40-Malaika: Kazi Za Malaika: (3)- Atakayepuliza Baragumu Siku Ya Qiyaamah

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

40:   Kazi Za Malaika

 

(3)- Atakayepuliza Baragumu Siku Ya Qiyaamah

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۖ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ"

 

“Na baragumu litapulizwa.  Watakufa kwa mshtuko walioko mbinguni na ardhini isipokua Amtakaye Allaah.  Kisha litapulizwa humo jengine, tahamaki hao wanasimama wakitazama”.  [Az-Zumar: 68]

 

Toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu): 

 

"ما طرَفَ صاحبُ الصورِ مُذْ وُكِّلَ بِهِ مُسْتَعِدًّا ينظُرُ نحْوَ العرشِ مخافَةَ أنْ يَؤْمَرَ قبْلَ أنْ يَرْتَدَّ إليْهِ طَرْفُهُ، كَأَنَّ عَيْنَيْهِ كَوْكَبَانِ دُرِّيَّانِ"

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  (Malaika) mwenye kulikamata baragumu hajawahi kupepesa jicho lake tokea pale alipokabidhiwa baragumu hilo, amekaa tayari wakati wote akiwa amelielekeza jicho lake upande wa ‘Arshi kwa kuhofia kupewa amri (ya kulipuliza) kabla jicho lake halijapepesa, macho yake ni kama nyota mbili zenye mwanga mkali”.  [Imekharijiwa na Abu Ash-Shaykh katika Al-‘Adhwamah (391) na Al-Haakim (8676).  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Silsilatu Al-Ahaadiythi As-Swahiyha (1078)]

 

Hali hii ilimfanya Rasuli (Swalla Acllaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukosa raha kabisa ya ladha ya maisha kutokana na kitisho cha jambo hilo hadi kuwaeleza Maswahaba wake ili nao wapate picha ya uhalisia huo.  Anasema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"كَيْفَ أَنْعَمُ وَقَدِ الْتَقَمَ صَاحِبُ الْقَرْنِ الْقَرْنَ وَحَنَى جَبْهَتَهُ وَأَصْغَى سَمْعَهُ يَنْتَظِرُ أَنْ يُؤْمَرَ أَنْ يَنْفُخَ فَيَنْفُخَ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ الْمُسْلِمُونَ: فَكَيْفَ نَقُولُ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ:‏ قُولُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ تَوَكَّلْنَا عَلَى اللَّهِ رَبِّنَا ‏"‏

 

“Vipi nitakuwa na utulivu wa maisha wakati ambapo mwenye baragumu ashalitia baragumu kinywani, ameinamisha paji lake na amelitega vizuri sikio lake akisubiri apewe amri ya kulipuliza akalipuliza?!  Maswahaba wakamuuliza:  Tuseme vipi ee Rasuli wa Allaah?  Akawaambia:  Semeni:  Allaah Anatutosha, Naye Ndiye Mtegemewa bora kabisa, Tumetawakkal kwa Allaah, Mola wetu”.  [Hadiyth Swahiyh katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3243)]

 

Hadiyth hii inatuonyesha ni namna gani Malaika huyu alivyojiandaa kusubiri amri toka kwa Allaah ya kulipuliza baragumu la kwanza kisha la pili.  Maswahaba walipoipata picha hii, wakamuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nini waseme ili Allaah Awapitishe salama na kizaazaa hicho cha siku hiyo, naye akawaambia nini cha kusema.

 

Kiufupi, jina la Malaika huyu ambaye amelishikilia baragumu halikutajwa katika Qur-aan wala Sunnah.  Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wamenukulu ‘Ijmaa ya kwamba Malaika ambaye atapuliza baragumu Siku ya Qiyaamah ni Israafiyl.

 

Hadiyth hii inatufunza yafuatayo:

 

1-  Rasuli pamoja na utukufu wake wa daraja, anaiogopa Siku hiyo ya Qiyaamah litakapopulizwa baragumu.  Hili liwe chachu kwetu kuiogopa zaidi Siku hiyo kwa kushikamana barabara na matendo mema na kujiepusha na mabaya.

 

2-  Neno: "حَسْبُنَا اللهُ ونعمَ الوَكِيْلُ" lina fadhila kubwa, nalo pia ni katika viokozi vya mfazaiko wa Qiyaamah.  Muislamu ajitahidi kulitamka nyakati zote ili aweze kusalimika na misukosuko ya dunia na kizaazaa cha kesho akhera.

 

3-  Baragumu liko pamoja na Malaika ambaye amelishikilia tayari kulipuliza akipewa amri, na kwamba Qiyaamah kipo karibu kutokana na utayari wa Malaika huyo.

 

4-  Namna ambavyo Malaika wanamwogopa Allaah Mtukufu na wanavyomtii kinyume na sisi ambao hatumpi Allaah heshima Anayostahiki.

 

5-  Nguvu kubwa aliyopewa Malaika huyo ya kuweza kupuliza baragumu hilo likavifanya viumbe vyote vya ardhini na mbinguni kufa.  Je, Huyo Aliyempa nguvu hizo, Nguvu Zake zikoje?!

 

 

Share