Shaykh Al-Albaaniy (رحمه الله): Mwanachuoni Wa Karne

 

Shaykh Al-Albaaniy - Mwanachuoni Wa Karne
Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

AL-IMAAM AL- MUHADITH SHAYKH MUHAMMAD NAASWIRUD-DIYN AL-ALBAANIY

1332H-1420H - 1914M-1999M 

  

 

JINA LAKE:   Muhammad Naaswir-ud-Diyn bin Nuuh An-Najaatiy

 

NASABA YAKE:  Al-Albaaniy (Kwa sababu asili yake ni mtu wa Albania)

 

KUN-YAH YAKE:  Abu ‘Abdir-Rahmaan (Baba ‘Abdur-Rahmaan’)

 

 

WAKE ZAKE:  Alioa wake wanne; watatu wa mwanzo walimzalia watoto, na wa nne ‘Ummu Al-Fadhwl’ hakujaaliwa kuzaa, na ndiye aliyekuwa naye hadi mwisho wa maisha yake.

 

WATOTO WAKE: Aliruzukiwa watoto 13; wakiwa 7 wa kiume na 6 wa kike. Wa kiume ni: ‘Abdur-Rahmaan, ‘Abdul-Latwiyf, ‘Abdur-Razzaaq, ‘Abdul-Muswawwir, ‘Abdul-Muhaymin, Muhammad na ‘Abdul-A’alaa. Wa kike ni: Aniysah, Aasiyah, Salaamah, Hassaanah, Sakiynah na HibatuLlaah.

 

Mwanachuoni Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn bin Nuuh An-Najaatiy Al-Albaaniy ni mmoja kati ya Maulamaa wakubwa wa Kiislam katika zama hizi. Anahesabika kuwa ni mwanachuoni wa Hadiyth maarufu kabisa katika fani ya elimu ya Jarh na Ta’adiyl. [1]

Shaykh Al-Albaaniy vilevile ni hoja katika elimu ya Mustwalahul-Hadiyth. [2] Na wanachuoni wamemsifu na kumwelezea kwamba kwa elimu yake hiyo, karejesha kumbukumbu za zama za kina Imaam Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy, Ibn Kathiyr na wengineo miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa fani hiyo.

 

Alikuwa na kumbukumbuku kali ya kuweka vitu kichwani na kuhifadhi mengi. Kumbukumbu inayotukumbusha wema waliotangulia kama kina Ibn ‘Abbaas, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliofuatia kama Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Ash-Shaafi’y, Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyah, Imaam Ibn Kathiyr, Imaam An-Nawawy na wengineo (Allaah Awarehemu wote).

 

KUZALIWA NA KUKUA KWAKE:

 

Alizaliwa mwaka 1332H – 1914M katika mji wa Ashkodera ambao kwa wakati huo ulikuwa ni mji mkuu wa Albania ulioko Ulaya Mashariki katika ukoo maskini. Baba yake aitwaye Shaykh Nuuh An-Najaatiy alihitimu katika chuo cha sheria huko Istanbul, Uturuki, na kurejea kwao akiwa ni mwanachuoni. Lakini baada ya mfalme Ahmad Zogo kutwaa madaraka ya nchi na kuendesha utawala wa nchi hiyo kikomunisti ikabidi baba yake Shaykh Al-Albaaniy ahame na kuelekea Damascus, Syria. Wakati huo Shaykh Al-Albaaniy alikuwa na umri wa miaka tisa.

 

Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy alianza masomo yake ya awali katika madrasah ya Al-Is’aaf Al-Khayriyah hapo Damascus na kuendelea hadi alipomaliza na kuwa msimamizi wa chuo hicho hadi kulipoanza mapinduzi dhidi ya Ufaransa nchini humo. Madrasah hiyo ikakumbwa na maafa ya moto yaliyosababishwa na vurugu na machafuko katika vita hivyo. Kisha baba yake aliamua kumuachisha masomo na akaanza kumsomesha mwenyewe. Alimwekea ratiba kali ya kimasomo aliyokuwa akimsomesha, nayo ni; Qur-aan, Tajwiyd, Swarf, Fiqh (ya Kihanafi, yaliyokuwa madhehebu ya baba yake aliyekuwa mwanachuoni mkubwa wa madhehebu hayo). Shaykh Al-Albaaniy alijifunza pia masomo mbalimbali ya Dini na lugha kutoka kwa wanachuoni wakubwa na Mashaykh mbalimbali waliokuwa marafiki wa baba yake kama vile Shaykh Sa’iyd Al-Burhaaniy ambaye alisoma kwake vitabu mbalimbali na masomo ya balaaghah na lugha.

 

KUJIFUNZA KWAKE ELIMU YA HADIYTH

Alitunukiwa shahada ya juu ya elimu ya Hadiyth kutoka kwa Shaykh Raaghib At-Twabbaakh, mwanachuoni mkubwa wa Halab katika wakati huo. Hapo ni wakati alipokutanishwa naye kupitia Shaykh Muhammad Al-Mubaarak ambaye alimjulisha Shaykh At-Twabbaakh kuhusu kijana huyo (Al-Albaaniy) jinsi alivyokuwa mahiri katika elimu ya Hadiyth. Na baada ya Shaykh At-Twabbaakh kumjaribu na kulithibitisha hilo mwenyewe, ndipo akamtunuku shahada (Ijaazah) hiyo. Shahada hiyo aliyopewa haikuwa moja, bali alipata vilevile kwa Wanachuoni wakubwa wa Hadiyth wengine kama Shaykh Bahjatul Baytaar (ambaye isnaad yake inafika hadi kwa Imaam Ahmad bin Hanbal). [3]

 

Aliingia kwenye fani hiyo ya Hadiyth akiwa na miaka ishirini. Aliathirika sana na tafiti mbalimbali alizokuwa akiziandika Muhammad Rashiyd Ridhwaa. Tafiti hizo za Rashiyd Ridhwaa zilikuwa katika jarida la Al-Mannaar. Anasema Imaam Al-Albaaniy: “Nilichokimulika mwanzo miongoni mwa vitabu, ni vile vitabu vya visa vya lugha ya kiarabu, kama vile; Adh-Dhwaahir, ‘Antarah, Malik Sayf na vinginevyo kama hivyo. Kisha nikazama katika vitabu vya visa vya kijasusi vilivyotarjumiwa katika lugha ya kiarabu. Na siku moja nikapita katika vibanda vya kuuza vitabu na macho yangu yakaangaza kwenye jarida moja  liitwalo Al-Mannaar na katika kupekuapekua ndani yake nikakutana na makala ya kitafiti ya Shaykh Rashiyd Ridhwaa akikielezea kitabu cha ‘Ihyaa ‘Uluum Ad-Diyn’ cha Shaykh Ghazaali, akitaja mazuri yaliyomo ndani ya kitabu hicho na kasoro zake. Na ndiyo kwa mara ya kwanza nakutana na aina kama hii ya uchambuzi wa kielimu. Nilivutika sana na uchambuzi sampuli hiyo na ukanifanya nisome toleo zima la makala hiyo. Kisha nikawa nafuatilizia maudhui za uchambuzi wa Hadiyth wa mwanachuoni Al-Haafidh Al-‘Iraaqiy alioufanya katika kuchambua Hadiyth zilizomo ndani ya kitabu hicho cha ‘Ihyaa ‘Uluum Ad-Diyn’. Sikutosheka hadi ikabidi nimuombe muuza duka aniazime jarida hilo kwa kuwa sikuwa na uwezo wa fedha wa kulinunua!

