006-Al-An'aam: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

006-Al-An’aam: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 165

 

Jina La Suwrah: Al-An’aam.

 

Suwrah imeitwa Al-An’aam (Wanyama), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila na Faida. Na pia imeitwa Al-An’aam (Wanyama) kutokana na kutajwa wanyama wa aina mbalimbali ambao washirikina waliwatumia kwa shirki na kufru zao na wakawa wanapotaka kuwala hawataji jina la Allaah.  

 

Na amesema Al-Swuyuutwiy: Imeitwa Suwrah Al-An’aam kwa sababu ya ufafanuzi wa hali za wanyama, japo neno Al-An’aam limekuja kwenye Suwrah isiyokuwa hii, lakini ufafanuzi uliokuja katika Aayah (142-144). [Al-Itqaanu fiy Uluwmil-Qur-aan (1/197)] Na pia Aayah (136) (138-139).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuithibitisha ‘Aqiydah ya Tawhiyd, na kuupinga upotevu wa washirikina. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuifanya Aqiydah iwe madhubuti, na kuidhoofisha na kuipinga shirki.

 

3-Kuwafahamisha watu Utukufu wa Muumba wao, na kusimamisha dalili ya kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko Peke Yake, Naye Ndiye Anayepasa kuabudiwa kwa haki.

 

4-Kuthibitisha Unabiy wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), na uhakika wa Siku ya Mwisho na malipo yake.

 

5-Kuwasimamishia hoja washirikina na watu wa bid’ah, na wale wanaokadhibisha kufufuliwa, na kuziondoa shubha ya hayo.  

 

6-Kubainisha ujahili wa washirikina.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى) na kubainisha kuwa Anayestahiki shukrani ni Yeye Allaah Pekee, kwani Yeye Ndiye Muanzilishi wa kila kilichomo ulimwenguni. Na kubatilisha athari za washirika kama vile masanamu na majini, kwa kuthibitisha kuwa Allaah Ndiye Muumba wa vyote vilivyomo ulimwenguni, na uumbaji wa binaadam na nidhamu ya maisha yake, ya kufa kwake kwa Hikma Yake Allaah (سبحانه وتعالى) na Ujuzi Wake. Na kumtakasa Allaah kutokana na kumhusisha na mke na mwana.

 

2-Kuna mawaidha kwa wale wanaopinga Aayah za Qur-aan, na wanaokadhibisha haki na Siku ya Mwisho, na kuwatisha kwamba yatawatokea kama yaliyowatokea watu (wapingaji) waliopita kabla yao, na waliozikufuru Neema za Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba kupinga kwao hakutamdhuru yeyote isipokuwa nafsi zao. Na ahadi ya adhabu zao watazikuta watakapotolewa roho zao kisha tena watakapofufuliwa.

 

3-Imetajwa sifa ya upumbavu ya washirikina kwa ile rai walioitoa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ya kumtaka alete vitu vinavyoenda kinyume na mazoea, kwa lengo la kumtingisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Na kuthitibisha uhakika wa Qur-aan na uhakika wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kwamba watu wa Kitabu wanatambua kuwa ni haki kuliko hata wanavowatambua watoto wao!  

 

4-Suwrah imetaja dalili nyingi za kuonyesha kuwa Allaah ni Mmoja na Mwenye Uwezo, na kwamba Yeye tu Ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.

 

5-Washirikina wamekemewa juu ya kupinga kwao ufufuo, na kuwathibitishia kwamba ufufuo upo na kwamba wao baada ya kufufuliwa watakuja kuadhibiwa. Na kwamba waabudiwa wao waliokuwa wakiwaabudu watawakana na watawatenga Siku hiyo, na watakuja kujuta kwa hilo, na wala haiwafai kitu katika maisha ya dunia kwani hawaombi kwa yeyote isipokuwa Allaah wakati wa majanga.

 

6-Imetajwa mateso ya washirikina na madhalimu kutokana shirki na kufru zao; mateso pale wanapotolewa roho zao na jinsi watakapohudhurishwa motoni. Miongoni mwao ni wale waliodai kuwa wameteremshiwa Wahyi ilhali ni uongo mkubwa kwani hakuna Nabii baada ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). Pia imetajwa hali zao watakapofufuliwa na watakapokana shirki zao.  

 

7-Kwenye Suwrah kuna kiliwazo kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuuthibitisha moyo wake, na kumlingania kuwa na subra kwa kuvumilia changamoto za Urasuli bila kuhisi uchovu wala uvivu, na ni mwongozo juu ya kuwaiga Rusuli waliopita kabla yake, ambao walisubiri pamoja na kupingwa na watu wao.

 

8-Imebainishwa Hikma ya Allaah juu ya kuwatuma Rusuli, na kwamba hikma kubwa ni kuwabashiria na kuwaonya watu, na wala kazi za Rusuli si kuwafahamisha watu mambo ya ghaibu.

 

9-Imebainishwa kwamba Allaah Pekee Ndiye Anayehusika kutambua ghaibu.

 

10-Suwrah imewabainisha wale ambao wanaweza kuitikia na kujibu daawah ya haki, kuwa ni wale wanaosikiliza na kukubali mawaidha. Ni wale ambao nyoyo zao ziko hai, ama wale ambao nyoyo zao zimekufa hawa hawataweza kunufaika na mawaidha, na wala hawakubali mwongozo, ila watambue kuwa hatima yao ni kwa Allaah na watakuja kulipwa juu ya kufru zao na matendo yao maovu.

 

11-Imebainishwa kuwa ubora wa watu upo katika taqwa ya Allaah na kujinasibisha katika Dini ya Allaah, na kubatilisha kile walichokiweka washirikina, ambayo ni sheria ya upotovu.

