015-Al-Hijr: Utangulizi Wa Suwrah

 

015-Al-Hijr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 99

 

Jina La Suwrah: Al-Hijr.

 

Suwrah imeitwa Al-Hijr (Eneo lilioko baina ya Sham na Hijaaz), na inayodalilisha ni kutajwa watu wa Al-Hijr katika Aayah namba (80). Hawa ni kina Thamuwd ambao walitumiwa Nabiy Swaalih (عليه السّلام) kuwalingania Tawhiyd ya Allaah.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwaahidi adhabu wale wote wanaoifanyia istihzai Qur-aan. Ahadi ya Allaah juu ya kuihifadhi Qur-aan, kwa kumuunga mkono Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumthibitisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha Uadhama wa Qur-aan kuwa ni Kitabu kinachobainisha na kuongoza katika njia ilyonyooka, na thibitisho la kuhifadhika kutokana na kubadilishwa.

 

3-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na kubainisha Uwezo Wake Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kusimamisha hoja dhidi ya makafiri kwa kueleza Aayaat (Ishara, Dalili) za mbinguni na ardhini. Pia Uwezo Wake Allaah (سبحانه وتعالى) wa Kuhuisha na Kufisha na kuthibitishwa kukusanywa kwa ajili ya kuhesabiwa matendo na malipo yao ya adhabu.      

 

4-Bainisho kwamba asili ya mwanaadam ni kutokana na udongo. Na bainisho kuhusu ushawishi na uchochezi wa shaytwaan kwa mwanaadam.

 

5-Bainisho kwamba mauti na uhai yako Mikononi mwa Allaah Pekee.

 

6-Kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumthibitisha pamoja na Waumini.  

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imewaonya  washirikina kuhusu kumzulia kwao Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa ni  majnuni (mwendawazimu) kwa sababu hakuwaletea Malaika wa kumsaidia na kuwapa khabari za Allaah (سبحانه وتعالى), ilhali Malaika hawashuki ila kwa hikma na amri ya Allaah (سبحانه وتعالى).  

 

2-Suwrah imewatahadharisha washirikina kwamba, watajutia matendo yao maovu ya kujishughulisha kwao na maisha ya dunia na kuzama kwao humo, na kutokusilimu kwao.  

 

3-Suwrah imethibitisha kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Ameteremsha Qur-aan na Ameahidi kuihifadhi kutokana na kubadilishwa au kupotoshwa Aayah zake.   

 

4-Imebainishwa  kwamba wale wanaomkadhibisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), wanamkadhibisha kwa inda, inadi na ukafiri tu, wala si kwa kukosa dalili zinazoonyesha ukweli wake (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

5-Makafiri wamesimamishiwa hoja kwa kuelezea ishara za ulimwengu zinazoashiria Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uadhimu Wake, na Qudra Yake ya Uumbaji wa mbingu na ardhi na kujaalia nyota mbinguni, na kuhifadhi vilivyomo mbinguni kwa kuwarushia vimondo mashaytwaan, na kuthibitishwa milima ardhini, na kurahisisha njia ardhini, na kujaaliwa rizki kwa kupeleka pepo za rehma zinazorutubisha na kuteremsha maji ya kumwagilia na kuihuisha ardhi, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Anayehuisha na Kufisha na watakusanywa makafiri hao Siku ya Qiyaamah kuadhibiwa.

 

6-Ukumbusho kwamba kuumbwa kwa mwanaadam ni kutokana na udongo mkavu. Na ndivyo alivyoumbwa Aadam (عليه السّلام), na kuamrishwa Malaika kumsujudia Aadam (عليه السّلام), na kuelezea kiburi cha Ibliys kukataa kumsujudia na kufukuzwa kwake Peponi.

 

7-Kumetajwa baadhi ya maelezo ya visa vya Rusuli wa Allaah, kama vile: Ibraahiym, Luutw, Shu’ayb na Swaalih (عليهم السلام).

 

8-Suwrah imewatahadharisha makafiri na moto wa Jahannam na adhabu kali za Allaah (سبحانه وتعالى), na kuwabashiria Waumini Jannah na Rehma za Allaah.  

 

9-Suwrah imekhitimishwa kwa Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kushikamana na kuendelea kubalighisha Risala Yake, wala asijali kukengeushwa na washirikina na istihzai zao, na kumliwaza  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Anatosheleza dhidi ya istihzai zao. Kisha ikamalizikia kwa amrisho la kuendelea kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) mpaka itakapomfikia yakini (mauti).

 

 

Share