 

Hapo ndipo ilipoanza safari ndefu ya kusoma vitabu mbalimbali. Nikatolesha nakala ya maudhui hiyo iliyofanyiwa uchambuzi wa kina katika jarida hilo”

 

Shaykh Al-Albaaniy alijifunza pia kwa baba yake elimu ya kutengeneza saa hadi akawa fundi mzuri maarufu kwa kazi hiyo. Ikawa ndiyo kazi impatiayo rizki yake ya halali. Akiwa ni fundi na hapo hapo ni mtafutaji elimu. Hali hiyo ikaendelea hivyo hadi alipoamua kutenga siku mbili tu za kufanya kazi hiyo ya utengenezaji wa saa kwa ajili ya kupata rizki yake, na siku zote zilizobaki zikawa ni za kutafuta elimu. Elimu hiyo alikuwa akiichukulia katika maktaba kubwa ya mji huo wa Damascus iitwayo Adh-dhwaahiriyah ambapo alikuwa akitumia siku nzima kusoma na kutafiti. Alishughulishwa mno na kusoma hadi akawa anasahau hata kula. Kilichokuwa kinamkatisha utafiti na masomo yake ni vipindi vya Swalah tu. Mwishowe wahusika wa maktaba hiyo wakamuamini na kuamua kumpa funguo zake awe anatumia maktaba wakati wa ziada, na akawa daima ni mtu wa mwisho kutoka na kufunga mwenyewe.

 

Elimu ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa zina athari kubwa sana katika maisha ya Shaykh kielimu na kiutendaji. Na ikamuelekeza katika Manhaj (Njia, mwenendo) Sahihi; ambao ni kuchukua kutoka kwa Allaah (Qur-aan) na Mtume Wake (Sunnah) tu. Akipata usaidizi wa ufahamu wa vyanzo hivyo viwili vikuu kutoka kwa Maimaaam wanachuoni katika wema waliotangulia (As-Salafu As-Swaalih) bila kuwa na ta’asub (kasumba) ya kumshabikia yeyote miongoni mwao au kumponda yeyote, bali msimamo wake ulikuwa ni kuchukua haki popote ipatikanapo na kwa yeyote itokapo.

Na kwa sababu hiyo ndivyo alivyoanza kuyaacha na kuyaweka pembeni madhehebu ya Kihanafi aliyokulia nayo na aliyosomeshwa na baba yake. Na alikuwa baba yake (Allaah Amrehemu) akivutana sana naye kuhusiana na masuala hayo ya kimadhehebu, kwani baba yake alikuwa ameshikilia kwa nguvu sana msimamo wa Kihanafi na hataki kusikia msimamo mingine japo ikiwa sahihi katika masuala mengine. Na Shaykh alijaribu sana kumfahamisha baba yake kuwa anapaswa kufanyia kazi Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) endapo itathibiti usahihi wake, na kuacha ya wengine wote kama hayawafikiani na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

VITABU VYAKE

 

Maktaba za Kiislam zimeneemeka kwa vitabu vingi vya Shaykh haswa vile vikubwa vyenye mijalada mingi vya ‘Silsilatul Ahaadiyth Asw-Swahiyhah’ na ‘Silsilatul Ahaadiyth Dhwa’iyfah wal Mawdhuw’ah’ na kitabu chake cha Swalah kiitwacho ‘Swiftatus Aswalaat An-Nabiy’ ambacho kimepokelewa kwa nguvu sana na wasomaji pande zote za ulimwengu, haswa vijana. Ni mojawapo ya vitabu vizuri na muhimu sana katika mafunzo ya Swalah kama ilivyoswaliwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Pia Shaykh ana vitabu maarufu sana vya Hadiyth vyenye kuvifanyia sharh, tahkiki, na hata kubainisha yale ya sahihi na ya dhaifu ndani ya vitabu hivyo, kama alivyofanya kwenye vitabu Sunnan At-Tirmidhy, Sunnan Ibn Maajah, Sunan Abu Daawuud n.k. Vilevile ana mijalada mingi ya vitabu kama tutakavyoona hapo chini kwenye orodha fupi. Vilevile ameweza kutoa vitabu vya kufafanua na kusahihisha vitabu maarufu vya wanachuoni wakubwa wa karibuni kama vitabu ‘Tamaamul-Minnah Fiyt-Ta’aliyq ‘Alaa Fiqhis-Sunnah’ kilichokuwa ni masahihisho ya Hadiyth zisizo sahihi katika kitabu cha Shaykh Sayid Saabiq kitwacho ‘Fiqhus-Sunnah’, na ana kitabu cha ‘Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal Haraam’ ambacho ni usahihisho wa Hadiyth zilizomo katika kitabu cha Shaykh Yuusuf Al-Qaraadhwaawiy kiitwacho ‘Al-Halaal Wal Haraam Fiyl Islaam’.

 

Kazi zake za uandishi kuhusu masuala ya Hadiyth zinazidi zaidi ya mia.

