002-Al-Baqarah: Utangulizi Wa Suwrah

 

002-Al-Baqarah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Ya Aayah: 286

 

Jina La Suwrah Al-Baqarah:

 

Suwrah imeitwa Al-Baqarah (Ng’ombe), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila za Suwrah. Na pia kwa kutajwa kwake katika Aayah namba (67).  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kulithibitisha jambo la ukhalifa (urithisaji wa kutawala) katika ardhi, kwa kuusimamisha Uislamu, na watu wote kunyenyekea kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na kuchukua tahadhari juu ya hali iliyowatokea Bani Israaiyl. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuelezea baadhi ya sifa za wanafiki.

 

3-Kuelezea baadhi ya sifa za Mayahudi katika itikadi zao, na katika kuasi amri za Allaah na Rasuli wao, na mengineyo waliyoyafanyia inadi.

 

4-Kubainisha umuhmu wa ‘Aqiydah na kubainisha misingi yake.

 

5-Kubainisha dalili zenye kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake wa kila kitu, na hoja za wazi kabisa za kuthibitisha kufufuliwa.

 

6-Kubainisha baadhi ya Sharia za Kiislamu katika ibaada mbalimbali, maswala ya ndoa, na miamala ya kifedha, au adhabu kutokana na makosa mbalimbali, yasiyokuwa hayo.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama  الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya namba (2:1). Kisha ikathibitisha kwamba Qur-aan haina shaka ndani yake, na kwamba ni mwongozo, na kuwasifu Waumini wanaomkhofu Rabb wao kwa ghaibu, na wanaosimamisha Swalaah na kutoa Zakaah. Pia wanaoamini yote Aliyoyateremsha Allaah, na wanoamini Siku ya Mwisho, kisha wakabashiriwa kuwa hao ndio waliohidiwa na waliofaulu.

 

2-Imebainisha aina za watu, ambao ni Waumini, makafiri na wanafiki na zimetajwa baadhi ya kufru na uasi wao.

 

3-Wameusiwa watu wote kumuabudu Rabb wao, na zikatajwa dalili zinazothibitisha kuwa Anaestahiki kuabudiwa ni Allaah Pekee, na kuwapa tahadhari watakaoabudu ghairi ya Allaah. Kisha Waumini wamebashiriwa Jannaat za kudumu walizoandaliwa na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

4-Imetajwa majadiliano kati ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Malaika kuhusu Kumuumba Nabiy Aadam (عليه السّلام), na Aadam kupewa ukhalifa hapa ardhini, na jinsi Ibliys alivyokataa amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) kumsujudia Aadam na kumshawishi kwake Aadam akamtelezesha, na tawbah ya  Aadam (عليه السّلام).

 

5-Imetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na kufadhilishwa kwa wana wa Israaiyl katika hali kadhaa, kama kuokolewa na mateso ya Firawni, kuwekewa kivuli, kuteremshiwa al-manna na as-salwaa na kadhaalika. Na imetajwa baadhi ya maasi yao, na inda zao za kutaka kumuona Allaah waziwazi. Imetajwa pia shirki zao za kumwabudu ndama, na zikatajwa baadhi ya adhabu zao.

 

6-Kimetajwa kisa cha Al-Baqarah (Ng’ombe) na imebainishwa Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa kuhuisha na kufisha.

 

7-Wamebashiriwa adhabu watu wa Kitabu kutokana na kubadilisha Maneno ya Allaah kwa kutaka manufaa ya dunia, na kukanusha Kitabu cha Allaah kwa kujitenga nacho na kumkanusha Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

8-Wamebashiriwa adhabu wana wa Israaiyl  kwa kuvunja kwao baadhi ya ahadi na fungamano kadhaa walizofungamana na Allaah, na kuamini kwao sehemu ya Kitabu na kukanusha mengineyo. Pia uasi wao wa kuwakanusha na kuwaua baadhi ya Rusuli. Pia kuasi kwao katika mambo kadhaa, na kukhiari kwao uhai wa dunia.

 

9-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemwambia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), awaambie waliomfanyia uadui Jibriyl (عليه السّلام), watambue kwamba yeye ndiye aliyeiteremsha Qur-aan kwake (صلى الله عليه وآله وسلم). Hivyo basi, kumfanyia kwao uadui Allaah na Rusuli Wake, na Malaika Wake khasa Malaika wawili Jibriyl na Miykaaiyl, kwamba wao ni maadui wa Allaah. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akamliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kuthibitisha kuwa Qur-aan ni ya haki na imetoka Kwake.

