24-Malaika: Malaika Hawali, Hawanywi, Hawaoani Wala Hawazai

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

24:  Malaika Hawali, Hawanywi, Hawaoani Wala Hawazai

 

Allaah Anasema:

 

’فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ   فَقَرَّبَهُ إِلَيْهِمْ قَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ"

 

Akaondoka bila kuhisiwa kuelekea kwa ahli yake, akaleta ndama aliyenona  Akawakurubishia pale walipo, akasema:  Mbona hamli?  Akawaogopa ndani ya nafsi yake. Wakasema:  Usikhofu!  Na wakambashiria ghulamu mjuzi”.  [Adh-Dhaariyaat: 26-28]

 

Hawa ni Malaika waliokwenda kwa Nabiy Ibraahiym (‘alayhis Salaam) katika umbile la kibinadamu kama wageni wake.  Naye haraka akawatayarishia ndama aliyenona.  Alipokuwa tayari, aliwatengea na kuwakaribisha lakini hawakula, na hapo akaingiwa na hofu, lakini walijitambulisha kwamba wao ni Malaika, na Malaika hawali, wala hawanywi.  Malaika hawa walikuwa wametumwa kwenda kwa Nabiy Lut (‘Alayhis Salaam) ili kuwaangamiza kaumu yake.

 

Ibn Kathiyr amesema:  “Malaika hawana habari na chakula, hawakitamani wala hawakili”.

 

As-Safaaraaniy amesema:  “Ulamaa wahakiki wamefikia itifaki ya kwamba Malaika hawali, wala hawanywi, wala hawazaani, na wala hawana matamanio ya kimwili.  Hii ni kwa vile wao wanamsabbih Allaah usiku na mchana na wala hawachoki kama Anavyosema Allaah Ta’aalaa:

 

"يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُون"

 

“Wanamsabbih Allaah usiku na mchana na wala hawachoki”.   [Al-Anbiyaa: 24]

 

Hawasiti hata dakika moja kumsabbih Allaah.  Ikiwa hii ndiyo sifa yao, basi haiwezekani wakawa wanakula, au kunywa, au kujamii.

 

 

Share