 

Baadhi ya vitabu vyake vilivyoenea sana ni:

1- Silsilatu Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (Mijalada 1-11)

2- Silsilatu Ahaadiyth Adhw-Dhw’iyfah wal Mawdhuw’ah (Mijalada 1-14)

3- Al-Irwaa Al-Ghaliyl (Mijadala 1-9)

4- At-Targhiyb wa Tahiyb (Mijalada 1-4)

5- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan Abu Daawuud (Mijalada 1-4)

6- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan At-Tirmidhy (Mijalada 1-4)

7- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan Ibn Maajah (Mijalada 1-4)

8- Mukhtaswar Swahiyh Al-Bukhaariy

9- Mukhtaswar Swahiyh Muslim

10- Sharhu Al-‘Aqiydah Atw-Twahaawiyah

11- Ahkaam Al-Janaaiz

12- At-Taswul: Anwa’uhu wa Ahkaamuhu

13- Kitaabu As-Sunnah

14- Swalaatu At-Taarawiyh (Qiyaamu Ramadhwaan)

15- Tamaamul-Minnah Fiyt-Ta’aliyq ‘Alaa Fiqhis-Sunnah

16- Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal Haraam

17- Adaabu Az-Zafaaf [4]

18- Swifatu Asw-Swalaatin-Nabiy [5]

 

KUENEZA KWAKE ELIMU 

 

Na baada ya Al-Imaam, Al-Muhadith, Shaykh Abu ‘Abdir-Rahmaan Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy kupata elimu yake akaanza kuwasiliana na watu kwa ajili ya kueneza Da’awah. Alibeba bendera ya Tawhiyd na Sunnah, na akatembelea Mashaykh wengi waliopo Damascus na kubadilishana nao mawazo na kujadili masuala mbalimbali ya kielimu haswa katika nyanja za Tawhiyd, na pia masuala ya kufuata madhehebu kibubusa (bila dalili), masuala ya bid’ah katika dini na mengine mengi ambayo ni gogoro katika jamii za Kiislam popote ulimwenguni.

Hali hiyo ya kusimamia haki na kupambana na batili ilimjengea Shaykh heshima kubwa na vipenzi wengi ingawa pia hawakukosekana wapinzani wasiotaka haki. Waliompinga ni wale wenye kufuata hawaa za nafsi zao, kasumba za kimadhehebu, mapenzi ya bid’ah na wapinzani wa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na Mashaykh wa aina hiyo walijaribu kumpinga na kumtilia fitna serikalini na kusababisha Shaykh kutiwa jela mara kadhaa, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 1967M kwa muda wa mwezi mmoja, na kisha akaja kufungwa tena kwa muda wa miezi sita.

 

Kilipoanzishwa chuo kikuu cha Madiynah Al-Munawarah huko Saudi Arabia, mwanachuoni mkubwa huko, Shaykh Muhammad Ibraahiym Aalu Shaykh aliyekuwa Rais wa baraza la Maulamaa na aliyekuwa mkuu wa chuo hicho, alimchagua Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni mwalimu wa elimu ya Hadiyth na vigawanyo vyake katika chuo hicho.

 

Miongoni mwa athari zake Shaykh Al-Albaaniy, aliweka msingi na kanuni ya fani la somo la elimu ya ‘Isnaad’ na akawa ndiye wa kwanza kabisa kufanya hivyo katika vyuo vyote vya Kiislam, na chuo cha Madiynah Al-Munawarah kikawa ni kinara cha vyuo vingine kwa hilo. Na hakika Ikhlaasw yake ndiyo iliyoacha athari kubwa duniani na kumjengea umashuhuri mkubwa na heshima kwa wengi. Hata hivyo, ilimuathiri kwa wale waalimu waliotawaliwa na ubinafsi na hivyo kumfanyia hila mbalimbali na majungu kwa wakuu wa chuo hadi ikafikia chuo kutumbukia katika mtego wa hao wenye husda na kuamua kumsimamisha Shaykh kwa madai kuwa anahamasisha vijana kutumia ‘mkono’ katika kuondosha munkari katika jamii. Kuna tukio la baadhi ya wanafunzi wake kwenda kuvunja na kuchoma moto maduka yanayouza video za sinema za makafiri zisizo na maadili na kanda za miziki katika mji mtakatifu wa Madiynah.

Tukio hilo lilifanywa na wanafunzi kwa hamasa za kupenda haki pamoja na kuwa Shaykh hakuwatuma kufanya hivyo. Vijana hao – kama alivyo Muislam yeyote mwenye wivu na Dini yake na pia ardhi hiyo takatifu – hawakupenda kuona ardhi yao ikiwa imejaa uchafu na athari za kikafiri.

 

Uongozi wa chuo ulimlazimisha Shaykh kulaani kitendo hicho, lakini Shaykh hakutoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo na hivyo kusababisha uongozi kumnyang’anya wadhifa aliokuwa nao na kumfukuza.

 

Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa wakamuomba tena arejee nchini Saudia na kufundisha tena, na Shaykh bila kuwa na kinyongo kwa dhulma aliyofanyiwa awali, aliitikia wito huo na kurejea na kufanya kazi yake kwa Ikhlaasw kubwa. Haukupita muda akasimamishwa tena!

 

Pamoja na matukio hayo, inatubainikia wazi kuwa Shaykh hakuwa ni kama wale waalimu wanaosomesha kwa ajili ya ajira tu. Yeye alisomesha na kuhakikisha yanafanyiwa kazi yale anayosomesha, ndio maana elimu yake ikawa na taathira kubwa kwa wanafunzi wa chuo hicho na hata ulimwengu mzima hivi leo. Vilevile, kama tutakavyoona mwisho wa Historia hii yake, ni kwamba, Shaykh hakuweka kinyongo kwa yote aliyotendewa na uongozi na baadhi ya wenye fitna wasiopenda haki na mabadiliko, bali aliacha wasia wa kuhamishwa maktaba yake yote kubwa yenye vitabu vingi na tafiti mbalimbali, kupelekwa katika chuo cha Madiynah Al-Munawarah kuwafaa wanafunzi na watafutao elimu. Alikuwa na Ikhlaasw isiyo na mfano.

 

SAFARI ZAKE

 

Shaykh (Allaah Amrehemu) alihama kutoka Damascus, Syria alipokuwa akiishi, na kuelekea ‘Ammaan, Jordan katika mwezi wa Ramadhaan 1400H. Akakaa kwa muda na kisha akaamua kurejea tena Damascus na kutoka huko akaelekea Beiruut, Lebanon, na baada ya muda akahama huko na kuelekea Al-Imaraat Al-‘Arabiyah Al-Muttahidah (United Arab Emirates). Huko alikaribishwa kwa heshima kubwa na taadhima na wale vipenzi vyake walioko huko ambao ni watu walioshikamana na mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Wakamkirimu kwa kila hali katika Jumuiya yao ya Daarul-Birr, na masiku aliyokaa hapo – kama kawaida yake – aliyatumia kuwaelemisha Waislam kwa juhudi zake zote kuanzia anapoamka kwa Swalah ya Alfajiri hadi anapolala usiku.

Katika kukaa kwake hapo United Arab Emirates, aliweza kupata fursa ya kusafiri nchi za jirani na kukutana na wanachuoni wakubwa na Mashaykh waliokuwa nchini hapo na  nchi ya jirani ya Qatar na kuweza kubadilishana mawazo na kujadili masuala mbalimbali ya Dini.

