019-Maryam: Utangulizi Wa Suwrah

 

019-Maryam: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 98

 

Jina La Suwrah: Maryam

 

Suwrah imeitwa Maryam, na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa katika nukta (3) ya Fadhila. Na imeitwa Maryam kutokana na kisa chake Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) kuanzia Aayah namba (16).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubatilisha ‘Aqiydah (itikadi) ya washirikina na Manaswara ya kumnasibishia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa na mtoto, na kubainisha ukunjufu (ukubwa) wa Rehma za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha Miujiza Ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uwezo Wake Mkubwa wa kuumba bila ya kuweko sababu.

 

3-Radd kwa Mayahudi waliomsingizia machafu Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام)

 

4-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah kwamba Anayestahiki kuabudiwa ni Allaah (سبحانه وتعالى). Na haramisho la kumshirikisha Allaah, na kwamba hilo ni chukizo kubwa hata kwa vitu Alivyoviumba Allaah mbinguni na ardhini. 

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha kimetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Zakariyyaa (عليه السلام) na kujaaliwa kwake kumzaa Nabiy Yahyaa (عليه السّلام)  juu ya kuwa alifikia uzee wa kuvuka mipaka pamoja na mkewe kuwa tasa.

 

2-Imetajwa kuzaliwa kwa Nabiy Yahyaa (عليه السّلام) na sifa zake.

 

3-Imetajwa kisa cha Maryam na muujiza wa kuzaliwa kwa Nabiy ‘Iysaa (عليهما السلام).

 

4-Imetaja sehemu fulani ya kisa cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) alivyojadiliana na baba yake aliyekuwa ni kafiri.

 

5-Wametajwa baadhi ya Manabii na ishara kuwa walikuwa wengi akiwemo: Is-haaq, Ya’quwb, Muwsaa, Haaruwn, Ismaa’iyl, Idriys, Nuwh, Aadam (عليهم السَّلام).

 

6-Suwrah imedhihirisha aina tatu za Tawhiyd; Rejea Aayah (65) kwa maelezo bayana.

 

7-Imetaja kuhusu moto ambao kila mtu lazima aupitie.

 

8-Suwrah imebainisha malipo ya wamchao Allaah, na adhabu za makafiri, na kufungua mlango wa tawbah kwa wanaomuasi.

 

9-Imetaja baadhi ya shubha za washirikina dhidi ya Qur-aan, na kufufuliwa, pamoja na kuziraddi.

 

10-Imebainisha baadhi ya mambo yatakayotokea Siku ya Qiyaamah.

 

11-Imebainisha jinsi gani mbingu zinavokaribia kupasuka, na ardhi kuraruka, na milima kuporomoka na kubomoka kwa kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa Ana mwana!

 

12-Suwrah imekhitimishwa kwa kile kilichoanzwa nacho ambacho ni kubainisha mapenzi ya Allaah na Ikraam Yake kwa vipenzi Vyake, na kubainisha hikma ya kuteremshwa Qur-aan.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Ni Suwrah pekee iliyoitwa kwa jina la mwanamke naye ni Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام). Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amemtakasa na kumsifia. Rejea Suwrah Aal-‘Imraan (3:42-43).

 

2-Na pia katika Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesifika kuwa ni katika wanawake bora kabisa:

 

عَنْ أَنَسٍ، رضى الله عنه أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ حَسْبُكَ مِنْ نِسَاءِ الْعَالَمِينَ مَرْيَمُ ابْنَةُ عِمْرَانَ وَخَدِيجَةُ بِنْتُ خُوَيْلِدٍ وَفَاطِمَةُ بِنْتُ مُحَمَّدٍ وَآسِيَةُ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ صَحِيحٌ ‏.‏

 

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wanakutosheleza katika wanawake wa ulimwengu: Maryam bint ‘Imraan, Khadiyjah bint Khuwaylid Faatwimah bint Muhammad na Aasiyah mke wa Firawni.” [At-Tirmidhiy na amesema: Hii ni Hadiyth Swahiyh na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy Uk au namba (3878)]

 

Na pia:

 

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: كَمَلَ مِنَ الرِّجَالِ كَثِيرٌ، وَلَمْ يَكْمُلْ مِنَ النِّسَاءِ إِلاَّ مَرْيَمُ بِنْتُ عِمْرَانَ، وَآسِيَةُ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ، وَفَضْلُ عَائِشَةَ عَلَى النِّسَاءِ كَفَضْلِ الثَّرِيدِ عَلَى سَائِرِ الطَّعَامِ  

Amesimulia Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wanaume wengi wamefikia daraja ya ukamilifu lakini hakuna mwanamke aliyefikia daraja hiyo isipokuwa Aasiyah mke wa Firawni, na Maryam bint 'Imraan. Na ubora wa 'Aaishah (رضي الله عنها) kwa wanawake wengine ni kama mfano wa ubora wa thariyd kwa vyakula vingine.” [Al-Bukhaariy na wengineo]

 

3-Suwrah Maryam ni miongoni mwa Suwrah zilizotangulia kuteremshwa, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akazitaja kuwa ni pato lake la mwanzo:

 

حَدَّثَنَا آدَمُ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، قَالَ سَمِعْتُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ يَزِيدَ، سَمِعْتُ ابْنَ مَسْعُودٍ، يَقُولُ فِي بَنِي إِسْرَائِيلَ وَالْكَهْفِ وَمَرْيَمَ وَطَهَ وَالأَنْبِيَاءِ إِنَّهُنَّ مِنَ الْعِتَاقِ الأُوَلِ وَهُنَّ مِنْ تِلاَدِي‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Yaziyd (رضي الله عنه): Nimemsikia  ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه) akisema: Suwrah Bani Israaiyl, Al-Kahf, Maryam, Twaahaa na Al-Anbiyaa ndio miongoni mwa pato langu la kwanza na mali yangu kongwe, na (hakika ni) ndio mali yangu kongwe.” [Al-Bukhaariy]

 

Share