030-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Hakuna Nadhiri Ya Kujikurubisha Kwa Allaah Kwa Asichokimiliki Mtu

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

030-Hakuna Nadhiri Ya Kujikurubisha Kwa Allaah

Kwa Asichokimiliki Mtu

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Katika Hadiyth ya ‘Imraan bin Huswayn (Radhwiya Allaah ‘anhu) kuhusiana na kisa cha mwanamke wa Kianswaar ambaye alitekwa:

 

"وَنَذَرَتْ لِلَّهِ إنْ نَجَّاهَا اللَّهُ عَلَيْهَا لَتَنْحَرَنَّهَا [أي: العَضْبَاءُ]، فَلَمَّا قَدِمَتِ المَدِينَةَ رَآهَا النَّاسُ، فَقَالُوْا: العَضْبَاءُ نَاقَةُ رَسولِ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَقَالَتْ: إنَّهَا نَذَرَتْ إنْ نَجَّاهَا اللَّهُ عَلَيْهَا لَتَنْحَرَنَّهَا، فأتَوْا رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، فَذَكَرُوا ذلكَ لَهُ، فَقَالَ: سُبْحَانَ اللهِ، بِئْسَمَا جَزَتْهَا، نَذَرَتْ لِلَّهِ إنْ نَجَّاهَا اللَّهُ عَلَيْهَا لَتَنْحَرَنَّهَا، لا وَفَاءَ لِنَذْرٍ في مَعْصِيَةٍ، وَلَا فِيما لا يَمْلِكُ العَبْدُ".

 

“Na akaweka nadhiri kwa Allaah kwamba Allaah Akimwokoa akiwa juu ya mgongo wake, yaani “Al-‘Adhbaa” (akiwakimbia maadui), basi atamchinja. Alipofika Madiynah, watu walimwona, wakasema: Al-‘Adhbaa, ngamia jike wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Akasema kuwa yeye ameweka nadhiri kuwa Allaah akimwokoa akiwa juu ya mgongo wake, basi atamchinja.  Wakaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam wakamweleza hilo.  Rasuli akasema: Subhaana Allaah! Amefanya kosa baya kumtoa kafara!  Ameweka nadhiri kwa Allaah kuwa Allaah Akimwokoa akiwa juu ya mgongo wake atamchinja!  Hakuna nadhiri katika jambo la maasia, wala katika ambacho mja hakimiliki”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1641), Abu Daawuwd (3316), An-Nasaaiy (7/19), Ibn Maajah (2124) na wengineo].

 

Na toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake amesema:  “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"لَا نَذْرَ لِابْنِ آدَمَ فِيمَا لَا يَمْلِكُ"

 

“Hakuna nadhiri kwa mwanadamu kwa kisicho mali yake”.  [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1181), Abu Daawuwd (2190), Ibn Maajah (2047) na wengineo].

 

·        Na Je Atalazimiwa Kafara Akiweka Nadhiri Kwa Kisicho Chake?

 

Kuna kauli mbili.  Yenye nguvu zaidi ni ile isemayo kuwa halazimiwi.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

·        Mwenye Kuweka Nadhiri Ya Kutoa Swadaqah Mali Yake Yote

 

Mwenye kuiwekea nadhiri mali yake yote kwa ajili ya Allaah ili itumiwe katika mambo ya kheri, ‘Ulamaa katika hili wana madhehebu kumi ambapo mengi yake hayana mwega wa dalili.  Na yale yenye mwega wa dalili kati yake yana kauli tatu:  [Al-Mughniy (10/72) na Kash-Shaaful Qinaa (6/279)].

 

Kauli Ya Kwanza:  Ni Lazima Atoe Swadaqah Mali Yake Yote.  Hili limesimuliwa toka kwa Ash-Shaafi’iy na An-Nakh’iy pamoja na Abu Haniyfah (ikiwa ni mali ya Zakaah).  Hujjah ya kauli hii ni dalili zilizotangulia juu ya uwajibu wa kutekeleza nadhiri ya twa’a au utiifu kama neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

"مَنْ نذَرَ أَنْ يُطيْعَ اللهَ فلْيُطِعْهُ".

“Mwenye kuweka nadhiri kwamba atamtii Allaah, basi amtii”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma].