Akarejea tena Damascus na ziara yake ya mwisho ya nchi ya United Arab Emirates ilikuwa ni mwaka 1989M ambako alikwenda kukaa nje ya mji kwenye Jumuiya ya Daarul-Birr kwenye shamba la kiongozi wa Jumuiya hiyo na kufanya darsa zake mbalimbali hapo katika msikiti uliokuwepo hapo ambao baadaye ulipewa jina la Shaykh kwa kumbukumbu za ziara zake za kielimu hapo, na pia kuuenzi mchango wake na elimu yake kubwa.

 

Katika mwaka 1419H, mwaka mmoja kabla ya kifo chake, Waislam duniani walifarijika kuona Shaykh akitambuliwa kimataifa kwa kupewa tunzo kubwa la kielimu na mchango katika Dini, itambulikanayo kama, ‘Tunzo La Mfalme Fayswal La Kimataifa’. Ambalo kinatolewa kila mwaka katika mchango wa nyanja mbalimbali za jamii, na kwa upande wa Dini hutolewa kwa yule mwanachuoni mkubwa katika Ummah wa Kiislam katika elimu maalum ya Dini. Na mwaka huo Ash-Shaykh, Al-Imaam, Al-Muhadith, Al-‘Alaamah Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) alitunukiwa jaiza hiyo kwa mchango wake mkubwa wa elimu ya Hadiyth na vigawanyo vyake.

 

Tunzo hilo kubwa la kimataifa halikuwashangaza wanachuoni wengi kupewa Shaykh Al-Albaaniy, bali kilichowashangaza ni kuchelewa Shaykh kutambulika na kupewa tunzo kama hilo muda mrefu nyuma kwa jinsi walivyokuwa wakiitambua elimu yake kwa muda mrefu.

Hiyo itakumbukwa na wengi kuwa ilikuwa ni hadhi kubwa ya heshima ya kuukubali mchango wake wa Dini hii aliyopewa na nchi ya Saudi Arabia pamoja na kwamba walimfukuza nchini humo mara mbili kutokana na msimamo wake thabiti usioyumba wa kusimamia Al-Kitaab (Qur-aan) na As-Sunnah pamoja na misimamo yake mingine ya kielimu iliyokuwa ikipingana na Mashaykh wa Saudiyah. Alikuwa anajali zaidi kumridhisha Allaah tu Pekee. Pamoja na hivyo, Mashaykh wa Saudiyah walikuwa wakimheshimu sana na kumpenda kama tutakavyoona mwisho katika kauli zao kumhusu Shaykh.

 

UPINZANI

 

Kama tulivyoona nyuma, kuwa Shaykh alikuwa akipata upinzani mbalimbali tangu alipokuwa kwenye nchi yake hadi alipokwenda nje kufundisha na kueneza elimu. Na wengi waliokuwa wakimfanyia uadui na hata kumfanyia fitna kwenye serikali tawala, ni wale waliokuwa wanatetea yale mambo yasiyo na dalili wala uthibitisho katika Dini. Wanachuoni walioweka matamanio ya nafsi zao mbele na kuendekeza uluwa wa kidunia na kuimarisha bid’ah katika Dini, ndio waliomchukia Shaykh kwa sababu yeye alikuwa mstari wa mbele kuyapinga maovu hayo na kuyabaini kwenye vitabu vyake. Watu wa bid’ah na matamanio ya nafsi zao, ndio waliokuwa wakimfanyia chuki na majungu hadi akafungwa jela na hata kuchukiwa na wachache wenye kuendekeza batili.

 

Mmoja katika waliokuwa wakikesha kumpiga vita Shaykh, ni kiongozi wa Kisufi aitwaye Hasan bin 'Aliy As-Saqaaf ambaye alikuwa huko Jordan na ndio katika waliochangia sana kumfanyia Shaykh majungu mengi ambayo hakika hayakusaidia kumuharibia Shaykh zaidi ya kumfanya ajulikane zaidi na watu wapate kuvijua na kuvisoma vitabu vyake ambavyo viliwafanya wamuheshimu badala ya kumchukia!

 

As-Saqaaf alitunga vitabu kumkosoa Shaykh kwenye masuala ya Hadiyth, na pia baada ya yeye kuona mafanikio makubwa ya kuenea na kununuliwa kwa wingi kitabu cha Shaykh kiitwacho ‘Swifatus-Swalaat An-Nabiy’, As-Saqaaf akaandika kitabu dhidi ya hicho! Hata hivyo, vitabu vyake vilijibiwa kielimu sana na wanafunzi wa Shaykh Al-Albaaniy. Moja ya vitabu vyenye majibu mazuri kujibu tuhuma za As-Saqaaf ni kile kilichoandikwa na Shaykh ‘Aliy Hasan Al-Halabiy.

As-Saqaaf licha ya kumshambulia Shaykh Al-Albaaniy, vilevile kuna mengi kayaandika kwenye vitabu vyake kushambulia baadhi ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). [6]

 

Shaykh Al-Albaaniy katika sifa zake kubwa ni kukabiliana na wote wanaopingana naye na kufanya nao mijadala yenye hoja na dalili. Na hivyo ndivyo alivyofanywa kwa As-Saqaaaf. Alikwenda nyumbani kwa As-Saqaaf baada ya mapatano ya kwenda kujadili mada kuhusu ‘At-Tawasul’, na alipofika kwake akakuta kinyume na alivyotarajia kwa kudhani kuwa Shaykh As-Saqaaf ni katika ‘wajukuu wa Mtume’ kama ajiitavyo, ingawa vitendo alivyovikuta – kama anavyosema mwenyewe – havikuwa kama vya babu yake [yaani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)], kwani vitendo vyake vilikuwa vya kiburi, ukubwa, ufakhari na kupenda kutukuzwa.

 

Shaykh Al-Albaaniy alipotaka waanze mjadala huo uliomleta hapo, As-Saqaaf akawa anazunguka huku na kule kwa mada zingine bila kuzungumzia walichopanga awali. Na Shaykh kwa utulivu, alivumilia yote na mwisho kuondoka bila kufikia alilolifuata. Na baada ya hapo, As-Saqaaf akawa anamtukana Shaykh Al-Albaaniy kwenye kanda, vitabu na majukwaani. Shaykh Al-Albaaniy hakuwahi kumtukana wala kuandika vitabu vya kumtukana kama alivyofanyiwa yeye. Insaafu hiyo na uadilifu mkubwa wa Shaykh ulimzidishia sana vipenzi na kukubalika.

 

Tukio moja lilinidhirishia utukufu wa hali ya juu sana wa Shaykh Al-‘Alaamah, nilipokuwa nasikiliza mawaidha yake, na haswa majibu ya maswali na matukio mbalimbali aliyokuwa akikabiliana nayo nyumbani kwake – nyumba ambayo mlango wake ulikuwa wazi masaa yote kwa wageni – pale alipotembelewa na wawakilishi wa As-Saqaaf. Wageni hao walijitambulisha kuwa wao ni vijana na wanafunzi wakubwa wa As-Saqaaf.

