017-Al-Israa: Utangulizi Wa Suwrah

 

017-Al-Israa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 111

 

Jina La Suwrah: Al-Israa

 

Suwrah imeitwa Al-Israa (Safari ya Usiku), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila, na kutajwa katika Aayah namba (1). Rejea pia Faida. 

 

Na imeitwa pia Suwrah Bani Israaiyl, kutokana na maelezo yaliyotajwa kuhusu Wana wa Israaiyl na ufisadi wao katika ardhi.  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Allaah (سبحانه وتعالى) kumthibitisha Rasuli wake, (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumtia nguvu kwa dalili za wazi, na kumpa bishara Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ya ushindi na kuthibiti. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuithibitisha misingi ya ‘Aqiydah ya Uislamu, na kuisafisha na kila kinachotia dosari katika Uislamu.

 

3-Kubainisha kwamba, Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka na inawabashiria Waumini ujira mtukufu na mkubwa. Na kuthibitishwa adhabu kwa wasioamini. Na kwamba malipo ya hidaaya na dhambi za upotevu humjia mtu binafsi. Na pia hakuna atakayebeba dhambi za mtu mwengine. Na kwamba Siku ya Qiyaamah, kila mtu atashuhudia mwenyewe matendo yake. 

 

4-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na kuwafanyia ihsaan wazazi wawili na kutokuwakemea hata kwa neno la uff! Rejea tanbihi ya Aayah namba (23). Pia kuwafanyia ihsaan arhaam (wenye uhusiano wa damu), walioharibikiwa safarini, kuwaonea huruma maskini na mafakiri.

 

5-Haramisho la kumshirikisha Allaah, na kufanya ubadhirifu wa mali, kukaribia zinaa, kuua na makatazo mengineyo.     

 

6-Kuthibitisha Qur-aan na kwamba ni mustahili kwa yeyote yule kuleta mfano wa Qur-aan kwani ni muujiza wa Dini Tukufu ya Kiislamu. Na pia kubainishwa kwamba Qur-aan imeteremshwa kidogo kidogo kwa hikma.

 

7-Maelezo yanayomuhusu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kubainisha misimamo ya washirikina kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

8-Kubainisha baadhi ya majukumu ya kisharia yanayoendana na tabia za kila mmoja na jamii kwa ujumla.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa muujiza wa safari ya Al-Israa na Al-Mi’raaj, ambayo ni safari ya sehemu ya usiku mmoja kuanzia Masjid Al-Haraam hadi Masjid Al-Aqswaa kisha kupanda mbinguni hadi mbingu ya saba.  

 

2-Imetajwa Kitabu ambacho Allaah alimpa Muwsaa (عليه السلام), ili kiwe mwongozo kwa watu wake, na kuwajulisha Bani Israaiyl kuwa watafanya uharibifu katika ardhi mara mbili.

 

3-Imebainisha fadhila za Qur-aan, na kwamba inaongoza kwenye jambo zuri zaidi, na inawabashiria Waumini kuwa watapata malipo makubwa.

 

4-Imethibitisha dalili ya kuwa Allaah Pekee Ndiye Anaepasa kuabudiwa. Imetaja dalili ya uwepo wa usiku na mchana na kwamba kuna faida nyingi kwa mwanaadam.

 

5-Imebainisha Desturi ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya maangamizo kwa watu wa karne zilizopita. Na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Haadhibu wala  Haangamizi watu isipokuwa baada ya kuwatumia Rusuli wake kuwabashiria na kuwaonya ili kuwasimamishia hoja.  

 

6-Imebainishwa kwamba maisha mazuri ya Aakhirah ni kwa matakwa Yake Allaah (سبحانه وتعالى), kukiambatana na matendo ya mja akiwa na imaan.

 

7-Kuna Makatazo na Maamrisho Ya Allaah (سبحانه وتعالى) ambayo yameanzia Aayah ya (22) hadi ya (39) yakiwemo: (i) Tahadharisho la kutokumshirikisha Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) (ii) Amri ya kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee (iii) Kuwafanyia wema wazazi wawili na kutokuwaudhi hata kwa neno la uff! Kuwanyenyekea, kuwahurumia na kuwaombea duaa. (iv) Kuwapa jamaa wa karibu haki zao na masaakini (v) Kutokufanya ubadhirifu na tahadharisho la shaytwaan anayepelekea ubadhirifu (vi) Kuwatamkia maneno mazuri jamaa wa karibu wanapoomba rizki (vii) Kutokufanya ubakhili na kutokutumia mali kwa israfu (viii) Kutokuwaua watoto kwa kukhofia ufuqara (ix) Kutokukaribia machafu ya zinaa (x) Kutokuua nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha (kuiua) isipokuwa kwa haki ya kisharia (xi) Kutokukaribia kula mali ya yatima (xii) Kutimiza ahadi (xiii) Kutimiza kipimo kamilifu kinapopimwa mizanini (xiv) Kutokufuata (au kusema) asiyekuwa nayo mtu kwayo ilimu (xv) Kutokutembea katika ardhi kwa majivuno (xvi) Akamalizia Allaah (سبحانه وتعالى) kwa tahadharisho la kutokumshirikisha Yeye (سبحانه وتعالى).     

