042-Ash-Shuwraa: Utangulizi Wa Suwrah

 

042-Ash-Shuwraa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 53

 

Jina La Suwrah: Ash-Shuwraa

 

Suwrah imeitwa Ash-Shuwraa (Ushauri), na inayodalilisha ni kutajwa neno hilo katika Aayah namba (38).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha ukamilifu wa Sharia za Allaah, na uwajibu wa kuzifuata, na kutahadharisha juu ya kuzikhalifu. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutambulishwa kwamba, tofauti katika Sharia za Allaah hazionyeshi tofauti katika chanzo chake.

 

3-Kubainishwa Rehma ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Maghfirah na Msamaha Wake kwa kupokea tawbah za Waja Wake na kuwapa bishara Waumini juu ya malipo yanayowangoja katika maisha ya Aakhirah.

 

4-Dalili za kubainisha Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake wa kuumba mbingu na ardhi na Rehma na Neema Zake, na kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki kuabudiwa.

 

5-Kuhimiza maadili mazuri, ikiwa ni pamoja na uvumilivu na kusameheana

 

6-Kuthibitisha kuwa Qur-aan ni Wahy kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kuja kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa kwamba Qur-aan imetoka kwa Allaah, na kwamba Alimpa Wahy Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kama Alivyowapa Wahy Rusuli wengineo, na kwamba kila kilicho mbinguni na ardhini ni Milki ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

2-Imebainishwa U’adhwama (Utukufu) wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba mpaka mbingu na ardhi zinakaribia kupasuka, na kwamba Malaika wanamsabbih Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba wanaombea maghfirah Waumini walioko ardhini, na kwamba Allaah ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

3-Imethibitishwa kwamba Wahy wa Qur-aan Ameuteremsha Allaah kwa lugha ya Kiarabu, ili awaonye watu wa Ummul-Quraa [Rejea Suwrah Al-An’aam (6:92)] kuhusu Siku ya Mkusanyiko; Siku ya Qiyaamah, na kwamba huko kutakuwa na makundi mawili; moja litakuwa Jannah na jengine motoni.

 

4-Imetajwa kuwapinga washirikina na kuonyesha baadhi ya dalili za kubatilisha ushirikina wao.

 

5-Imetajwa amri ya kurudi katika Kitabu cha Allaah itakapotokea mizozo na kutofautiana.

 

6-Imethibitishwa kuwa Rusuli wote (عليهم السّلام) walitumwa na Risala (Ujumbe) mmoja tu, na kwamba tofauti zinazojitokeza kwa watu ni kutokana na uovu na kufuata matamanio tu.

 

7-Imetajwa kukaribia Qiyaamah, na msimamo wa Waumini na makafiri juu ya hilo, na kubainisha mafikio ya kila mmoja siku ya Qiyaamah.

 

8-Radd kwa washirikina waliomzushia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  kwamba amemtungia Allaah uongo. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akawapinga hilo!

 

9-Zimetajwa Aayaat (Ishara, Dalili) mbalimbali za kudhihirisha Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake.

 

10-Zimetajwa sifa kadhaa za Waumini na mojawapo ni kwamba jambo lao ni kushauriana na ndio jina la Suwrah hii tukufu.

 

11-Imetolewa mwongozo wa kuamiliana na dhulma, ima kulipiza au kusamehe na kusamehe ni katika mambo ya kuazimiwa.

 

12-Imebainishwa aina za kuteremshwa Wahy kwa Risuli Wake (عليهم السّلام).

 

13-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa jinsi Allaah Alivyomneemesha Rasuli Wake  (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kumpa Wahy wa Qur-aan ambayo ni Nuru Anayomwongoza Kwayo  Allaah Amtakaye, na kwamba mambo yote yanaishia kwa Allaah.

 

 

 

Share