 

Shaykh aliwapokea vizuri sana kwa heshima kubwa. Na katika mazungumzo waliyokuja nayo ni mijadala mbalimbali kuhusu masuala ya ‘Aqiydah na huku wakimtuhumu Shaykh kuwa anamfananisha Allaah na viumbe, na masuala mengine mbalimbali. Shaykh kwa upole na bashasha alianza kuwauliza waliposikia hayo na ushahidi wake, wakawa hawana, na akaendelea kujadiliana nao kwa masaa yasiyopungua manne, kwa mjadala mkali wa kielimu bila Shaykh kukasirika wala kuchoka na mwishowe vijana hao waliondoka kwa Shaykh kwa heshima kubwa sana na kumuomba Shaykh aandike kitabu kuhusu ‘Aqiydah ili aweke wazi msimamo wake kuhusu sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) maana baadhi ya watu wanamtungia uongo na kumtuhumu. [7]

 

Huo ni mfano wa mwanachuoni wa aina ya nadra sana katika ulimwengu huu.

 

Vilevile Shaykh Al-Albaaniy aliwahi kujadiliana na mahasimu zake wengine kama kiongozi mwengine wa kisufi wa Syria, Dr. Muhammad Sa'iyd Ramadhaan Al-Buutwiy ambaye anapinga sana mtu kutokuwa na madhehebu na ameandika vitabu vya kushambulia watu wenye kutotaka kujinasibisha na madhehebu maalum. Shaykh Al-Albaaniy alijaribu mara nyingi kumwandikia barua ya kukutana naye na kuyajadili masuala hayo na mengineyo lakini ilichukua muda mrefu hadi Al-Buutwiy kukubali. Walikutana kwenye mjadala uliodumu masaa matatu na mwisho wa mjadala Al-Buutwiy alidhihirika kuwa hoja zake zilikuwa dhaifu na akakataa mjadala mwengine alioombwa na Shaykh Al-Albaaniy. [8]

 

UHUSIANO WAKE NA WANACHUONI

 

Imaam Al-Albaaniy alichunga sana heshima na mahusiano bora na Maulamaa wenzake. Mahusiano aliyokuwa akiyajenga kwa misingi ya haki na ukweli. Aliwaheshimu wanachuoni wenzake na kujifunza mengi kutoka kwao. Hakuwastahi katika haki haswa pale wanapokosea. Alikuwa ana njia nzuri za kukosoa na kutoa nasaha kwa wenzake. Alipokuwa anapata kitabu cha mwanachuoni mwenzake na kukuta ndani kuna makosa ya ‘Aqiydah, Hadiyth au Fiqh, alikuwa hachelewi kuwasiliana nao kwa maandishi, kwa simu, au hata kuwafuata mwenyewe japo wanaishi mji au nchi za mbali na alipo yeye.

 

Mifano mizuri ya hili, ni barua zake kwa Mashaykh mbalimbali kama Shaykh Muhammad Mitwaliy Ash-Sha’arawiy aliyekuwa Misr, Shaykh Sayyid Saabiq aliyekuwa Misr vilevile, Shaykh Yuusuf Al-Qaaradhwaawiy (Mmisr) ambaye hivi sasa ni Mufti wa nchi ya Qatar na kiongozi wa Umoja wa Maulamaa Duniani. Pia aliwahi kukutana nao uso kwa uso.

 

Vile vile aliandika vitabu vya kusahihisha Hadiyth zilizomo kwenye vitabu vya Mashaykh hao. [9] Pia alikuwa anawasiliana na Mashaykh wakubwa wa Saudia kama Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Allaah Amrehemu) na kujadili masuala mbalimbali ya ki-Fiqh. Pamoja na kutofautiana kwao lakini bila kugombana wala kupunguza mapenzi baina yao kama tutakavyoona mwisho maoni ya Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Allaah Amrehemu) na wengineo kuhusu Shaykh Al-Albaaniy.

 

FADHILA NA MEMA YAKE

 

Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) alikuwa ni mwenye kufuata mwenendo wa watangu wema (Salafus-Swaalih), akifuata matendo yao na tabia zao, na yakawa macho yake yanafuata kile kilichosemwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Alikuwa hastahi katika haki, akiitangaza haki katika vitabu vyake na mihadhara yake. Na hii ni sifa ya nadra sana kuipata katika ulimwengu wa leo, ambao wengi hawapendi kusema haki kwa kuchelea kuwaudhi wengine au kupoteza kukubalika. Na Shaykh alikuwa akijirudi pindi anapokutana na dalili sahihi inayokwenda kinyume na kauli yake, na huiacha kauli yake na kufuata dalili hiyo iliyosihi bila kuangalia imetoka kwa nani. Kuna baadhi ya Hadiyth alizokuwa akiitakidi ni sahihi kwa elimu yake, na baadaye zikambainikia au akatanababishwa kuwa si sahihi, akawa anajirudi haraka na kukubali na kuzitaja katika vitabu vyake. Sifa hiyo pamoja na uzuri wake, lakini kuna waliokuwa na chuki wakatumia kumtilia kasoro na kudai kuwa ‘anajigongagonga’, na hadi wakaandika vitabu kumkosoa kwa sababu hiyo!!

 

Sifa hiyo ndiyo waliyokuwa nayo Maimaam wanne wa Sunnah, ambao misimamo yao ni pale ilipothibiti dalili sahihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Walikuwa na kauli nyingi kuhusu hayo, hapa nitaziorodhesha chache:

Imaam Abu Haniyfah (Allaah Amrehemu)

"Ikiwa Hadiyth imeonekana kuwa ni sahihi, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu" "Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kukubali rai zetu ikiwa pindi hawatojua wamezipata kutoka wapi". [10]

Katika riwaya nyingine: "Imekatazwa mtu ambaye hajui dalili zangu kutoa hukmu kutokana na maneno yangu"

Katika riwaya nyingine imeongezwa: "….Kwani sisi ni wanaadamu, tunasema jambo siku moja na kulirudisha siku ya pili yake".