 

Na kwa yaliyothibiti kwamba Abu Bakr (Radhwiya Allaah ‘anhu) alitoa swadaqah mali yake yote, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkubalia.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1678), At-Tirmidhiy (3675) na Ad-Daaramiy (1660)].

 

Kauli Ya Pili:  Yamtosheleza Kutoa Theluthi Ya Mali Yake.  Ni madhehebu ya Maalik, Ahmad (katika riwayah mashuhuri), Al-Layth na Az Zuhriy.  Hujjah yao ni:

 

Hadiyth ya Ka-‘ab bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu) kuhusiana na Tawbah ya Allaah kuwasamehe watatu ambao walibaki nyuma wasende vitani (Vita vya Tabuk).  Mwisho wa maneno yake alisema:

 

 

"يَا رَسُولَ اللَّه إنَّ مِن تَوْبَتي أنِّي أنْخَلِعُ مِن مَالِي صَدَقَةً إِلى اللَّهِ وَرَسُولِهِ، فَقَالَ النبيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أمْسِكْ عَلَيْكَ بَعْضَ مَالِكَ، فَهُوَ خَيْرٌ لَكَ".

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Hakika sehemu ya tubio langu ni kwamba mimi najiondoa na kujivua na mali yangu iwe swadaqah kwa Allaah na Rasuli Wake.  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Bakisha sehemu ya mali yako kwa ajili yako, hilo ni bora zaidi kwako”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2758) na Muslim (2769)].

 

Na katika riwaayah nyingine:

 

"إنَّ مِنْ تَوْبتي إِلَى اللَّهِ أَنْ أُخْرِجَ مِنْ مَاليْ كُلِّهِ إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَدَقةً. قَالَ: لا، قُلْتُ: فَنِصْفَهُ، قَالَ: لا، قُلْتُ: فَثُلُثَهُ؟ قَالَ: نَعَمْ، قُلْتُ: فَإِنِّيْ أُمْسِكُ سَهْمِيْ مِنْ خَيْبَرَ".

 

“Hakika sehemu ya tubio langu kwa Allaah ni kuwa mimi ninaitoa mali yangu yote kwa Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iwe swadaqah. Akasema:  Hapana.  Nikasema:  Basi nusu yake.  Akasema:  Hapana.  Nikasema: Basi theluthi yake.  Akasema:  Na’am.  Nikasema:  Basi mimi nabakisha fungu langu (la ngawira) lililoko Khaybar”.  [Isnaad yake ni Hasan.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3331)].

 

Wenye kauli hii wamesema:  “Mwonekano wa Hadiyth ni kwamba Ka’ab alikuja kwa niya ya kutaka kutoa mali yake yote kama nadhiri na toba, hakuja kutaka ushauri, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru abakishe sehemu ya mali na kumweleza wazi kuwa hilo ni bora zaidi”.

 

Utoaji huu wa dalili umepingwa kwa kusemwa kwamba tamshi alilokuja nalo Ka’ab bin Maalik si la kutoa swadaqah mali yake mpaka liingie ndani ya duara la mvutano, bali ni tamshi linaloelezea niya ya kukusudia kufanya jambo ambalo bado hajalifanya.  Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwashiria asifanye hilo, bali abakishe sehemu ya mali yake, na hiyo ni kabla hajafanya aliloliazimia.  Hivi ndivyo tamshi linavyoonekana, au linavyochukulika.

 

Hoja hii imejibiwa kwa kusemwa kwamba inavyoonekana ni kuwa yeye hakuja kwa ushauri, bali alishaazimia kwa kukata, kwa sababu tamshi lake limeanzwa kwa sentensi taarifu iliyotiliwa usisitizo na herufi ya usisitizo ambayo ni "إِنَّ" katika neno lake: "إنَّ مِنْ تَوْبَتِي"  .  Na tamshi ambalo liko katika muundo huu haiwezekani kulipa maana ya kusita na kutaka ushauri.

