22-Malaika: Malaika Wana Uwezo Wa Kujigeuza Umbo Jingine Lisilo Lao

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

22:  Malaika Wana Uwezo Wa Kujigeuza Umbo Jingine Lisilo Lao

 

Allaah Ta’aalaa Amewapa Malaika uwezo wa kujibadilisha umbo lao la asili na kujiweka kwenye umbo jingine.   Jibriyl ‘Alayhis Salaam alipomwendea Bibi Maryam (‘Alayhas Salaam), alijimithilisha katika umbo la binadamu kama inavyoeleza Qur-aan Tukufu:

 

"فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا  •  قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا "

 

Akafanya pazia kujitenga nao, Tukampelekea Ruwh Wetu (Jibriyl عليه السلام) akajimithilisha kwake kama bin Aadam timamu  ● (Maryam) akasema:  Najikinga kwa Ar-Rahmaan usinidhuru, ukiwa ni mwenye taqwa”.  [Maryam: 17-18]

 

 

Jibriyl alikuwa katika umbo la mwanaume kamili, ndipo Maryam akaogopa asije kumdhuru na hapo akajikinga kwa Allaah Ta’aalaa.  Muislamu anapohisi hatari kutoka kwa mtu au kiumbe chochote, basi aharakie kujikinga kwa Allaah na shari yake.

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alijiwa na Malaika wakiwa katika sura ya binadamu, naye hakuwajua kama ni Malaika mpaka alipowatengea nyama na chakula akaona hawala na akaingiwa na hofu, na wao wakajitambulisha kwamba ni Malaika ambao wametumwa kwenda kutekeleza kazi maalum ya kuwaangamiza kaumu Lut waliochupa mipaka.  Allaah Anatuambia:

 

"وَلَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ ۖ فَمَا لَبِثَ أَن جَاءَ بِعِجْلٍ حَنِيذٍ فَلَمَّا رَأَىٰ أَيْدِيَهُمْ لَا تَصِلُ إِلَيْهِ نَكِرَهُمْ وَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۚ قَالُوا لَا تَخَفْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمِ لُوطٍ"

 

Na kwa yakini walimjia Ibraahiym Wajumbe Wetu kwa bishara, wakasema: Salaam! (Naye) Akasema:  Salaam.  Basi hakukawia ila alikuja na ndama aliyebanikwa Alipoona mikono yao haisogei kumla (ndama) aliwashangaa na ikamuingia khofu kutokana nao.  Wakasema:  Usiogope!  Hakika Sisi Tumetumwa kwa kaumu Luwtw”.   [Huwd: 69-70]

 

Malaika hao baada ya kuondoka kwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), walikwenda kwa Nabiy Lut (‘Alayhis Salaam) kwa umbo lile lile la kibinadamu.  Allaah Anatuambia:

 

 

"وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَصِيبٌ"

 

Na Wajumbe Wetu walipomjia Luwtw, alisononeka kwa ajili yao na akawaonea dhiki, akasema:  Hii ni siku ngumu mno”.   [Huwd: 77]

 

Mufassiruna wengi wanasema kwamba Malaika hao walipofika kwa Lut, walijiweka katika sura ya vijana wazuri ili kuwajaribu watu hao, nao kwa ujasiri wao wa kiovu wakawataka, na Allaah Akawateremshia mvua ya mawe baada ya mji wao kunyanyuliwa juu kisha ukapinduliwa.

 

Naye Jibriyl (‘Alayhis Salaam) alikuwa akimjia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sura tofauti.  Mara humjia kwa sura ya Dihyat bin Khaliyfah Al-Kalbiy, mara nyingine kwa sura ya bedui, na mara mbili katika umbile lake la asili aliloumbiwa nalo akiwa na mbawa mia sita ambapo kati ya kila mbawa mbili ni kama baina ya mashariki na magharibi.  Dihyat bin Khaliyfah Al-Kalbiy alikuwa ni miongoni mwa Maswahaba wakubwa na alikuwa na sura nzuri mno.

 

Malaika hawa walikuwa wakija kwa umbo la kibinadamu ili waweze kuonekana. Mwanadamu hana uwezo wa kumwona Malaika katika umbile lake la asili kutokana na udhaifu wake wa kuweza kukabiliana na hilo isipokuwa wale tu ambao Allaah Amewapa nguvu ya kuliweza hilo kama Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Maswahaba walibahatika kumwona Jibriyl (‘Alayhis Salaam) katika umbo la kibinadamu kama inavyoeleza Hadiyth ya ‘Umar:

 

“Wakati tukiwa tumekaa siku moja pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam), mara ghafla akatutokezea mtu aliyevaa nguo nyeupe mno, nywele zake nyeusi mno, haonekani na athari yoyote ya safari, na hakuna yeyote kati yetu anayemjua.  Akaja na kukaa mbele ya Rasuli na akaegemeza magoti yake kwenye magoti ya Rasuli, na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake, kisha akasema:  Ee Muhammad!  Nieleze kuhusu Uislamu. …………”

 

Baada ya kumuuliza Rasuli kuhusu Uislamu, iymaan, ihsaan, qiyaamah na alama zake aliondoka, na Rasuli akawajulisha Maswahaba kwamba huyo alikuwa ni Jibriyl ambaye alikuja kwa ajili ya kuwafundisha dini yao kupitia maswali aliyomuuliza yeye.

 

Kadhalika, katika kisa cha mtu aliyeua watu 99, mtu huyo alipokuwa anahama kwenda sehemu nyingine baada ya kutubia, mauti yalimjia katikati ya njia ya kati ya kule alikotoka na kule anakoelekea.    Malaika wa rahmah wakavutana na Malaika wa adhabu kuhusu nani anayestahiki kumchukua kati yao.  Hapo akawajia Malaika katika umbo la kibinadamu akawaambia:   Pimeni masafa ya kuanzia hapa alikofia baina ya kule anakoelekea na kule alikotoka.  Kama kule anakoelekea pamebakia kidogo, basi Malaika wa rahmah wamchukue.

 

 

Share