 

Imaam Maalik naye (Allaah Amrehemu)

"Hakika mimi ni mwanaadamu: Ninafanya makosa (mara nyingine) na ninakuwa sahihi (mara nyingine). Kwa hiyo, tazameni rai zangu: zote ambazo zinakubaliana na Kitabu (Qur-aan) na Sunnah, zikubalini; na zote ambazo hazikubaliani na Kitabu (Qur-aan) na Sunnah, basi zipuuzeni". [11]

 

Imaam Ash-Shaafi’iy (Allaah Amrehemu)

"Ukiona katika maandishi yangu jambo ambalo ni tofauti na Sunnah ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi zungumza kwa kurejea Sunnah ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na acha niliyoyasema mimi"

Katika usimulizi mwengine: "…basi ifuate (Sunnah) na usitazame tena pembeni kufuata usemi wa mwingine yeyote" [12]

Na akasema:

“Hadiyth ikipatikana kuwa ni sahiyh, basi hiyo ndio madhehebu yangu" [13]

 

Imaam Ahmad bin Hanbal (Allaah Amrehemu)

Msifuate rai yangu, wala msifuate rai ya Maalik, au Ash-Shaafi'iy au ya Awzaa’iy, wala Thawriy, lakini chukueni kutoka walikotoa" [14]

 

Na sifa hiyo waliyokuwa nayo hao Maimaam wanne wakubwa na yeye kuifuata ndiyo iliyomfanya Shaykh kupendwa na kupata wafuasi wengi kila pande ulimwenguni. Na ndiyo iliyomfanya kupata wenye chuki dhidi yake.

 

Shaykh ameacha athari kubwa katika elimu ya Hadiyth hadi imefikia sasa wanachuoni wengi wanapotaja Hadiyth basi hawaachi kutaja usahihi au udhaifu wa Hadiyth hiyo kwa mujibu wa uchambuzi wake.

 

Alikuwa haachi kufunga Swawm za Sunnah haswa za Jumatatu na Alkhamiys katika maisha yake ila tu alipokuwa safarini. [15]

 

Nyumba yake ilikuwa ‘ingia toka’ ya watu wa kila aina waliokuwa wakija kwake kutafuta elimu, kuuliza masuala ya Dini, kutatuliwa masuala ya kijamii, kifamilia, na hata kuhitaji misaada mbalimbali pamoja na kuwa hali ya Shaykh ilikuwa ya wastani, hata hivyo, alikuwa haachi kuwasaidia wanaomfuata kwa shida.

 

Shaykh alikuwa baadhi ya nyakati akitaja jinsi alivyokuwa siku za nyuma akiokota makaratasi njiani au kadi zilizotupwa au kupekua kwenye sehemu zilitupwa karatasi ambazo alikuwa akizitumia kuandikia Hadiyth. Yote ni kutokana na hali ya umaskini na shida kwa kutokuwa na uwezo wa kununua madaftari ya kuandikia.

 

Alikuwa akichunga sana wakati. Hakuwa akiacha sekunde ya maisha yake ipite bila kuifanyia kazi na kuchuma ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Alikuwa mwingi wa kufanya dhikr, kuelimisha, na kujifunza kutoka kwa wengine.

 

Sifa yake ya kujifunza ilikuwa haina mithali! Alikuwa akitumia zaidi ya masaa kumi na nane (18) kwa siku katika maktaba yake kupitia na kufanya rejea mbalimbali, kutafiti na kuandika! Muda aliokuwa akikatisha masomo yake na utafiti wake ulikuwa ni wa kuswali na kula kidogo.

 

Waliobahatika kukutana na Shaykh wanashuhudia utaratibu wake na heshima yake na ucha Mungu wake wa hali ya juu. Alikuwa haachi fursa bila kumfundisha mtu kitu kipya au kumkosoa makosa yake kwa utulivu na busara. Siku moja alipokuwa Hospitali amelazwa, Daktari aliyekuwa amenyoa ndevu zake zote akaingia na kumpa dawa na baada ya kumaliza akiwa anaondoka, akamuomba Shaykh amuombee Du’aa, Shaykh akaomba na kusema “Namuomba Allaah Akupendezeshe kwa kile kinachompendeza mwanaume”

[Makusudio ya Shaykh hapa yalikuwa ni kuwa yule Daktari apendezeshwe kwa kuongozwa kuweka ndevu, kwani ni jambo lililosisitizwa sana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)]. [16]

 

Alikuwa Shaykh kila alfajiri akipita na gari lake kwenye nyumba za wanafunzi wake kuwaamsha kwa ajili ya Swalah ya Alfajiri. [17]

 

Kwa kuchelea kwake ‘Riyaa’, wakati mmoja alijiwa na ujumbe wa watu kutoka Bangladesh na kumwalika akafanye ziara ya wiki moja kutoa mihadhara kwa watu waliokuwa wakimsubiri ambao idadi yao ilikuwa haipungui milioni nne! Shaykh alishtushwa sana na akakataa kabisa. Ujumbe ule ukamuomba akubali japo siku tatu. Shaykh akakataa! Wakamuomba siku moja, akataa! Mwisho wakamwambia basi kwa mhadhara mmoja tu kisha watampakia kwenye ndege arudi siku hiyo hiyo. Shaykh hakukubali na ujumbe ukaondoka ukiwa na huzuni kubwa. Alipoulizwa Shaykh sababu iliyomfanya akatae fursa hiyo kubwa ya kutoa elimu kwa watu wengi kiasi hicho, Shaykh akajibu: “Watu milioni nne wananisubiri! Je, nitasalimika na Riyaa katika hali kama hiyo?”.

 

Alikuwa akiendesha baiskeli yake kutoka Damascus kuwafuata Waislam kwenye vitongoji vingine, akiendesha kwa masafa ya kilomita 45 kwa ajili ya kwenda kutoa elimu.

 

Alikuwa akiingia msikitini siku ya Ijumaa, akiswali Raka’ah mbili mbili za Naafilah (Sunnah) na akiendelea hadi Khatwiyb atakapopanda minbar kuanza kutoa Khutbah. [18]

 

Shaykh inasemekana alikuwa katika daraja ya Al-Haafidh (Mwanachuoni wa Hadiyth aliyehifadhi Hadiyth laki moja (100,000) pamoja na mnyororo wa wapokezi wake na ‘mutuun’ zake (maneno ya kila Hadiyth). Hayo yanaelezwa na Shaykh ‘Ashiysh aliyemuuliza suala hilo na Shaykh akakataa kumjibu kwa unyenyekevu na kutotaka kujifakharisha, alichojibu baada ya kukazaniwa sana swali hilo, alijibu kwa Aayah hii: {{Na neema yoyote mliyonayo inatoka kwa Allaah}} An-Nahl: 56. [19]

 

Katika wasia wake Shaykh alitoa hadiya maktaba yake ya vitabu na kazi zake za uandishi kuitunuku Chuo Kikuu Cha Madiynah Al-Munawarah kama anavyosema katika wasia wake: “Nimeiachia maktaba yangu – vyote vilivyomo, vikiwa ni vilivyochapishwa tayari, au nakala, au kazi nilizoziandaa kuchapishwa; kwa maandishi ya mkono wangu, au ya mwengine aliyeniandikia – kwa kuipa maktaba ya Jaami’atul-Islaamiyah (Chuo Cha Kiislam) kilichopo katika mji wa Madiynah Al-Munawarah. Kwa sababu ni kumbukumbu nzuri na chuo hicho wakati nilipokuwa huko nikifundisha, kwa kulingania kwake kwa msingi wa Kitaab (Qur-aan) na Sunnah kwa kufuata mwenendo (Manhaj) wa wema waliotangulia (Salafus-Swaalih)”. [20]

 

Alikuwa hapendi kuitwa mwanachuoni na mara nyingi akijiita ‘Twaalibul-‘Ilm’ Mtafutaji elimu.