 

10-Imetolewa tahadharisho la kuwafuata mashaytwaan wanaofundisha watu uchawi (2:102), na la kufuata twaghuti (2:256-257).

 

11-Allaah (سبحانه وتعالى) Amefichua chuki na uhasidi wa waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manaswara), kuchukia kheri na Fadhila za Allaah Alizomteremshia Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), na kwamba wanatamani Waislamu wawe makafiri kama wao.   

 

12-Radd kwa makafiri kumsingizia Allaah kuwa kajichukulia mwana, ilhali Allaah Ametakasika na hayo!

 

13-Imetanabahishwa kwamba watu waliopewa Kitabu hawataridhia mpaka Waislamu wafuate mila zao, na wameonywa Waislamu kutokuwafuata au kufuata matamanio yao, bali wameamrishwa wathibitike katika Dini ya haki.

 

14-Imetajwa Allaah kumtahini Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kwa maneno. Na kuhusu ujenzi wa Al-Ka’bah alipojenga Nabiy Ibraahiym na mwanawe Ismaa’iyl, na du’aa walizoziomba kuwaombea vizazi vyao, na kumuomba Allaah Awapelekee Rasuli atakayewasomea Aayah Zake, na kuwafunza Hikma na kuwatakasa.

 

15-Imetajwa wasia wa Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kwa wanawe, kisha Ya’quwb (عليه السّلام) kuwausia watoto wake watahadhari na wathibitike katika Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) hadi kufariki kwao.

 

16-Waislamu wamefaridhishwa Swibghah (Dini) ya Allaah yenye kuwaongoza katika ‘Aqiydah sahihi na mwenendo mzuri upasao wa Kiislamu. Rejea faida katika Aayah namba (138).

 

17-Suwrah hii imetaja faradhi zote za Muislamu (Shahaada, Swalaah, Zakaah, Swawm na Hajj). Hizi zimetajwa katika sehemu mbalimbali za Suwrah, kuanzia mwanzo wake na kwengineko. Pia, Suwrah imedhihirisha Sharia nyingi upande wa ibaada, yanayohusiana na Swalaah kama umuhimu wa kusimamisha Swalaah, na Qiblah cha Waislamu. Swawm na kuteremshwa Qur-aan ndani ya Ramadhwaan. Pia baadhi ya hukmu za Hajj.

 

18-Imedhihirishwa  miamala, kadhaa kama  mas-ala ya kisasi, uharamu wa riba kisha baada ya haramisho la riba ikafuatia Aayah ya mwisho kabisa kuteremshwa katika Qur-aan. (2:281). Pia miamala ya deni na Aayah ya deni ikawa ni Aayah ndefu zaidi kuliko Aayah zote katika Qur-aan. Pia miamala ya rehani na mengineyo. Na katika upande wa familia, mambo ya ndoa, talaka, hedhi, eda, mama kumnyonyesha mwanawe, viapo (vya kujitenga na wake zao) na hukmu nyenginezo.

 

19-Suwrah imeweka wazi matukio ya kuhuisha wafu ambayo yanadhihirisha  Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa Kufufua wafu. Miongoni mwa hayo, ni kisa cha aliyeuwawa katika Bani Israaiyl na kuhusiana na Al-Baqarah (ng’ombe). Kisa cha wale waliokufa kwa radi. Kisa cha wale waliotoka katika majumba yao wakiwa maelfu kwa maelfu ilihali wanaogopa kufa Allaah (سبحانه وتعالى) Akawafisha kisha Akawafufua. Kisa cha yule aliyepita kwenye kijiji kikiwa magofu matupu, Allaah (سبحانه وتعالى) Akamfisha miaka mia kisha Akamfufua (2:259). Na kisa cha Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) na ndege waliokatwa vipande vipande na jinsi Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyowafufua ndege hao kwa Kuunga vipande hivyo na mbele ya macho yake (2:260). 

 

20-Wametahadharishwa watu kutokumfuata shaytwaan anayeelekeza katika uasi na machafu.

 

21-Wamebashiriwa Waja wa Allaah (سبحانه وتعالى) ambao wamejaaliwa hikma kwa kunena na kutenda yaliyo haki, kwamba hao wamejaaliwa kheri nyingi mno.

