080-‘Abasa: Utangulizi Wa Suwrah

 

080-‘Abasa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 42

 

Jina La Suwrah:  ‘Abasa

 

Suwrah imeitwa ‘Abasa (Alikunja Kipaji) cha uso. Na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwakumbusha dalili za kufufuliwa makafiri walioghafilika na Rabb wao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Uhalisia wa da’wah ya Qur-aan na utukufu wa yule mwenye kunufaika nayo, na udhalili wa yule mwenye kuipuuza.

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kudhihirika ukunjaji uso wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumgeukia kwake Swahaba Mtukufu, Ibn Ummi Maktuwm (رضي الله عنه) aliyemwendea kutaka kujifunza kwake, lakini Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  akawa ameshughulika kumlingania Quraysh mmoja aliyekuwa tajiri, naye Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa ana himma ya kuongoza watu, akataraji ahidike tajiri huyo. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuwaidhi Rasuli Wake Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), mawaidha mazuri ya upole.

 

2-Ikabainishwa kwamba mawaidha hayo ya Allaah (سبحانه وتعالى) Alimyomuwaidhi Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), Anawakumbusha Waja Wake pia kwamba, ni mawaidha kwa mwenye kutaka kuwaidhika kwa Qur-aan. Na Anawabainishia usawa baina ya watu katika da’wah na kubalighisha ilimu kwa wenye hadhi na walio wanyonge.

 

3-Imebainishwa Utukufu wa Qur-aan iliyomo katika Sahifa zenye kutakaswa na kuadhimiwa, na zimo katika Mikono ya Malaika waandishi walio watukufu na watiifu.

   

4-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah kwa kutajwa asili ya chimbuko la mwanaadam na Neema za Allaah kwao za kuwawepesishia njia, na hifadhi na takrima zao za kuzikwa makaburini, na Kuwateremshia mvua inayokuza mimea ikatoka humo kila aina ya mazao, yawanufaishe katika uhai wao, wao pamoja na wanyawa wao.

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kukumbushwa vitisho vya Siku ya Qiyaamah, na hali za watu itakavokuwa kwamba, kila mtu atamkimbia mwenzake hata kuwakimbia wazazi wake, na wengineo wa uhusiano wa damu. Na kwamba watu watakuwa aina mbili; ambao watakaofaulu kwa kudhihirika nyuso zao kunawiri na kuwa na furaha. Na watakaokhasirika kwa kudhihirika nyuso zao kufunikwa na vumbi na kubadilika kuwa nyeusi, na hawa ndio makafiri wapotofu wavukao mipaka katika kufru na shirki zao, na matendo yao.

 

 

 

 

Share