114-An-Naas: Utangulizi Wa Suwrah

 

114-An-Naas: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.

 

Idadi Za Aayah: 6

 

Jina La Suwrah: An-Naas

 

Suwrah imeitwa An-Naas (Watu), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila na kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

Mahimizo juu ya kujilinda (kutaka hifadhi) kwa Allah kutokana na shari za Mashetani na wasiwasi wao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa amri ya kujilinda na shari, kwa Rabb wa wanaadam, Ambaye ni Mfalme wa wanaadam Mwenye Kumiliki kila kitu ulimwenguni na Mwenye Kuyaendesha mambo ya walimwengu Anavyotaka. Kunapasa kujilinda Naye  (سبحانه وتعالى)  kwa sababu, Yeye Pekee Ndiye Mweza wa kurudisha shari hizo. Na Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Ambaye hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Na pia kujilinda kutokana na shari ya shaytwaan ambae katika sifa zake, hujificha na kuchochea watu, na kutia wasiwasi katika nyoyo za wanaadam. Na kwamba yeye (shaytwaan) anaweza kuwa katika majini na anaweza kua katika watu.  

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Suwrah hii ina fadhila nyingi mno. Miongoni mwa fadhila zake ni:

 

1-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Alikuwa Anajisomea Kila Alipoumwa:

 

حَدَّثَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ يُوسُفَ، أَخْبَرَنَا مَالِكٌ، عَنِ ابْنِ شِهَابٍ، عَنْ عُرْوَةَ، عَنْ عَائِشَةَ، رضى الله عنها أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم كَانَ إِذَا اشْتَكَى يَقْرَأُ عَلَى نَفْسِهِ بِالْمُعَوِّذَاتِ وَيَنْفُثُ، فَلَمَّا اشْتَدَّ وَجَعُهُ كُنْتُ أَقْرَأُ عَلَيْهِ وَأَمْسَحُ بِيَدِهِ رَجَاءَ بَرَكَتِهَا‏.‏

Amesimulia ‘Urwah (رضي الله عنه): ‘Aaishah (رضي الله عنها) amesema: Pindi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa anaumwa, anajisomea mwenyewe Al-Mu‘awwidhaat na anapuliza katika vitanga vyake vya mikono na anajifuta kwavyo mwili wake. Ugonjwa ulipomzidi nilikuwa ninamsomea, na ninafuta kwa mkono wake nikitaraji baraka zake (mkono). [Al-Bukhaariy na Muslim]

Al-Mu‘awwidhaat  ni Al-Falaq (113) na An-Naas (114).

 

2-Ni Sunnah Kuisoma Katika Swalaah Ya Witr:

 

عَنْ عَبْدِ الْعَزِيزِ بْنِ جُرَيْجٍ، قَالَ سَأَلْنَا عَائِشَةَ بِأَىِّ شَىْءٍ كَانَ يُوتِرُ رَسُولُ اللَّهِ ـ صلى الله عليه وسلم ـ قَالَتْ كَانَ يَقْرَأُ فِي الرَّكْعَةِ الأُولَى بِـ  سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى ‏ وَفِي الثَّانِيَةِ ‏ قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُون ‏ وَفِي الثَّالِثَةِ   قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ  وَالْمُعَوِّذَتَيْنِ ‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdul-‘Aziyz Bin Jurayj (رضي الله عنه): Tulimuuliza ‘Aaishah (رضي الله عنها); Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma nini katika Swalaah ya Witr? Akasema: Alikuwa akisoma katika Rakaa ya kwanza:

 

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى

Na katika ya pili:

 

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ

 

Na katika ya tatu:

 

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ

Na Al-Mu’awwidhatayni. [Ibn Maajah, At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (463)]

 

3-Kuisoma Katika Adhkaar Za Asubuhi Na Jioni Na Adhkaar Za Kulala Kumkinga Mtu Na Kila Shari.

 

عَنْ عَائِشَةَ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ إِذَا أَوَى إِلَى فِرَاشِهِ كُلَّ لَيْلَةٍ جَمَعَ كَفَّيْهِ ثُمَّ نَفَثَ فِيهِمَا فَقَرَأَ فِيهِمَا  ‏قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‏ وَ ‏قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ  وَ ‏قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ‏ ثُمَّ يَمْسَحُ بِهِمَا مَا اسْتَطَاعَ مِنْ جَسَدِهِ يَبْدَأُ بِهِمَا عَلَى رَأْسِهِ وَوَجْهِهِ وَمَا أَقْبَلَ مِنْ جَسَدِهِ يَفْعَلُ ذَلِكَ ثَلاَثَ مَرَّاتٍ‏.‏

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها):  Pindi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoingia kitandani kila usiku, alikuwa akikusanya vitanga vyake vya mikono na kupuliza juu yake baada ya kusoma:

 

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾

na

 قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾

na

 قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾

Kisha akipangusa kwa mikono yake sehemu za mwili wake ambazo alikuwa anaweza kuzipangusa, akianza na kichwa chake, uso wake na sehemu yake ya mbele ya mwili. Alikuwa akifanya hivyo mara tatu. [Al-Bukhaariy]

 

4-Haijapata Kuteremshwa Kabla Katika Tawraat Wala Injiyl:

 

عَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ، قَالَ قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ أُنْزِلَ - أَوْ أُنْزِلَتْ - عَلَىَّ آيَاتٌ لَمْ يُرَ مِثْلُهُنَّ قَطُّ الْمُعَوِّذَتَيْنِ ‏"

Amesimulia ‘Uqbah Bin ‘Aamir (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: zimeteremshwa -au nimeteremshiwa Aayaat ambazo hazijapata kuteremshwa kabla. Nazo ni Al-Mu’awwidhatayni [Muslim] Na katika Riwaaya: Nimeteremshiwa usiku..

 

Al-Mu’awwidhatayni ni Al-Falaq (113) na An-Naas (114)

 

5-Ni Sunnah Kuisoma Kila Baada Ya Kumaliza Swalaah Za Fardhi Pamoja na Al-Ikhlaasw (112) na An-Naas (114).

 

عَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ، قَالَ أَمَرَنِي رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ أَقْرَأَ الْمُعَوِّذَاتِ دُبُرَ كُلِّ صَلاَةٍ ‏.‏

Amesimulia ‘Uqbah Bin ‘Aamir (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameniamrisha nisome Al-Mu’awwidhaat kila baada ya Swalaah. [At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Abiy Daawuwd (1523)]

 

 

 

 

 

Share