039-Az-Zumar: Utangulizi Wa Suwrah

 

039-Az-Zumar: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 75

 

Jina La Suwrah: Az-Zumar

 

Suwrah imeitwa Az-Zumar (Makundi), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila za Suwrah. na kutajwa katika Aayah namba (71-72).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Daawah ya Tawhiyd na ikhlaasw, na kuacha shirki. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Muabudiwa Pekee, na Mweza wa Kuumba, Kuhuisha na Kufufua.

 

3-Kuwasimimishia hoja washirikina na kubatilisha shirki zao na malipo yao motoni.

 

4-Tofauti ya taathira ya Qur-aan kwa Waumini na makafiri, na kuelezea sababu za hidaaya na taqwa, imaan na uthabiti katika haki,

 

5-Kudhihirisha Uwezo wa Allaah mbinguni na ardhini na kujulisha baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah na hali za Waumini na makafiri.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuitukuza Qur-aan na kuthibitisha kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyeiteremsha kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).  

 

2-Waja wanaamrishwa kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) kwa ikhlaas na kubainisha shubha za wale wanaoabudu asiyekuwa Allaah kwa kisingizio kuwa waabudiwa wao wanawakuribisha tu kwa Allaah.

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Anajitakasa na usingiziaji wa makafiri kuwa Kajichukulia mwana!

 

4-Imetajwa baadhi ya dalili za Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola) ya uumbaji wa mbingu na ardhi, kugeuza usiku na mchana, na kutiisha jua na mwezi kwenda mpaka muda maalumu, na uumbaji wa mwanaadam katika tumbo la uzazi.

 

5-Imetajwa hali za makafiri na hali za Waumini, na kubainisha mwisho wa wenye kuvuta subira.

 

6-Imetajwa baadhi ya maelekezo kwa Waumini na kubainisha mwisho wao, na maonyo ya adhabu kwa asiyemwabudu Allaah.

 

7-Imetajwa onyo kwa wenye nyoyo zinazo susuwaa kwa sababu ya kutajwa Allaah. Na kisha ikatajwa namna ya uteremshaji wa Qur-aan, na jinsi inavyowaathiri Waumini ngozini na nyoyoni mwao. Na kwamba Qur-aan hiyo Adhimu ambayo ni ya lugha ya Kiarabu, haina kombo.

 

8-Allaah (سبحانه وتعالى) Anapiga mfano wa mtu (kafiri, mshirikina) aliye chini ya washirika wagombanao, na mtu mwengine (Muumini) aliye pweke na bwana mmoja tu, (anamwabudu Allaah Pekee) kwamba hawalingani sawa. 

 

9-Imebainishwa dhalimu anayekadhibisha haqq (ukweli) ulipomjia na adhabu zake, na Muumini aliyekubali na akapokea haqq, na jazaa zao.

 

10-Imethitibishwa kuwa washirikina waliamini Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji, Ufalme, Uendeshaji ulimwengu, Kuruzuku na kadhaalika), lakini hawakumpwekesha Allaah katika Tawhiyd ya Al-Uluwhiyyah (ibaada).

 

11-Imetajwa hali ya mwanaadam anapolala kuwa anafishwa usingizini, kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anazuia roho za Aliowaqadaria kufa, na Anarudisha roho za Aliowaqadaria kuendelea kuishi mpaka muda wao maalumu. Na kwamba hili ni zingatio kwa watu ili waweze kutafakari kwamba usingizi ni kama mauti madogo.  

 

12-Imetajwa kuwa madhalimu watatamani kufidia mali zote walizonazo ili waepukane na Adhabu za Allaah za Siku ya Qiyaamah.

 

13-Imetajwa hali ya kafiri anapoguswa na dhara, na hali yake anapoondoshewa dhara, kuwa hana shukurani.

 

14-Imethibitishwa kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anaghufuria madhambi yote pindi mtu akirudia kutubia Kwake kabla ya kufikia sakaraatul-mawt.  

 

15-Imetajwa majuto ya nafsi ya mtu muovu pindi inapotolewa roho, au pindi inapomfikia adhabu. Na hatakuwa na hoja kwani zilimfikia Aayaat (Ishara na Dalili) za waziwazi lakini alizikadhibisha na kuzikufuru, basi makazi yake ni Jahannam. Ama Waumini, Allaah (سبحانه وتعالى) Atawaokoa na watakuwa hawana khofu wala huzuni.

 

16-Imetajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah pindi litakapopulizwa baragumu na vitisho vyake. Na jinsi ardhi itakavong’ara kwa Nuru ya Allaah (سبحانه وتعالى), na kutakuweko mkusanyiko wa viumbe wote, na watahukumiwa kwa haki.

 

17-Imebainishwa hali ya waovu watakavyoingizwa makundi makundi katika moto wa Jahannam kudumu humo, na kulaumiwa kwa kuwakanusha Rusuli wa Allaah (سبحانه وتعالى) walipowajia duniani kuwalingania. Kisha ikafuatilia kutaja hali za Waumini watakapoingizwa katika Jannah makundi makundi kubashiriwa kheri zake; raha na neema za Jannah. Na kwa hayo, Wanamhimidi Rabb wao Aliyewatimizia Ahadi Yake.

 

18-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa Malaika watakaozunguka ‘Arsh ya Allaah (سبحانه وتعالى) huku Wakimsabbih na Kumhimidi Allaah Rabb wa walimwengu.

 

Fadhila Za Suwrah Az-Zumar:

 

Miongoni mwa Suwrah alizokuwa akizisoma Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kabla ya kulala ni Suwrah Az-Zumar:

 

 عن عائشة رضي الله عنها قالت: كانَ النَّبيُّ صلَّى اللَّهُ عليهِ وسلَّمَ لا ينامُ علَى فِراشِه حتَّى يقرأ بَني إسرائيلَ ، والزُّمَرِ

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa halali kitandani mwake ila akisoma kwanza (Suwrah) Bani Israaiyl na Az-Zumar. [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (2920), Swahiyh Al-Jaami’ (4874)]

 

 

 

Share