 

8-Kuna Radd kuwapinga wanaomzulia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa Ana wana wa kike.

 

9-Imetajwa kuwa kila kilichopo mbinguni na ardhini kinamsabihi na Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى).

 

10-Imetajwa sehemu ya kauli za washirikina kutokuamini kwao kufufuliwa.

 

11-Waumini wameamrishwa watamke maneno mazuri na wajitahadharishe na shaytwaan.

 

12-Imetajwa kisa cha kuumbwa Aadam na kumkirimu kwa kuamrisha Malaika wamsujudie, na msimamo wa Ibliys juu ya hilo.

 

13-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemthibitisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na Kumuamrisha kudumisha Swalaah za usiku na mchana na kusoma Qur-aan.

 

14-Imebainishwa kuwa Qur-aan ni shifaa na rehma kwa Waumini.

 

15-Imeelezewa madai ya washirikina kumtaka Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alete mambo ya ajabu yasiyokuwa ya kibinaadam; rejea Aayah (90-95).

 

16-Imetajwa kuhusu miujiza na ishara tisa alizopewa Nabiy Muwsaa (عليه السلام) kwa Firawni.

 

17-Imebainishwa kuwa Qur-aan imeteremshwa kidogo kidogo kwa hikma yake ya kuwasomea watu kwa kituo.

 

18-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitisha Majina ya Allaah, kwamba yote ni Mazuri kwani madai ya washirikina walikuwa wakipinga sifa ya Ar-Rahmaan. Basi kwa Jina lolote lile atakavoombwa duaa ikiwa ni “Yaa Allaah” au “Yaa Rahmaan” basi yote ni sahihi.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Miongoni mwa Suwrah alizokuwa akizisoma Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kabla ya kulala ni Suwrah Al-Israa:

 

 عن عائشة رضي الله عنها قالت: كانَ النَّبيُّ صلَّى اللَّهُ عليهِ وسلَّمَ لا ينامُ علَى فِراشِه حتَّى يقرأ بَني إسرائيلَ ، والزُّمَرِ

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa halali kitandani mwake ila akisoma kwanza (Suwrah) Bani Israaiyl na Az-Zumar. [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (2920), Swahiyh Al-Jaami’ (4874)]

 

Faida:

 

1-Suwrah imeitwa Al-Israa kutokana na tukio adhimu la safari ya Al-Israa Wal-Mi’raaj ambayo ilikuwa ni safari ya baadhi ya nyakati za usiku mmoja (Al-Israa) kuanzia Masjid-Al-Haraam Makkah hadi Masjid Al-Aqswaa (Mji wa Quds Jerusalem), kisha kupanda (Mi’raaj) kufika mbingu ya saba, (na kurudi usiku huo huo Makkah). Imetajwa mwanzo wa Suwrah, rejea Aayah namba (1) kwenye maelezo bayana.

 

2-Suwrah Al-Israa ni miongoni mwa Suwrah zilizotangulia kuteremshwa, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akazitaja kuwa ni pato lake la mwanzo:

 

حَدَّثَنَا آدَمُ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، قَالَ سَمِعْتُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ يَزِيدَ، سَمِعْتُ ابْنَ مَسْعُودٍ، يَقُولُ فِي بَنِي إِسْرَائِيلَ وَالْكَهْفِ وَمَرْيَمَ وَطَهَ وَالأَنْبِيَاءِ إِنَّهُنَّ مِنَ الْعِتَاقِ الأُوَلِ وَهُنَّ مِنْ تِلاَدِي‏.‏

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Yaziyd (رضي الله عنه): Nimemsikia  ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه) akisema: Suwrah Bani Israaiyl, Al-Kahf, Maryam, Twaahaa na Al-Anbiyaa ndio miongoni mwa pato langu la kwanza na mali yangu kongwe, na (hakika ni) ndio mali yangu kongwe.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

 

Share