06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Chinjo La Kisharia:Taratibu Njema Za Kuchinja

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 التَّذْكِيَةُ الشَّرْعِيَّةُ

 

Chinjo La Kisharia

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

06-Chinjo La Kisharia: Taratibu Njema Za Kuchinja

 

Katika kuchinja, kuna mambo kadhaa ambayo yamestahabiwa, nayo ni haya yafuatayo:

 

1-  Mnyama achinjwe bila maumivu au mateso

 

Hili linafanikishwa kwa kukinoa vyema kisu au mfano wake, na kumchinja mnyama chinjo la haraka.  Hili humpumzisha haraka, na hateseki wala hapati maumivu.

 

Toka kwa Shad-daad bin Aws, amesema:  Mambo mawili nimeyahifadhi toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Amesema Rasuli:

 

"إِنَّ اَللَّهَ كَتَبَ اَلْإِحْسَانَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ ، فَإِذَا قَتَلْتُمْ فَأَحْسِنُوا اَلْقِتْلَةَ ، وَإِذَا ذَبَحْتُمْ فَأَحْسِنُوا اَلذِّبْحَةَ، وَلْيُحِدَّ أَحَدُكُمْ شَفْرَتَهُ, وَلْيُرِحْ ذَبِيحَتَهُ"

 

“Hakika Allaah Ameamuru wema katika kila kitu.   Mnapoua, basi uweni kwa njia nzuri (yenye maumivu kidogo iwezekanavyo), na mnapochinja, basi chinjeni chinjo zuri (la haraka bila mateso), na mmoja wenu akinoe vyema kisu chake, na asimpe tabu mnyama wake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1955)].

 

Inakuwa ni vyema zaidi kwa mchinjaji akinoe vyema kisu chake kabla ya kumlaza chini mbuzi na mfano wake.  Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamekirihisha mchinjaji kukinoa kisu chake mbele ya mnyama anayekusudiwa kuchinjwa.  Na hii ni kutokana na yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba mtu mmoja alimlaza chini kondoo anayetaka kumchinja huku akiendelea kukinoa kisu chake.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 

"أتُرِيْدُ أَنْ تُمِيْتَهَا مَوْتَاتٍ؟ هَلَّا حَدَّدْتَ شَفْرَتَكَ قَبْلَ أَنْ تَضْجَعَهَا؟"

 

“Hivi wataka kumuua mauti mengi?  Kwa nini basi usinoe kisu chako kabla ya kumlaza chali?”  [Imekharijiwa na Al-Haakim (4/257), Al-Bayhaqiy (9/280), na ‘Abdurraaziq (8608).   Wamekhitilafiana katika kuwa Hadiyth hii ni Mawswuul au Mursal].

 

 

2-   Mnyama alazwe chali

 

Hili linakuwa ni la huruma zaidi kwake, nalo limekubaliwa na Waislamu wote.  Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah:

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمَرَ بِكَبْشٍ أَقْرَنَ يَطَأُ فِي سَوَادٍ وَيَبْرَكُ فِي سَوَادٍ وَيَنْظُرُ فِي سَوَادٍ فَأُتِيَ بِهِ لِيُضَحِّيَ بِهِ فَقَالَ لَهَا : يَا عَائِشَةُ هَلُمِّي الْمُدْيَةَ ، ثُمَّ قَالَ : اشْحَذِيهَا بِحَجَرٍ ، فَفَعَلَتْ ثُمَّ أَخَذَهَا وَأَخَذَ الْكَبْشَ فَأَضْجَعَهُ ، ثُمَّ ذَبَحَهُ ، ثُمَّ قَالَ : بِسْمِ اللَّهِ ، اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنْ مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ وَمِنْ أُمَّةِ مُحَمَّدٍ ،  ثُمَّ ضَحَّى بِهِ."

 

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza beberu la kondoo mwenye pembe, mwenye miguu myeusi, mwenye tumbo jeusi, na mwenye macho meusi.  Akaletewa ili amchinje (kwa udhwhiya). Akamwambia:  Ee ‘Aaishah!  Niletee kisu.  Kisha akamwambia:  Kinoe kwa jiwe. ‘Aaishah akakinoa, Rasuli akakichukua, akamkamata beberu, kisha akamchinja huku akisema:  Bismil Laah.  Ee Allaah!  Mtakabalie Muhammad, na familia ya Muhammad, na ummah wa Muhammad”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1967) na wengineo.  Itakuja kwenye mlango wa kuchinja wanyama wa swadaqah].

 

Kumlaza kunakuwa ni kwa ubavu wake wa kushoto, kwa vile inakuwa ni wepesi kwa mchinjaji katika kukikamata kisu kwa mkono wake wa kulia, na kukikamata kichwa cha mnyama kwa mkono wake wa kushoto.

