009-At-Tawbah: Utangulizi Wa Suwrah

 

009-At-Tawbah:  Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 129

 

Jina La Suwrah: At-Tawbah:

 

Suwrah imeitwa At-Tawbah (Kutubia), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Faida namba (1). Na kutokana na Allaah (سبحانه وتعالى) Kupokea tawbah ya Nabiy na Muhaajiruwna na Answaar na pia Amepokea Tawbah ya Swahaba watatu waliotubia baada ya makosa yao kutokwenda vita vya Jihaad vya Tabuwk. Rejea Aaya (117-118). Pia kutokana na neno hili kukariri katika Aayah kadhaa za Suwrah hii. 

 

Inajulikana pia kama Suwrah Al-Baraa-ah kutokana na Hadiyth:

 

حَدَّثَنَا سُلَيْمَانُ بْنُ حَرْبٍ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، سَمِعْتُ الْبَرَاءَ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ آخِرُ سُورَةٍ نَزَلَتْ بَرَاءَةَ .

Amesimulia Al-Baraa (رضي الله عنه): Suwrah ya mwisho kuteremka ni Baraa-ah. [Al-Bukhaariy Kitaab At-Tafsiyr]

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Utakaso kutokana na wanafiki na washirikina, na (kwamba inafaa kuwapiga) Jihaad hao, na kufungua mlango wa tawbah kwa watakaotubia.

[Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuweka mchoro wa njia ambayo wanalazimika kuipita hiyo Waumini katika mahusiano yao pamoja na washirikina, na pamoja na Ahlul-Kitaab na wanafiki.

 

3-Kuwakashifu wanafiki na matendo yao, na kuwafedhehesha mbele ya jamii ya Kiislamu.

 

4-Kubainisha hukmu nyingi na miongozo ambayo inatakiwa kufuatwa kwa dola changa (inayoanza).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kukumbushwa kujiweka mbali na kujitakasa na washirikina, na amri ya kuwapiga vita kwa sababu ya kuvunja ahadi zao, na kuwazuia kuingia Masjidul-Haraam. Makatazo ya kutokuwapenda washirikina hata kama watakuwa ndugu wa karibu.

 

2-Kuna ishara ya kutokea kwa Vita vya Hunayn, na kuzilea nafsi za Waumini juu ya ukweli wa kumtegemea Allaah (سبحانه وتعالى).

 

3-Imewatangazia vita Ahlul-Kitaab mpaka walipe kodi, na kwamba wao hawako mbali sana na washirikina, na kwamba mali zao wala nguvu zao hazitawafaa.

 

4-Radd kwa kauli za Manasawara na Mayahudi juu ya dhulma kubwa ya kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Uzayr na Nabiy ‘Iysaa ni wana wa Allaah.

 

5-Imetiliwa msisitizo Risala ya haki ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

6-Wasomi wa Kiyahudi wamekemewa katika kula kwao mali za watu kwa baatwil.

 

7-Imetajwa heshima ya miezi mitukufu, na kudhibiti kwa miaka ya kisharia, na kubatilisha kuichelewesha miezi (kuibadilisha miezi mitukufu kuiweka si mahala pake), kama ilivyokuwa tabia za Kijaahiliyyah.

 

8-Kuna mahimizo ya Jihaad na kuwataka watu wajitolee kwa mali na nafsi zao, na kutoielemea dunia na mapambo yake.

 

9-Imeelezwa Nusrah ya Allaah kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa na swahibu yake (Abubakar Asw-Swidddiyq), na jinsi Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyowahami kutoonekana na makafiri katika pango.

 

10-Zimetajwa sifa za wanafiki na tabia zao za kuwafanyia vitimbi Waislamu, na kumuudhi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa maneno na matendo, na kuamrisha kwao maovu na kukataza wema.   

 

11-Imetajwa ujenzi wa Masjid Dhwiraar uliojengwa na wanafiki kwa lengo la uharibifu, na vitimbi vya wanafiki kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

12-Imetajwa ujenzi wa Masjid Qubaa uliojengwa kwa lengo la Taqwa na kumtii Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba Msikiti huo ndio bora zaidi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasimame na kuswali hapo.

 

13-Kuna makatazo ya kuwaombea washirikina maghfirah hata kama ni wenye uhusiano wa damu.

 

14-Imetajwa kukubaliwa kwa tawbah ya wale waliokhalifu (wasioenda) katika Vita vya Tabuwk.