 

Wamesema:  Hili linatiliwa nguvu na kwamba wakati Allaah Ta’aalaa Alipomkubalia Abu Lubaabah tawbah yake alisema:

 

" يَا رَسُولَ اللَّه، إِنَّ مِنْ تَوْبَتِي أَنْ أَهْجُرَ دَارَ قَوْمِي وَأُسَاكِنُكَ وَأَنْ أَنْخَلِعَ مِنْ مَالِي كُلِّهِ صَدَقَةً لله عَزَّ وَجَلَّ وَلِرَسُوْلِهِ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "يُجْزِئُ عَنْكَ الثُّلُثُ"

 

“Ee Rasuli wa Allaah! Hakika sehemu ya tubio langu, ni kuwa mimi naihama nyumba ya watu wangu (ambayo nilifanyia makosa ndani yake) na badala yake nakuja kukaa karibu nawe, na ninajivua na mali yangu yote iwe swadaqah kwa Allaah ‘Azza wa Jalla na Rasuli Wake.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Hapana, inakutosheleza theluthi”.  [Kuna mvutano kuhusu Sanad yake.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3319), Ahmad (3/452-502) na Maalik (1039)].

 

Kauli Ya Tatu:  Halazimiwi Chochote.  Ni riwaayah toka kwa Abu Haniyfah (isiyohusiana na mali ya Zakaah).  Na haya ni madhehebu ya Abu Muhammad bin Hazm ambaye anategemeza hujjah yake kuwa kutoa swadaqah mali yote si jambo halali akitolea dalili kwa haya yafuatayo:

 

1-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا"

 

26.  Na mpe jamaa wa karibu haki yake, na masikini, na msafiri (aliyeharibikiwa); na wala usifanye ubadhirifu wa ufujaji mkubwa.  [Al-Israa: 017].

 

2-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

" وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ ۖ وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ"

 

Na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake; na wala msifanye israfu. Hakika Yeye Hapendi wafanyao israfu.  [Al-An’aam: 006].

 

 

Amesema:  “Hapa Allaah Amelaumu na Ameeleza wazi kuwa Hampendi mtu mwenye kutoa swadaqah mali yake yote anayoimiliki”.

 

 

3-  Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah, amesema:

 

"كُنَّا عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذْ جَاءَهُ رَجُلٌ بِمِثْلِ بَيْضَةٍ مِنْ ذَهَبٍ فَقَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ : أَصَبْتُ هَذِهِ مِنْ مَعْدِنٍ فَخُذْهَا فَهِيَ صَدَقَةٌ مَا أَمْلِكُ غَيْرَهَا ‏.‏ فَأَعْرَضَ عَنْهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِرَارًا، وَهُوَ يُرَدِّدُ كَلاَمَهُ هذَا، ثُمَّ أَخَذَهَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَحَذَفَهُ بِهَا، فَلَوْ أَنَّهَا أَصَابَتْهُ لأَوْجَعَتْهُ أَوْ لَعَقَرَتْهُ، وَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ‏"‏ يَأْتِيْ أَحَدُكُمْ بِمَا يَمْلِكُ فَيَقُولُ هَذِهِ صَدَقَةٌ ثُمَّ يَقْعُدُ فَيَتَكَفَّفُ النَّاسَ، خَيْرُ الصَّدَقَةِ مَا كَانَ عَنْ ظَهْرِ غِنًى".

 

“Tulikuwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomjia mtu mmoja na dhahabu ya uzito wa yai.  Akasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Nimeipata hii kwenye mgodi, basi ichukue ni swadaqah, sina ninachokimiliki zaidi yake.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumjibu kitu mara kadhaa huku mtu akikariri maneno yake hayo hayo.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaichukua akamrushia nayo.  Lau ingelimpata ingemtia maumivu au kumuumiza vibaya. Na Rasuli wa Allaah akasema:  Analeta mmoja wenu kile anachomiliki na kusema hiki ni swadaqah, kisha anakaa na kuanza kuomba omba watu.  Bora ya swadaqah ni kile atoacho mtu huku yeye amejitosheleza”.  [Isnaad yake ni Layyin.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1673), Ad-Daaramiy (1659), Bin Humayd (1121), Abu Ya’alaa (2084) na Ibn Hibaan (3372).  Kuna upokezi wa Ibn Ishaaq ambaye ni mdanganyifu].

 

Amesema:  Na kama watatoa hoja kwa kutumia Kauli Yake Ta’aalaa:

 

وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ

 

“na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wanahitaji”.  [Al-Hashr: (59:09)], basi wataambiwa kwamba Aayah hii haimaanishi kwamba hawakujibakishia wenyewe cha kuwaendeshea maisha yao, bali walikuwa wakitoa kidogo na kujibakishia baadhi ya chakula.

