066-At-Tahriym: Utangulizi Wa Suwrah

 

066-At-Tahriym: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 12

 

Jina La Suwrah: At-Tahriym

 

Suwrah imeitwa At-Tahriym (Haramisho), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kulingania juu ya kusimamisha na kuheshimu mipaka ya Allaah ndani ya majumba (yetu), kwa kutanguliza kumridhisha Allaah Pekee. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha mafundisho na miongozo inayofungamana na familia.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kumwongoza Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) aache kujiharamishia yale ambayo Allaah Amemhalalishia, kwa kuwa alipendelea kuwaridhia wake zake.

 

2-Imeelezea sehemu ya yaliyotokea kati ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na wake zake wawili. Mmoja wao aliitoa siri ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akampasha mwenzake.  Allaah (سبحانه وتعالى) Akamfichulia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) maongezi hayo ya siri. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaonya wake hao wawili wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), kuwa pindi watakaposaidiana katika kufanya yanayomuudhi Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), basi Allaah Anamtosheleza kumhifadhi, pamoja na Jibriyl na Waumini wengineo. Kisha wakanasihiwa watubie kwa kosa lao hilo la kibinaadam, na kuwatishia kwamba wasipofanya hivyo, basi Allaah Atambadilishia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), wake waliobora wenye sifa nzuri kadhaa.  

 

3-Waumini wameamrishwa wajikinge na moto pamoja na ahli zao, na wamekumbushwa moto wa Jahannam, na walinzi wake ambao ni Malaika wakali na washupavu wasiokwenda kinyume na Amri za Allaah.

 

4-Waumini wameamrishwa kutubia tawbah ya nasuha (ya kweli) na kubainisha athari zake nzuri za kufutiwa madhambi na kuingizwa Jannah.

 

5-Wameamrishwa pia Waumini kuhusu Jihaad dhidi ya makafiri na wanafiki.

 

6-Suwrah imekhitimishwa kwa kupiga mifano miwili: (i) Mfano wa waliokufuru ambao wamefananishwa na mke wa Nabiy Nuwh na mke wa Nabiy Luutw, ambao walikuwa chini ya hifadhi ya ndoa ya waja wawili hawa. Wake hao wawili walimkufuru Allaah (سبحانه وتعالى) na wakawafanyia khiyana Rusuli hao. Basi uhusiano wao kama wake wa Rasuli wa Allaah, haukuwafaa kitu kwa sababu ya kufru zao,  wakaingizwa motoni kuwa ni jazaa yao waliyostahiki. (ii) Mfano wa walioamini ambao wamefananishwa na (Aasiyah) mke wa Firawni, ambaye alikuwa kwenye hifadhi ya ndoa na kafiri huyo, lakini hakumtii katika kufru zake, na matokeo yake yakawa ni kuadhibiwa na mumewe Firawni. Basi pindi alipokuwa anaadhibiwa, aliomba duaa Allaah Amjengee nyumba Peponi, na Amuokoe na ukafiri wa Firawni na maasi yake, na Amuokoe na madhalimu. Wakafananishwa tena walioamini, kwa mfano wa Maryam Bint ‘Imraan ambaye ni mama yake Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام), aliyejihifadhi na akajilinda na uzinifu, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuamrisha Jibriyl (عليه السّلام) apulize kwenye mfuko wa nguo yake, na mpulizo huo ukafika katika uzao wake akabeba mimba ya ‘Iysaa (عليه السّلام). Akayaamini Maneno ya Rabb wake, akafuata Sharia Zake, na akawa miongoni mwa wenye kumtii Allaah (سبحانه وتعالى).  

 

 

 

 

Share