 

15-Kuna mahimizo ya kutafuta ilimu ya Dini ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kuibalighisha Dini kwa watu.

 

16-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa sifa nyengineyo ya wanafiki kwamba inapoteremshwa Suwrah, wanafiki huashiriana kwa macho, kwa kuchukia kuteremka kwake kwa sababu ya kutajwa aibu zao na matendo yao, kisha huondoka kuogopa fedheha. Na mwishowe Waislamu wamekumbushwa neema ya Allaah kwao, ambayo ni kutumiwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na wao; Nabiy ambaye anawajali Waislamu, na huruma zake juu yao.  

 

Faida:

 

1-Suwrah At-Tawbah ni Suwrah ya fedheha kwa sababu ya kufichuliwa maovu ya makafiri na wanafiki:

 

 عَنْ سَعِيدِ بْنِ جُبَيْرٍ، قَالَ قُلْتُ لاِبْنِ عَبَّاسٍ سُورَةُ التَّوْبَةِ قَالَ التَّوْبَةُ هِيَ الْفَاضِحَةُ، مَا زَالَتْ تَنْزِلُ وَمِنْهُمْ وَمِنْهُمْ، حَتَّى ظَنُّوا أَنَّهَا لَمْ تُبْقِ أَحَدًا مِنْهُمْ إِلاَّ ذُكِرَ فِيهَا‏.‏ قَالَ قُلْتُ سُورَةُ الأَنْفَالِ‏.‏ قَالَ نَزَلَتْ فِي بَدْرٍ‏.‏ قَالَ قُلْتُ سُورَةُ الْحَشْرِ‏.‏ قَالَ نَزَلَتْ فِي بَنِي النَّضِيرِ‏.‏

Amesimulia Sa’iyd Bin Jubayr: Nilimuuliza Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nini Suwrah At-Tawbah? Akasema At-Tawbah ni fedheha (yaani Suwrah inayofichua maovu yote ya makafiri na wanafiki). Na iliendelea kuteremka; Wa minhum, wa minhum (na miongoni mwao, na miongoni mwao), mpaka wakadhani kuwa Suwrah hiyo haikubakisha hata mtu mmoja isipokuwa atakuwa ametajwa humo.” Nikamuuliza: Nini kuhusu Suwrah Al-Anfaal? Akanijibu “Imeteremka kuhusu Badr.” Nikamuuliza: Suwrah Al-Hashr?   Akasema “Imeteremka kuhusiana na Bani Nadhiyr.” [Al-Bukhaariy Kitaab At-Tafsiyr]

 

 

2-Aayah mbili za mwisho za Suwrah At-Tawbah zimepatikana kwa Abuu Khuzaymah Al-Answaariyy (رضي الله عنه):

 

  عَنِ ابْنِ السَّبَّاقِ، أَنَّ زَيْدَ بْنَ ثَابِتٍ، حَدَّثَهُ قَالَ أَرْسَلَ إِلَىَّ أَبُو بَكْرٍ فَتَتَبَّعْتُ الْقُرْآنَ حَتَّى وَجَدْتُ آخِرَ سُورَةِ التَّوْبَةِ مَعَ أَبِي خُزَيْمَةَ الأَنْصَارِيِّ لَمْ أَجِدْهَا مَعَ أَحَدٍ غَيْرِهِ  لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِنْ أَنْفُسِكُمْ  حَتَّى خَاتِمَةِ بَرَاءَةٌ‏.‏ حَدَّثَنَا يَحْيَى بْنُ بُكَيْرٍ، حَدَّثَنَا اللَّيْثُ، عَنْ يُونُسَ، بِهَذَا وَقَالَ مَعَ أَبِي خُزَيْمَةَ الأَنْصَارِيِّ‏.‏

Amesimulia ‘Ubayd bin As-Sabbaaq (رضي الله عنه): Zayd bin Thaabit (رضي الله عنه) amesema: Abu Bakr (رضي الله عنه) alimtuma mtu kuniita. Hivo nikaanza kuikusanya Qur-aan mpaka nikaipata sehemu ya mwisho ya Suwrah At-Tawbah kutoka kwa Abuu Khuzaymah Al-Answaariyy (رضي الله عنه), na haikupatikana kutoka kwa mtu mwengine yeyote. (Aayah zenyewe ni):

 

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ  

“Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe.”

 

mpaka mwisho wa Suwrah [At-Tawbah (9:128-129) – Hadiyth Ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]

 

 

 

Share