 

Siku moja mwanamke kutoka Algeria alimpigia simu na kumwelezea kuwa mwenzake (dada wa Kiislam) kamuota kwenye ndoto, akiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) jambo lililomfanya Shaykh alie sana na kushindwa kuzungumza kwenye simu. (“Mazungumzo ya simu katika kipindi cha maswali na majibu”. Unaweza kusikiliza mazungumzo hayo hapa). [21]

 

Shaykh alipambana na kila aina ya upotofu na moja ya aliokumbana nayo ni mtu mwenye kudai utume. Kwa utulivu bila hasira wala kutaka kumlaani na kumshambulia pamoja na kuwa ni dai la ukafiri ulio wazi. Shaykh alimsikiliza kwa makini na kumuuliza maswali na kuzikatakata hoja zake hadi mwisho baada ya masaa, yule mtu akaomba Tawbah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Unaweza kusikiliza mjadala huo hapa. [22]

 

Alijiwa na watu waliokuwa wakimtukana na kumuita kafiri, na bila kukasirika na kugombana nao akajadiliana nao kwa upole na mapenzi na ilipofika wakati wa Swalah wakakataa kuswalishwa naye, yeye hakukasirika bali aliomba mmoja wao aswalishe na yeye atamfuata! Baada ya Swalah hiyo wakaendelea na mjadala na ilipofika Swalah nyingine, wao wenyewe wakamuomba Shaykh awaswalishe!! Akawa kwao si kafiri tena, bali mwanachuoni mwenye kuheshimiwa kabisa na wao.

 

Alikuwa mtu wa kawaida sana, mnyenyekevu asiye na makuu na asiyeweza kuonekana tofauti na watu wengine ila kwa vitendo na maongezi yake ya kielimu.

Katika kipindi cha maisha yake, alifanya tafiti nyingi na kuzichambua taqriban nyororo 30,000 za wasimulizi wa Hadiyth (isnaad) za Hadiyth zisizo na idadi, akiwa ametumia kiasi cha miaka 60 ya umri wake kusoma na kupitia vitabu vya Sunnah na kuwa karibu navyo kwa muda wote huo, na mawasiliano ya nyanja hiyo, na pia kuwa karibu na Maulamaa wa elimu hiyo. [23]

Wanachuoni wengi walimuheshimu sana na kumtegemea katika masuala ya uchambuzi na uhakiki wa Hadiyth na wakawa wanamtumia kusahihisha vitabu vyao walivyoviandika. Shaykh Muhammad Mustafa ‘Azami (Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Hadiyth katika Chuo kikuu cha Makkah) alimchagua Shaykh kupitia vitabu vyake vinavyofika mijalada minne ili ahakikishe usahihi wake na pia kuweka maelezo yake ndani. Huo ilikuwa ni ushahidi kutoka kwa Maulamaa kuiamini elimu yake na ubingwa wake wa Hadiyth. Kama ambavyo Chuo Kikuu Cha Madiynah kilipomchagua yeye kukupitia na kuhakiki na kuweka maelezo yake kwenye kitabu maarufu cha Hadiyth kiitwacho ‘Mishkaat Al-Maswaabiyh’. [24]

Aliwaheshimu sana wanachuoni wenzake na kuwaenzi. Siku moja aliletewa habari za masikitiko makubwa kutoka kwa mwanafunzi wake maarufu Shaykh ‘Aliy bin Hasan Al-Halabiy kuhusu kifo cha mwanachuoni mkubwa wa zama hizo, Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Allaah Amrehemu), Shaykh Al-Albaaniy alibubujikwa na machozi na kuomba: ((Innaa Lillaahi wa innaa ilayhi raaji’uun; Allaahumma Ajurniy fiy muswiybatiy wa Akhlifniy khayram minhaa))

[Kwake Allaah tumetoka na Kwake ndio tutarejea. Ee Allaah, nilipe kwa msiba wangu huu na nibadilishie bora kuliko hicho (ulichokichukua)] Hii ni Du’aa inayoombwa na yule aliyepewa taarifa ya kifo kama ilivyofundishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [25]

 

KIPINDI CHA MWISHO CHA MAISHA YAKE

Shaykh (Allaah Amrehemu) hakutulia kutafuta elimu hadi umri wa miaka 86, akisoma, akifundisha, akielimisha akiandika vitabu, akiandika barua kwa wanachuoni wenzake kuwapongeza, kuwanasihi, kuwakosoa makosa ya vitabuni mwao au fatwa zao. Hakuwa hadi umri huo akiacha kutafiti masuala ya Hadiyth, akipangua sahihi na dhaifu na za kutungwa, aliweza kuvigawa vitabu vingi vikubwa vya Hadiyth kama vya Maimaam Abu, Dawuud, Ibn Maajah, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na wengineo, akaweza kuvigawa Sahihi zake na Dhaifu zake na kuwasaidia kuwarahisishia wenye elimu na wanafunzi katika uandishi wao na katika tafiti zao.

 

Shaykh ameshukuriwa sana kwa kazi hiyo iliyosaidia Ummah leo hii, na kuamsha Ummah leo kujua Hadiyth sahihi na dhaifu na pia kuwafanya wengi wapate kuwa karibu na kuifuatilizia elimu ya Hadiyth na sayansi yake.  Aliyafanya yote hayo – kwa sababu moyo wake ulikuwa umefungamana nayo hayo kwa mapenzi ya juu – na hakuacha hadi taqriban miezi miwili ya mwisho ya maisha yake, alipokuwa dhaifu akiugua kitandani. Pamoja na magonjwa mazito yaliyomdhoofisha sana na kuwa hatoki kitandani, hakuacha kusoma wala hakupoteza kumbukumbu zake, akiwa anamjua kila aliyekwenda kumtazama, akimuita kila mmoja kwa jina lake! Hadi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipoirejesha roho yake na akamfisha katika nyakati za mwisho za Alasiri, siku ya Jumamosi, tarehe 22 katika mwezi wa Jumaadah Al-Aakhirah, mwaka 1420H sawa na 10-02-1999M huko ‘Ammaan, Jordan.