 

22-Imeelezea pia kisa cha Twaalutw na Jaalutw wakiwa pamoja na watukufu katika Bani Israaiyl baada ya Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na ikadhihirisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) ya kuwapa ushindi waja wake wema kama Nabiy Daawuwd (عليه السّلام) katika kisa hicho cha Twaalutw na Jaalutw.

 

23-Imetajwa Aayah tukufu kabisa ambayo ni Aayatul-Kursiy. Na wakatahadharishwa Waislamu kutokumfuata twaghuti wasije kutoka katika nuru wakaingia vizani.

 

24-Imeelezea kisa cha mfalme Nimruwdh aliyehojiana na Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kuhusu Rabb wake, akaangamizwa kwa kutakabari kwake kujifanya yeye ndiye mwenye uwezo wa kuhuisha na kufisha. 
 

25-Imetajwa utoaji wa swadaqa kwa wingi na fadhila zake, na Allaah Akapiga mfano wa asiyetoa swadaqa na khasara zake. Na Waumini wameamrishwa kutoa vilivyo vizuri badala ya kutoa vilivyoharibika katika rizki za Allaah Alizomjaalia mtu. Na pia wamesifiwa wanaojizuia kuomba omba.

 

26-Imetaja uharamisho wa riba na ikatajwa Aayah ya mwisho kuteremshwa ambayo ni Aayah namba (281).

 

27-Imetajwa Aayah ndefu kabisa katika Qur-aan, nayo ni Aayah ya deni, Aayah namba (282).

 

28-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa Aayah mbili ambazo zina fadhila adimu kama ilivyothibiti katika Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Fadhila za Suwrah:  

 

Hadiyth mbalimbali zimethibiti, miongoni mwazo ni:

 

1-Atakayesoma Usiku Aayah Mbili Za Mwisho Zinamtosheleza:

 

حَدَّثَنَا عُمَرُ بْنُ حَفْصٍ، حَدَّثَنَا أَبِي، حَدَّثَنَا الأَعْمَشُ، قَالَ حَدَّثَنِي إِبْرَاهِيمُ، عَنْ عَلْقَمَةَ، وَعَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ يَزِيدَ، عَنْ أَبِي مَسْعُودٍ الأَنْصَارِيِّ، قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ الآيَتَانِ مِنْ آخِرِ سُورَةِ الْبَقَرَةِ مَنْ قَرَأَ بِهِمَا فِي لَيْلَةٍ كَفَتَاهُ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Abuu Mas‘uwd Al-Answaariyy: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesoma usiku Aayah mbili za mwisho wa Suwratul-Baqarah zitamtosheleza.” Yaani: zinamtosheleza kumkinga na kila baya na kila lenye kumdhuru. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

2-Shaytwaan Haingii Nyumba Inayosomwa Suwrah Al-Baqarah:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ لاَ تَجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ مَقَابِرَ وَإِنَّ الْبَيْتَ الَّذِي تُقْرَأُ فِيهِ الْبَقَرَةُ لاَ يَدْخُلُهُ الشَّيْطَانُ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Msifanye nyumba zenu makaburi. Kwa hakika shaytwaan haingii nyumba ambayo husomwa humo Suwratul-Baqarah.” [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Swahiyh] Na katika Riwaayah ya Muslim, Hadiyth (780): “Shaytwaan anakimbia nyumba inayosomwa ndani yake Suwratul-Baqarah.”

 

عن سَهْل بن سعد قال: قال رسولُ الله  صلى الله عليه وآله وسلم : إِنَّ لِكُلِّ شَيْءٍ سَنَامًا، وَإِنَّ سَنَامَ القُرْآنِ سُورَةُ الْبَقَرَةِ، مَنْ قَرَأَهَا فِي بَيْتِهِ لَيْلًا لَمْ يَدْخُلِ الشَّيْطَانُ بَيْتَهُ ثَلَاثَ لَيَالٍ، وَمَنْ قَرَأَهَا نَهَارًا لَمْ يَدْخُلِ الشَّيْطَانُ بَيْتَهُ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ

 

Amesimulia Sahl bin Sa’d (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kila kitu kina kinara, na Al-Baqarah ndio kinara cha Qur-aan. Atakayesoma Al-Baqarah usiku nyumbani kwake, shaytwaan hatoingia ndani ya nyumba yake nyusiku tatu. Na atakayesoma mchana ndani ya nyumba yake, shaytwaan hatoingia ndani ya nyumba hiyo kwa siku tatu.[Atw-Twabaraaniy (6/163), Ibn Hibbaan (2/78) na Ibn Mardawayh, Swahiyh At-Targhiyb (2/314)]

