085-Al-Buruwj: Utangulizi Wa Suwrah

 

085-Al-Buruwj: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 22

 

Jina La Suwrah: Al-Buruwj (Buruji), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha Nguvu za Allaah (سبحانه وتعالى) Zilizozunguka kila kitu, na Nusra Yake kwa Vipenzi Vyake na Mkamato Wake wa kuwaadhibu maadui Wake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba wake kwa yale yaliyawapata kutoka kwa maadui zao, na kuwafanya Waumini wathibitike katika haqq.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia mbingu na buruji. Na kwa Siku ya Qiyaamah Aliyoahidi kuwafufua na kuwakusanya viumbe wahesabiwe. Na kwa kila mwenye kushuhudia na anayeshuhudiwa. Ikafuatia jambo linalohakikishwa kiapo kwamba, wamelaaniwa na wameangamia watu wa mahandaki waliowatesa Waumini kwa kuwaingiza katika shimo kubwa lilowashwa moto kwa kuni nyingi, huku wakiwatazama wanavyoadhibika. Na mateso hayo waliyoteswa Waumini ni kwa sababu washirikina hao wa mahandaki, waliwalazimisha warudi katika dini yao wamshirikishe Allaah, lakini Waumini walikataa kabisa kwa kuwa walithibitika katika Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى)  wakamwamini.      

 

3-Wameahidiwa wenye kuchupa mipaka ambao wanawafitini Waumini, kwamba watapata adhabu ya Jahannam.

 

4-Waumini wenye kutenda mema, wamebashiriwa kuingizwa Jannah zenye neema, na hawa ndio waliofaulu.

 

5-Imeashiriwa Adhabu kali ya Allaah (سبحانه وتعالى), na ikathibitishwa Tawhiyd Yake ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji, Uhuishaji na Ufishaji) na Sifa Zake nyenginezo Kamilifu, na Umiliki Wake wa ‘Arsh Tukufu, na Uwezo Wake wa Kufanya Atakalo, wala hakuna anayeweza kuzuia jambo Alitakalo Allaah (سبحانه وتعالى), bali Anaposema Kun! (Kuwa), basi jambo linakuwa!

 

6-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameliwazwa kwa kupigiwa mfano wa watu wa Firawni na Thamuwd, ambao waliokufuru na kukanusha Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى) kupitia Rusuli Wake ya kwamba, Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwazunguka kwa Ujuzi Wake na Uwezo Wake Kuwaadhibu na kuwaangamiza.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kuendelea kumliwaza Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kuitukuza na kuisifu Qur-aan aliyoteremshiwa, kwamba Qur-aan hii si kama wanavyodai washirikina kuwa ni mashairi na uchawi hivyo wakaikanusha, na kwamba Qur-aan hii iko katika Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa) haiwezi kubadilishwa au kupotoshwa.

 

Faida:

 

عَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةَ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يَقْرَأُ فِي الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ بِالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ وَنَحْوِهِمَا ‏.‏

Amesimulia Jaabir Bin Samrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Adhuhuri na Alasiri:

 

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ ﴿١﴾

Naapa kwa mbingu yenye buruji.” [Al-Buruwj (85)]

 

Na

وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ ﴿١﴾

“Naapa kwa mbingu na kinachogonga kinapotoka usiku.” [Atw-Twaariq (86)]

 

Na Suwrah zinazofanana kama hizo. [Hadiyth Hasan Swahiyh - At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Swahiyh Abiy Daawuwd (805)]   

 

 

Share