011-Huwd: Utangulizi Wa Suwrah

 

011-Huwd: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 123

 

Jina La Suwrah: Huwd

 

Suwrah imeitwa Huwd, na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini kwenye Faida. Na imeitwa Huwd kutokana na kisa cha Nabiy Huwd (عليه السّلام) kwa kaumu yake ya ‘Aad ingawa pia kisa chake kimetajwa katika Suwrah nyenginezo. Rejea Aayah (50-60).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumpa thabati Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) (na kumliwaza) pamoja na Waumini kwa visa vya waliotangulia, na makemeo makali kwa wenye kukadhibisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Uthibitisho wa daawah ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na kuthibitisha misingi ya imaan ya Kiislam ya Tawhiyd ya Allaah.

 

3-Kubashiria na kuonya shirki na maovu, na kukumbushwa viumbe malipo ya mema na maovu Siku ya  Qiyaamah. 

 

4-Kubainishwa Desturi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwaadhibu na kuwaangamiza makafiri wa nyumati zilizopita, na kutajwa sababu za dhulma kwamba, wengi wao walifuata starehe na matamanio yaliyopelekea kwenye uasherati, dhulma, ubadhirifu, ufisadi na kuwafanyia dhihaka Rusuli wa Allaah.

 

5-Kumthitibisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na Waumini wabakie imara katika Dini kwa kutolewa kisa cha Nabiy Nuwh (عليه السّلام), kwamba mapenzi yake kwa mwanawe ni tabia ya kibinaadam, na kwamba kuna mipaka ya sharia katika haki za baina ya mzazi na mwana katika kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imebainishwa kwamba Qur-aan ni Aayah zilizofasiliwa waziwazi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), ikafuatilia kutaja fadhila za Istighfaar. Rejea Aayah namba (3).

 

2-Imebainishwa kwamba, Allaah (سبحانه وتعالى) Anazitambua siri za viumbe wote na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anadhamini rizki zote za viumbe.

 

3-Imethibitishwa kufufuliwa na jazaa (malipo) ya mema na maovu.

 

4-Imebainishwa hali za watu katika shida na raha.

 

5-Imemthibitisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumliwaza juu ya maudhi ya watu wake; washirikina wa Makkah.

 

6-Imebainishwa makundi ya makafiri na Waumini, na kuyapigia mifano.

 

7-Vimetajwa sehemu ya visa vya Manabii, na kuchambua baadhi ya matukio yao, na yale yaliyojiri pamoja na watu wao, kama vile kisa cha Nuwh, Huwd, Swaalih, Ibraahiym, Luutw, Shu’ayb na Muwsaa (عليهم السّلام).

 

8-Kuna muongozo juu ya yale yanayoweza kumfanya mtu aishi maisha mazuri, kama vile kuthibitika katika Dini, na kutojiegemeza kwa watu wa dhulma, na kusimamisha Swalaah.

 

9-Imebainishwa faida ya visa vya Manabii na kuwataja watoto wao kama Nabiy Nuwh (عليه السّلام) na mwanawe aliyegharikishwa. Faida kama hii, ni kwa ajili ya kuuthibitisha moyo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Waumini wanapokuwa na watu wenye uhusiaono wa damu, wanaomuasi Allaah (سبحانه وتعالى).   

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kutoa amri ya kuwataka watu watawakkal kwa Allaah kwa kila hali na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Haghafiliki na matendo yoyote yale; mema au maovu.

 

Faida:

 

 عَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ، قَالَ اتَّبَعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَهُوَ رَاكِبٌ فَوَضَعْتُ يَدِي عَلَى قَدَمِهِ فَقُلْتُ أَقْرِئْنِي يَا رَسُولَ اللَّهِ سُورَةَ هُودٍ وَسُورَةَ يُوسُفَ ‏.‏ فَقَالَ ‏"‏ لَنْ تَقْرَأَ شَيْئًا أَبْلَغَ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ

   قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَق   وَ   قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ .

Amesimulia ‘Uqbah Bin ‘Aamir (رضي الله عنه): Nilikwenda kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa amepanda kipando, nikaweka mkono wangu juu ya mguu wake, nikasema: Nifundishe Suwrah ya Huwd, nifundishe Suwrah ya Yuwsuf. Akasema: "Hutasoma kitu chochote chenye timilifu zaidi (katika kinga) mbele ya Allaah: (Soma):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾

“Sema: Najikinga na Rabb wa mapambazuko.[Al-Falaq (113)]

 

Na

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾

“Sema: Najikinga na Rabb wa watu.” [An-Naas (114)]

 

[Hadiyth katika Sunan An-Nasaaiy, Ahmad, Ibn Hibbaan, ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika Swahiyh An-Nsaaiy (5454)]

 

 

 

Share