعْبَةِ ، وَاللَّهِ لَوْ أَعْلَمُ أَنَّكَ فَكَّرْتَ فِيهَا قَبْلَ أَنْ تَحْلِفَ لَعَاقَبْتُكَ ، احْلِفْ بِاللَّهِ فَأْثَمْ أو أبْرُرْ"

 

Kwamba ‘Umar alipokuwa Mahmasw akitokea ‘Usfaan, watu walishindana na ‘Umar akawatangulia.  Ibn Az-Zubayr akasema: Nikavizia nafasi, nami nikamtangulia, nikasema:  Nimemtangulia, naapa kwa Al-Ka’abah.  Kisha naye akavizia nafasi, akanitangulia na akasema:  Nimemtangulia, wa Allaah (naapa kwa Allaah).  Kisha akamtua chini ngamia wake na kuniambia:  Unaona ulivyoapa kwa Al-Ka’abah!  Wa Allaah, lau ningelijua kwamba umekifikiria kiapo chako hicho kabla ya kukiapa, basi ningelikuadhibu.  Apa kwa Allaah upate dhambi (kwa kuvunja kiapo chako), au ukitekeleze.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (15927) na Al-Bayhaqiy (10/29)].

 

4-  Toka kwa Ibn Mas-‘uwd amesema:

 

" لأَنْ أَحْلِفَ باللهِ كاذِبًا أَحَبُّ إِليَّ مِنْ أَنْ أَحْلِفَ بِغَيْرِهِ صَادِقًا"

 

“Mimi kuapa kwa Allaah nikiwa mwongo ni nafuu zaidi kwangu kuliko kuapa kwa asiye Allaah nikiwa mkweli”.  [Isnaad yake ni Swahiyh.  Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (15929) na wengineo.  Angalia Al-Irwaa (8/192)].

                                               

 

 

 

Share