050-Qaaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

050-Qaaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 45

 

Jina La Suwrah: Qaaf

 

Suwrah imeitwa Qaaf, na inayodalilisha ni kutajwa katika katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila, katika Aayah namba (1).   

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Mawaidha ya nyoyo juu ya kifo na ufufuo. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwakumbusha watu Utukufu wa Qur-aan.

 

3-Kuelezea misingi ya imaan ambayo makafiri waliikanusha nayo ni kufufuliwa Siku ya Qiyaamah, kukusanywa, kuhesabiwa matendo. Na pia msingi wa Risala (Ujumbe) na Rusuli wa Allaah.

 

4-Wasifu Waumini Siku ya Qiyaamah na jinsi Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyowaandalia malipo mema.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imeitukuza na kuisifu Qur-aan kwa sifa ya Al-Majiyd.

 

2-Imetaja madai ya washirikina na kupinga kwao Unabii pamoja na kufufuliwa, na radd juu ya hayo.

 

3-Imehimizwa kutazama uumbwaji wa mbingu na vilivyomo ndani yake, na uumbwaji wa ardhi na vilivyopo juu yake, na kuota mimea na mazao,  na kuteremshwa maji mbinguni yenye baraka yanayohuisha ardhi baada ya kufa kwake, na hii ni dalili ya wazi ya kuhuishwa baada ya mauti.

 

4-Imetajwa kukadhibisha kwa (i) Kaumu ya Nabiy Nuwh (عليه السّلام) (ii) Watu wa Ar-Rass (kisima) (iii) Kaumu ya Thamuwd wa Nabiy Swaalih (عليه السّلام) (iv) Kaumu ya ‘Aad watu wa Nabiy Huwd (عليه السّلام) (v) Watu wa Nabiy Luutw (عليه السّلام) (vi) Watu wa Al-Aykah (kichakani) wa Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام) (vii) Kaumu ya Tubba’ (mfalme wa Yemen) basi tishio Alilowaahidi Allaah kwa ukafiri wao, likathibiti. 

 

5-Imekumbushwa kuwa Allaah ni Mjuzi wa yanayowazwa katika nafsi, na kwamba kuna Malaika wa kuliani na kushotoni wanaoandika kila jambo hata kauli iwe ndogo vipi inaandikwa katika kitabu kinachorekodi matendo.    

 

6–Imetajwa sakaraatul-mawt na Malaika watakaosukuma watu katika ardhi ya mkusanyiko na wengineo watakaoshuhudia matendo Qiyaamah. Kisha kila kafiri, mshirikina na mvukaji mipaka ataingizwa Jahannam.  Waliopotoshwa watalaumiana na mashaytwaan waliowapotosha, na Jahannam itajazwa kwa watu na majini.

 

7-Kisha Waumini wameahidiwa kuingizwa Jannah kwa utiifu wao na kumkhofu Rabb wao kwa ghaibu. Basi watapokelewa kwa Salaam na watapata wanayoyatamani humo na watadumu milele.

 

8-Ameliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa yaliyomsibu kutoka kwa watu wake. Akaelekezwa katika yatakayomsaidia kuvuta subira; miongoni mwayo ni Kumsabbih Allaah usiku na jioni  na kila baada ya Swalaah.

     

9-Imeelezwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah kama kupulizwa baragumu na watu watoke makaburini mwao, wafike katika mkusanyiko.

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuamrishwa akumbushe kwa Qur-aan mwenye kukhofu maonyo ya Allaah na Adhabu Zake.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Suwrah Qaaf inapendekezwa kuisoma katika minbari, Swalaah ya Ijumaa.

 

عَنْ أُمِّ هِشَامٍ بِنْتِ حَارِثَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ:  مَا أَخَذْتُ: "ق وَالْقُرْآنِ اَلْمَجِيدِ", إِلَّا عَنْ لِسَانِ رَسُولِ اَللَّهِ ‏- صلى الله عليه وسلم ‏-يَقْرَؤُهَا كُلَّ جُمُعَةٍ عَلَى اَلْمِنْبَرِ إِذَا خَطَبَ اَلنَّاسَ   رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Amesimulia Ummu Hishaam Bint wa Haarithah (رضي الله عنها): Sikuichukua

ق ۚ وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ﴿١﴾

“Qaaf. Naapa kwa Qur-aan Al-Majiyd”

 

Isipokua kutoka kwenye ulimi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiisoma kila Siku ya Ijumaa juu ya mimbari pindi anapo wakhutubia watu. [Muslim]

 

2-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiisoma Suwrah Qaaf katika Swalaah za ‘Iyd:

 

عَنْ أَبِي وَاقِدٍ اللَّيْثِيِّ قَالَ: { كَانَ اَلنَّبِيُّ ‏- صلى الله عليه وسلم ‏-يَقْرَأُ فِي اَلْأَضْحَى وَالْفِطْرِ بِـ (ق)‏, وَ (اقْتَرَبَتْ)‏.   أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ  

Amesimulia Waaqid Al-Laythiyy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alikuwa akisoma katika (‘Iyd) Alfitwri na Al-Adhwhaa ق (Suwrah 50) na اقْتَرَبَتْ  (Suwrah 54). [Muslim]

 

3-Suwrah ya Qaaf ndio ya kwanza katika Suwrah za Mufasw-swal (yaani zinazokithiri kutenganishwa kwa BismiLLaah kutokana na ufupi wake) kwa kauli iliyotiwa nguvu na ‘Ulamaa.

 

 

Share