028-Al-Qaswasw: Utangulizi Wa Suwrah

 

028-Al-Qaswasw: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 88

 

Jina La Suwrah: Al-Qaswasw

 

Suwrah imeitwa Al-Qaswasw (Visa), na inayodalilisha ni kutajwa neno hili katika Aayah namba (25).  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Desturi ya Allaah katika kuwamakinisha Waumini wanyonge, nakuwaangamiza waovu wenye kiburi.  [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) katika kuwaangamiza madhalimu na wadanganyifu, hata kama watazitegemea nguvu zote za ardhini.

 

3-Kuwapa thabati Waumini na kuwapa bishara ya kwamba mwisho mwema ni wa kwao.

 

4-Kunyenyekea kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kujisalimisha kwa kila jambo.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha ikathibitishwa kwamba Qur-aan ni Kitabu kinachobainisha wazi.

 

2-Imetaja uovu na ufisadi wa Firawni, na Ahadi ya  Allaah (سبحانه وتعالى) ya kuwaangamiza wanaofanya ufisadi.

 

3-Suwrah imetaja kisa cha kuzaliwa Nabiy Muwsaa (عليه السلام), Ulinzi wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwake pindi alipotiwa sandukuni akatupwa katika mto wa Nile akafika kupelekwa kwenye qasri la Firawni na mkewe akampenda na kumtaka kumlea. Pia jinsi Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyopanga kwa hikma Akajaalia Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) kurudishwa kwa mama yake ili amnyonyeshe.

 

4-Imetajwa matukio ya wakazi wa Misri na Bani Israaiyl. Na kuhama kwa Nabiy Muwsaa (عليه السّلام)  kutoka Misri kuelekea Madyan. Kisha kisa chake cha kuwasaidia wanawake wawili kunywesha mifugo yao, kumfikia mja mwema na kumhadithia Al-Qaswasw (Visa), na kuoa binti mmoja wa mja mwema huyo, kuwa ni malipo ya kufanya kazi kwake.

 

5-Imetaja Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) alipofika katika sehemu iliyobarikiwa akaongea na Allaah (سبحانه وتعالى) na akaamrishwa kwenda kwa Firawni kumlingania.

 

6-Imetajwa kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa yaliyomsibu kutoka kwa watu wake. Na ikabainisha kwamba hii Qur-aan inatoka kwa Allaah, na kwamba Rasuli kamwe hana uwezo wa kumhidi amtakae, na kwamba uongofu unatoka kwa Allaah.

 

7-Imetaja kisa cha Qaaruwn na uovu wake kwa watu wa Nabiy Muwsaa  (عليه السلام), na kudanganyika kwake na mali zake, na ikataja adhabu yake ya kudidimizwa ardhini kuwa ndio mwisho wa uovu na kiburi.

 

8-Suwrah imekhitimishwa kwa kuamrishwa kufanya ibaada kwa ikhlaasw, na kukataza ushirikina.

 

 

 

 

Share