 

12-Kuna makatazo juu ya kukaa na wale wanaozipuuza na kuzifanyia istihzai Aayah za Allaah, na kutokukaa kuongea nao.

 

13-Kuna amri ya kuwapuuza washirikina, na makatazo ya kuyatukana masanamu na wale wanaoyaabudia ili wasilipize kumtukana Allaah (سبحانه وتعالى).

 

14-Suwrah pia imebainisha kwamba taqwa ya kweli haipatikani kwa mtu kujinyima vitu vizuri tu, bali kwa kujinyima pia matamanio ya nafsi.

 

15-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amepigiwa mfano pamoja na watu wake, kama mfano wa Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) baba yake pamoja na watu wake, na Manabii na Rusuli wote walikuwa katika mifano hiyo, kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho. Katika Suwrah hii Manabii kumi na nane wametajwa pamoja na Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام). Rejea Aayah namba (83-86).

 

16-Zimetajwa Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kadhaa, ikiwemo neema kwa Ummah kutokana na kuteremshiwa Qur-aan yenye mwongozo kwao, kama Alivyoteremsha Kitabu kwa Muwsaa (عليه السّلام) na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amejaalia kuwa ni ummah bora wa mwisho.

 

17-Suwrah imebainisha fadhila ya Qur-aan na Dini ya Kiislam, na malipo makubwa Aliyoyaweka Allaah (سبحانه وتعالى) kwa mtu atakayeisoma.

 

18-Suwrah imetajwa Neema nyingi za Allaah (سبحانه وتعالى) ambazo zimewaenea viumbe wa Allaah (سبحانه وتعالى) kama neema za mazao mbalimbali na imetaja funguo za ghaibu.

 

19-Suwrah imeelezea sifa za Waarabu zama za Ujahiliyyah, pamoja na kubainisha shirki na kufru zao kuhusiana na wanyama. Na Suwrah hii ya Al-An’aam ndio Suwrah pekee katika Qur-aan iliyoelezea kwa kina juu ya hilo.

 

20-Suwrah imetaja Wasia wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa maamrisho kadhaa na makatazo. Rejea Aayah (151-153).

 

21-Allaah Ametaja katika Suwrah hii ukhalifa (utawala) wa viumbe, na utofauti wa daraja zao, na Allaah (سبحانه وتعالى) Akamalizia kwa kutaja uharaka wa Adhabu Zake kwa wanaostahiki, na Rehma na Maghfirah Yake kwa wanaostahiki kupata.

 

22-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitishwa Tawhiyd ya Uluwhiyyah (Kumpwekesha Allaah katika ibaada) kama Swalaah, kuchinja. Na pia kwa kukanusha shirki. Na ikathibitishwa pia Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola; Uumbaji), na kwamba marejeo ya viumbe yatakuwa kwa Allaah Siku ya Qiyaamah ambako kutakuwa na malipo ya matendo mema na maovu, na kubainika Siku hiyo mambo yote waliyokhitilafiana watu katika Dini.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

عنِ ابنِ عبَّاسٍ رضِي اللهُ عنهما، قالَ: نزَلَتْ سورَةُ الأنعامِ بمَكَّةَ ليلًا جُملةً، حولَها سَبعونَ ألفَ مَلَكٍ، يَجأرُونَ حولَها بالتَّسبيحِ

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Suwrah nzima ya Al-An’aam imeteremshwa Makkah, usiku, ikifuatiliwa na Malaika elfu sabini wakinyanyua sauti zao kumsabihi Allaah. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Faida:

 

1-Suwrah Al-An’aam (6), ni miongoni mwa Suwrah tano zinazoanzia kwa AlhamduliLlaah. Nyenginezo ni Al-Faatihah (1), Al-Kahf (18), Saba-a (34) na Faatwir (35).

 

2-Ni Suwrah mojawapo yenye kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na kupinga shirki kwa dalili nyingi za wazi kabisa.

 

3-Suwrah inayodhihirisha ujinga wa washirikina wa Makkah kama ilivyoelezewa katika Hadiyth:

 

عنِ ابنِ عباسٍ رضي اللهُ عنهما، قالإذا سَرَّك أنْ تَعلَمَ جَهْلَ العربِ، فاقرَأْ ما فَوقَ الثَّلاثينَ ومِئَةٍ في سورةِ الأنعامِ: قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ قَتَلُوا أَوْلَادَهُمْ سَفَهًا بِغَيْرِ عِلْمٍ... إلى قولِه: قَدْ ضَلُّوا وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ

Imesimuliwa na Ibn Abbas (رضي الله عنهما) amesema: Likikufurahisha wewe kutambua ujinga wa waarabu, basi soma Aayah zilizo zaidi ya mia moja na thelathini ya Suwrah Al-An’aam:

 

 قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ قَتَلُوا أَوْلَادَهُمْ سَفَهًا بِغَيْرِ عِلْمٍ وَحَرَّمُوا مَا رَزَقَهُمُ اللَّـهُ افْتِرَاءً عَلَى اللَّـهِ ۚ قَدْ ضَلُّوا وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ ﴿١٤٠﴾

“Kwa yakini wamekhasirika wale waliowaua watoto wao kwa upumbavu bila ya ujuzi na wakaharamisha vile Alivyowaruzuku Allaah kwa kumtungia uongo Allaah. Kwa yakini wamepotea na wala hawakuwa wenye kuhidika.” [Al-An’aam (6:140)- Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]

 

4-Suwrah imeanzia Aayah ya mwanzo kwa Thanaa ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Kumhimidi na pia hapo hapo imepinga shirki kwa kumlinganisha Allaah (سبحانه وتعالى) na viumbe. Kisha Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na imepinga kumshirikisha Allaah. Rejea Aayah (161-163).

 

 

 

Share