 

 

3-  Mchinjaji aweke mguu wake kwenye ubapa wa shingo ya mnyama

 

Anas amesema:

 

"ضَحَّى رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ ، فَرَأَيْتُهُ وَاضِعًا قَدَمَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا يُسَمِّي وَيُكَبِّرُ، فَذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ‏."

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja beberu wawili wenye rangi mseto ya weupe na weusi.  Nikamwona akiuweka mguu wake juu ya bapa za shingo zao huku akipiga Bismil Laahi na kutamka takbiyr. Akawachinja wote wawili kwa mkono wake”.  [Hadiyth Swahiyh.   Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5558), na itakuja mbeleni].

 

An Nawawiy kasema:  “Bila shaka alifanya hivi ili awe katika hali ya uimara na kujimudu zaidi, na ili pia mnyama asiweze kufanya matata kwa kichwa chake na hivyo kumzuia kukamilisha zoezi au hata kumjeruhi yeye”.

 

 

 

4-  Mnyama aelekezwe Qiblah

 

Kuelekezwa kunakuwa ni kwa machinjio yake na si kwa uso wake.  Jaabir bin ‘Abdillaah amesema:

 

"ذَبَحَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ الذَّبْحِ كَبْشَيْنِ أَقْرَنَيْنِ أَمْلَحَيْنِ مُوْجِئَيْن فَلَمَّا َوجَّهَهُمَا قَالَ: إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِيْ فَطَرَ السَّمَوَاتِ وَالْأَرْضَ ، عَلَى مِلَّةِ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ،  وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ، إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ، وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ ، اللَّهُمَّ مِنْكَ وَلَكَ عَنْ مُحَمَّدٍ وَأُمَّتِهِ ، بِسْمِ اللَّهِ وَاللَّهُ أَكْبَرُ ، ثُمَّ ذَبَحَ"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja siku ya kuchinja kondoo wawili madume, wenye pembe, wenye rangi nyeupe na nyeusi na waliohasiwa.  Alipowaelekeza (Qiblah) alisema:  Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa Yule Aliyeziumba mbingu na ardhi, juu ya mila ya Ibraahiym aliyejiengua na shirki, na mimi si katika washirikina.  Hakika swala yangu, ibada zangu, uhai wangu na kufa kwangu, yote hayo ni ya Allaah, Mola wa walimwengu Asiye na mshirika.   Hayo ndiyo niliyoamrishwa kuyafanya, na mimi ni katika Waislamu.  Ee Allaah, hii inatoka Kwako na ni Yako, toka kwa Muhammad na umati wake.   Kwa Jina la Allaah, na Allaah Ni Mkubwa”.  Kisha akachinja”.   [Al Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2778) na wengineo.   Angalia Al-‘Ilal cha Ibn Abiy Haatim (2/39,44) na Ad-Daaraqutwniy (7/20)].

 

Na toka kwa Naafi’i, kwamba Ibn ‘Umar:

 

"كَانَ هُوَ يَنْحَرُ هَدْيَهُ بِيَدِهِ يَصِفُهُنَّ قِيَامًا وَيُوَجِّهُهُنَّ إِلَى الْقِبْلَةِ ، ثُمَّ يَأْكُلُ وَيُطْعِمُ"

 

“Alikuwa akiwachinja wanyama wake wa (udhwhiya) kwa mkono wake, anawasimamisha na anawaelekeza Qiblah, kisha anakula na kugawa nyama”.

 

Angalizo:

 

Kumwelekeza mnyama Qiblah si sharti la lazima katika kuchinja.  Na kama kungekuwa lazima, basi Allaah Ta’aalaa Asingelisahau kulibainisha hilo.  Ni jambo linalopendeza tu.

 

 

5, 6 –  Mchinjaji apige Bismil Laah na alete Takbiyr

 

Katika Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomlaza kondoo dume chini, alisema:  Bismil Laah.  [Imetajwa nyuma kidogo].

 

Na pia katika Hadiyth ya Anas:

 

"فَرَأَيْتُهُ وَاضِعًا قَدَمَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا يُسَمِّي وَيُكَبِّرُ ، فَذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ‏.‏"

 

“Nikamwona akiuweka mguu wake juu ya bapa za shingo zao huku akipiga Bismil Laahi na kutamka takbiyr, na akawachinja kwa mkono wake”.  [Imetajwa nyuma kidogo].

 

Vile vile, Hadiyth ya Jaabir iliyotajwa nyuma kidogo kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"بِسْمِ اللَّهِ وَاللَّهُ أَكْبَرُ ، ثُمَّ ذَبَحَ."

 

“Kwa Jina la Allaah, na Allaah Ni Mkubwa”.  Kisha akachinja”.  [Imetajwa punde kidogo].

 

 

 

 

Share