025-Al-Furqaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

025-Al-Furqaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 77

 

Jina La Suwrah: Al-Furqaan

 

Suwrah imeitwa Al-Furqaan (Pambanuo), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Faida. Na pia kutajwa neno hilo la Al-Furqaan katika Aayah namba (1). Rejea Tanbihi yake yenye ufafanuzi wa maana ya Al-Furqaan.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Ushindi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na Qur-an, na kuondosha shubha za washirikina. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kupambanua baina ya haqq (haki) na baatwil na mwongozo wa kufuata haqq na kwamba mwenye kufuata atapata mafanikio ya duniani na neema za Jannah huko Aakhirah. Na maonyo ya adhabu ya moto wa Jahannam kwa wanaofuata baatwil.  

 

3-Kuinua hadhi ya Quraan na kuthibitisha kuwa inatoka kwa Allaah (عزّ وجلّ), na kwamba imeteremshwa kwa ajili ya walimwengu wote. Na kuthibitisha Taadhima ya Aliyeiteremsha na kubainisha dalili za ukweli wake.   

 

4-Kuthibitisha moyo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumliwaza.

 

5-Kujulisha sifa za waja wa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kumtukuza Allaah (تبارك وتعالى) na kumuelezea kwa Sifa zinazodalilisha Tawhiyd Yake ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji, Umiliki, Uendeshaji na kadhaalika) na Al-Uluwhiyyah (ibaada) kwamba Yeye Ndiye Mwabudiwa wa haki. 

 

2-Suwrah imetaja simulizi za baadhi ya maneno ya washirikina, na shubha zao za kumpachika sifa ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na Qur-aan. 

 

3-Imelinganisha kati ya mafikio mabaya ya washirikinana mafikio mazuri ya Waumini Siku ya Qiyaamah.

 

4-Imetaja sehemu ya visa vya baadhi ya Manabii pamoja na kaumu zao.

 

5-Imetaja baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah.

 

6-Suwrah imetaja kumliwaza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya yale aliyoudhiwa na kudhikishwa kutoka kwa washirikina.

 

7-Imeelezea juu ya baadhi ya Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) na Uwezo Wake katika kuendesha ulimwengu.

 

8-Imewaradd washirikina wasioamini Jina la Ar-Rahmaan.

 

9-Suwrah ikamalizia kwa kuelezea sifa za ‘Ibaadur-Rahmaan (Waja wa Mwingi wa Rehma); ibaada zao na wanayojiepusha nayo, na duaa zao, na ikataja mwishowe umuhimu wa kuomba duaa.

 

Faida:

 

حَدَّثَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ يُوسُفَ، أَخْبَرَنَا مَالِكٌ، عَنِ ابْنِ شِهَابٍ، عَنْ عُرْوَةَ بْنِ الزُّبَيْرِ، عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ عَبْدٍ الْقَارِيِّ، أَنَّهُ قَالَ سَمِعْتُ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ ـ رضى الله عنه ـ يَقُولُ سَمِعْتُ هِشَامَ بْنَ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ، يَقْرَأُ سُورَةَ الْفُرْقَانِ عَلَى غَيْرِ مَا أَقْرَؤُهَا، وَكَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَقْرَأَنِيهَا، وَكِدْتُ أَنْ أَعْجَلَ عَلَيْهِ، ثُمَّ أَمْهَلْتُهُ حَتَّى انْصَرَفَ، ثُمَّ لَبَّبْتُهُ بِرِدَائِهِ فَجِئْتُ بِهِ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقُلْتُ إِنِّي سَمِعْتُ هَذَا يَقْرَأُ عَلَى غَيْرِ مَا أَقْرَأْتَنِيهَا، فَقَالَ لِي ‏"‏ أَرْسِلْهُ ‏"‏‏.‏ ثُمَّ قَالَ لَهُ ‏"‏ اقْرَأْ ‏"‏‏.‏ فَقَرَأَ‏.‏ قَالَ ‏"‏ هَكَذَا أُنْزِلَتْ ‏"‏‏.‏ ثُمَّ قَالَ لِي ‏"‏ اقْرَأْ ‏"‏‏.‏ فَقَرَأْتُ فَقَالَ ‏"‏ هَكَذَا أُنْزِلَتْ‏.‏ إِنَّ الْقُرْآنَ أُنْزِلَ عَلَى سَبْعَةِ أَحْرُفٍ فَاقْرَءُوا مِنْهُ مَا تَيَسَّرَ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia ‘Umar Bin Al-Khatwaab (رضي الله عنه): “Nilimsikia Hishaam ibn Hakiym akisoma Suwratul-Furqaan tofuati na vile ninavyoisoma na alivyonifundisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Nilikaribia kugombana naye juu ya hilo, lakini nikamvumilia mpaka akamaliza kisha nikamfunga nguo yake shingoni na kumvuta mpaka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikasema: “Nimesikia huyu mtu akisoma (Suwratul-Furqaan) kinyume na ulivyonifundisha.” Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Mwachie!” Akamwambia (Hishaam): “Soma.  Akasoma. Akasema: “Hivi ndivyo ilivyoteremshwa.” Kisha akaniambia mimi: “Soma.” Nikasoma. Akasema: “Hivi ndivyo ilivyoteremshwa. Hakika Qur-aan imeteremshwa kwa Herufi saba, hivyo someni iliyokuwa sahali kwenu.” [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

 

Share