 

3-Suwrah Al-Baqarah Ni Taa Mbili Zitakazomuombea Mtu Siku Ya Qiyaamah, Na Kushikamana Nayo Ni Baraka, Kuicha Ni Majuto, Na Wachawi Hawaiwezi: 

 

عن ابي أُمَامَةَ الْبَاهِلِيُّ قَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ ‏ "‏ اقْرَءُوا الْقُرْآنَ فَإِنَّهُ يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ شَفِيعًا لأَصْحَابِهِ اقْرَءُوا الزَّهْرَاوَيْنِ الْبَقَرَةَ وَسُورَةَ آلِ عِمْرَانَ فَإِنَّهُمَا تَأْتِيَانِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كَأَنَّهُمَا غَمَامَتَانِ أَوْ كَأَنَّهُمَا غَيَايَتَانِ أَوْ كَأَنَّهُمَا فِرْقَانِ مِنْ طَيْرٍ صَوَافَّ تُحَاجَّانِ عَنْ أَصْحَابِهِمَا اقْرَءُوا سُورَةَ الْبَقَرَةِ فَإِنَّ أَخْذَهَا بَرَكَةٌ وَتَرْكَهَا حَسْرَةٌ وَلاَ تَسْتَطِيعُهَا الْبَطَلَةُ ‏"‏.‏ قَالَ مُعَاوِيَةُ بَلَغَنِي أَنَّ الْبَطَلَةَ السَّحَرَةُ ‏.‏

Amesimulia Abuu Umaamah Al-Baahiliy (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Someni Qur-aan kwani itakuja Siku ya Qiyaamah ikiwa ni shafaa’ah (kiombezi) kwa watu wake wanaoisoma na kutekeleza (amri zake). Someni taa mbili: Al-Baqarah na Aal-‘Imraan kwani zitakuja Siku ya Qiyaamah kama kwamba ni maumbile ya mawingu, au sehemu mbili za mawingu, au makundi mawili ya ndege waliotandaza mbawa zao wakiruka. Zitawatetea watu wake (walioshikamana nazo) siku hiyo. Someni Suwratul-Baqarah, kwani kushikamana nayo ni baraka, na kuiacha kwake ni majuto, na wachawi hawawezi kuihifadhi kwa moyo.” [Muslim (804)] 

 

Rejea pia Utangulizi wa Suwrah Aal-‘Imraan kupata fadhila nyenginezo zinazohusiana na Suwrah hii ya Al-Baqarah.

 

Faida:  

 

Suwrah hii ni Suwrah ndefu kabisa kuliko Suwrah zote za Qur-aan. Ndani yake kuna hukmu za faradhi kadhaa kama Swalaah, Swiyaam za Ramadhwaan, Hajj, na hukmu nyenginezo ambazo Waislamu wanazihitaji katika maisha yao ya kijamii ya kila siku.

 

Pia zimetajwa maudhui mbalimbali, pamoja visa kadhaa, vikiwemo visa vyenye kudalilisha  miujiza ya Allaah na Uwezo Wake wa kuhuisha na kufisha. Kisa kimojawapi ni kisa cha Al-Baqarah (Ng’ombe), ambacho ni kuhusu mtu aliyemuua mwenzie zama za Nabiy Muwsaa (عليه السّلام), ikawa hakujulikana nani aliyemuua mtu huyo. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaamrisha wana wa Israaiyl wamchinje ng’ombe, kisha wampige maiti huyo kwa kipande cha sehemu ya ng’ombe. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akumhuisha mtu huyo, nae akawa hai na akataja mtu aliyemuua. Na hii ni ushahidi wa Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni Muweza wa kufufua wafu baada ya kufa kwao na Muweza wa kila kitu. Rejea Aayah (67-73).

 

Na katika kutofautisha na Suwrah nyenginezo, ni kuweko ndani yake Aayatul-Kursiyy ambayo ni Aayah Tukufu kabisa ya Qur-aan. Pia Aayah mbili za mwisho wa Suwrah, ambazo amepewa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) pekee katika Manabii, alipokuwa mbingu ya saba katika Safari ya Al-Israa na Al-Mi’raaj.   

 

 

 

Share