 

Kauli Yenye Nguvu:

 

Linalonibainikia mimi ni kuwa kusema kuwa halazimiwi na chochote ikawa ndio basi katika kauli ya mwisho (ya tatu), usemi huu ni dhaifu.  Mtu kutoa swadaqah mali yake yote ni jambo linaloruhusiwa, kwani imethibiti kwamba Abu Bakr (Radhwiya Allaah ‘anhu) alileta mali yake yote akaikabidhi kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akamkubalia hilo na akamsifia kwa kheri kwa hilo.  Aidha, ‘Umar alitoa swadaqah nusu ya mali yake –ambayo ni zaidi ya theluthi- na Rasuli akamkubalia.  Hivyo inaonekana kuwa mwenye kuweka nadhiri kwa mali yake yote –bila kuweko madhara kwake na kwa wanaomtegemea kwa hilo- basi ni lazima atoe swadaqah mali yake yote.

 

Lakini kama yatakuwepo madhara kwake na kwa wanaomtegemea, hapo ni lazima atoe swadaqah kwa kiasi ambacho hakitomletea madhara, ni sawa ikiwa theluthi, au chini yake, au zaidi.  Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

" وَيَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلِ الْعَفْوَ"

 

“Na wanakuuliza nini watoe. Sema:  Yaliyokuzidieni”.  [Al-Baqarah: (02:219)].

 

Na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam):

 

" لاَ ضَرَرَ وَلاَ ضِرَارَ "

 

 “Usidhuru mtu (kwa kukusudia) wala msidhuriane (kwa kukusudia).  [Hadiyth Swahiyh.  Angalia Al-Irwaa (896)].

 

·        Mwenye Kuweka Nadhiri Ya Kuswali Baytul Maqdis Itamtosheleza Kuswali Al-Masjidul Haraam

 

Toka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah:

 

 

"أنَّ رَجُلاً قَامَ يَوْمَ الْفَتْحِ فَقَالَ : يَا رَسُولَ اللهِ، إِنِّيْ نَذَرْتُ لِلهِ إِنْ فَتَحَ اللهُ عَلَيْكَ مَكَّةَ أَنْ أُصلِّيَ فِيْ بَيْتِ الْمَقْدِسِ رَكْعَتَيْنِ . فَقَالَ لَهُ النَّبيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: صَلِّ هَاهُنَا . ثُمَّ أَعَادَ عَلَيْهِ، فَقَالَ : صَلِّ هَاهُنَا . ثُمَّ أَعَادَ عَلَيْهِ فَقَالَ : شَأنُكَ إذًا".

“Kwamba mtu mmoja alisimama Siku ya ukombozi (wa Makkah) akasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Hakika mimi niliweka nadhiri kwa Allaah kwamba Allaah Akikufungulia Makkah, basi nitaswali rakaa mbili huko Baytul Maqdis (Al-Masjidul Aqswaa).  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Swali hapa hapa.  Mtu yule akarudia maneno hayo hayo.  Rasuli akamwambia:  Swali hapa hapa.  Akarudia tena maneno hayo hayo.  Rasuli akamwambia:  Basi fanya uonavyo mwenyewe (nenda ukaswali huko)”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3305), Ahmad (3/363), Ad-Daaramiy (2339) na wengineo].

 

·        Tanbihi:

 

Lau ataweka nadhiri ya kufunga safari kwenda kuswali Msikiti mwingine na si Al-Masjidul Haraam, au Al-Masjidun Nabawiy, au Al-Masjidul Aqswaa, basi haijuzu kuitekeleza, kwa sababu ni nadhiri ya ma’aswiyah, lakini ni lazima atoe kafara ya yamini.  Kwani Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

" لَا تُشَدُّ الرِّحَالُ إِلَّا إِلَى ثَلَاثَةِ مَسَاجِدَ: مَسْجِدِ الْحَرَامِ وَالْمَسْجِدِ الْأَقْصَى وَمَسْجِدِي هَذَا. "

 

“Safari ndefu hazifungwi isipokuwa kwenda Misikiti Mitatu:  Masjidul Haraam, Al-Masjidul Aqswaa na Msikiti wangu huu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1189) na Muslim (1397)].

 

 

 

Share