 

KIFO CHAKE NA JINSI KILIVYOATHIRI UMMAH

Alizikwa siku hiyo hiyo aliyofariki, pamoja na kuwa alizikwa usiku, lakini idadi ya watu ilikuwa kubwa kuweza kuzidi maelfu kwa maelfu. Aliswaliwa katika ‘Muswallaa’ (Eneo la wazi la kuswaliwa nje ya msikiti) kama ilivyo Sunnah. Aliswaliwa haraka kama alivyoacha maagizo yake kwenye wasia wake aliouacha ambao ndani yake alisisitiza mambo yote ya kifo chake yaendeshwe kwa mujibu wa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Wanachuoni, watafuta elimu, wanafunzi, na watu wa kawaida wote waliathirika sana na kifo cha Shaykh. Taarifa za kifo chake kilipowafikia Waislam, majonzi yalienea pote na wengi kuhisi kuwa ile elimu na yule ‘Mujaddid’ (Mkarabati wa Dini) wa zama atakuwa hayupo tena na wao. Mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa huzuni, kwa kutanguliwa na kifo cha Mwanachuoni mkubwa wa zama hizo hizo ambae ni Mufti wa Saudia wa wakati huo, Shaykh Al-‘Alaamah ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdullaah bin Baaz, na baada yao kufuatiwa na kifo cha Mwanachuoni Faqiyh Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn, na Mashaykh wengine wakubwa waliofariki mwaka huo ni, Shaykh Swaalih bin 'Aliy Ghaswuun, Shaykh 'Aliy Twantwawiy, Dkt. Mustwafaa Az-Zarqaa, Shaykh Mana'a Al-Qahtwaan na Shaykh 'Atwiyah bin Muhammad Saalim (Allaah Awarehemu wote hao na Awaweke katika pepo Yake Tukufu).

 

WANAFUNZI WAKE MAARUFU

Wanafunzi wake ni wengi mno na miongoni mwao maarufu katika Mashaykh ni hawa ambao baadhi yao wako hai hadi leo:

Shaykh Muqbil bin Haadiy Al-Waadi’iy (Yemen)

Dkt. ‘Umar Sulaymaan Al-Ashqar (Jordan)

Shaykh ‘Aliy Hasan ‘Abdul-Hamiyd Al-Halabiy (Jordan)

Shaykh Saalim Al-Hilaaliy (Palestina)

Shaykh Hamdiy ‘Abdul-Majiyd

Shaykh Muhammad ‘Iyd ‘Abbaasy

Shaykh Muhammad Ibraahiym Shaqrah (Jordan)

Shaykh ‘Aliy Khushshaan

Shaykh Muhammad Jamiyl Zaynuu (Saudi Arabia)

Shaykh ‘Abdur-Rahmaan ‘Abdus-Swamad

 

Na waliojifunza kwake kwa njia isiyo ya moja kwa moja ni:

Shaykh Muhammad Hasaan (Misr)

Shaykh Abu Is-haaq Al-Huwayniy (Misr)

 

 

SIFA NJEMA WALIZOTOA MAULAMAA KWA MUJADDID WA ENZI HII SHAYKH MUHAMMAD NAASWIR-UD-DIYN AL-ALBAANIY (ALLAAH AMREHEMU)

 

SHAYKH ‘ABDUL-‘AZIYZ BIN BAAZ [ALIYEKUWA MUFTI WA SAUDI ARABIA] (ALLAAH AMREHEMU)

Sikumuona mtaalamu wa Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika enzi yetu ya leo chini ya qubah la mbingu kama mwanachuoni mkubwa Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Aliulizwa kuhusu Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:

"Allaah Hutuma kwa Ummah huu mwanachuoni katika kila miaka mia mtu wa kupiga msasa mambo ya dini Yake". [26] Aliulizwa ni nani mpiga msasa wa karne hii? Akajibu: Ninadhani Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ndiye mpiga msasa wa enzi hii. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

MWANACHUONI MKUBWA MUHAMMAD IBN SWAALIH AL-‘UTHAYMIYN (ALLAAH AMREHEMU)

Yale niliyoyajua kuhusu Shaykh na ambayo ni kidogo wakati nilipokuwa nakutana naye, ni kuwa yeye ana shime ya hali ya juu ya kutumia Sunnah na kupiga vita bid’ah; sawasawa katika ‘Aqiydah au matendo. Ama kwa kusoma kwangu vitabu vyake, hakika nimemjua vyema kwa hayo. Yeye ana elimu kubwa ya Hadiyth kwa upande wa Riwaayah na Diraayah, na Allaah Amewanufaisha watu wengi kutokana na yale aliyoyaandika kwa upande wa elimu, mfumo na mwelekeo katika taaluma ya Hadiyth. Na hii ni faida kubwa sana kwa Waislam. Na Allaah ni Zake Himdi. Ama kwa upande wa uhakiki wake wa kitaaluma katika fani ya Hadiyth, basi hayo hayasemeki. 

 

MWANACHUONI MKUBWA MFASIRI MUHAMMAD AL AMIYN ASH-SHANQIYTWY (ALLAAH AMREHEMU)

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Al-Haddaah anasema:

"Hakika Mwanachuoni mkubwa Ash-Shanqiytwy anamtukuza Shaykh Al-Albaaniy utukuzo wa kushangaza. Anapomuona anapita nailhali yeye yuko katika darsa yake katika Msikiti wa Madiynah, husimamisha darsa lake, husimama na kumsalimia kwa ajili ya kumuheshimu".

 

MTUKUFU SHAYKH ‘ABDUL-MUHSIN AL’ABAADIY (ALLAAH AMHIFADHI)

Bila shaka Shaykh Al-Albaaniy, alikuwa ni katika Maulamaa wa kipekee walioumaliza umri wao katika kuitumikia Sunnah, kuitungia vitabu, kulingania kwa Allaah Mtukufu, kuinusuru ‘Aqiydah ya kisalafiya, kuipiga vita bid'ah, na kuitetea Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yeye ni katika Maulamaa wazuri wenye sifa za kipekee. Sifa zake zimeshuhudiwa na watu maalumu na watu wa kawaida. Na hakuna shaka yoyote kwamba kumpoteza mwanachuoni kama huyu, ni katika misiba mikubwa inayowapata Waislamu. Allaah Amlipe kheri njema kutokana na juhudi zake kubwa na Amweke katika Pepo Yake pana.

  

SHAYKH ‘ABDULLAH AL-UBAYLAAN (ALLAAH AMHIFADHI)

Ninajipa pole mwenyewe, na ninawapa pole ndugu zangu Waislamu kote duniani kwa kufariki Imaam Mwanachuoni Mkubwa Mhakiki Mcha Mungu Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Ukweli ni kwamba maneno hayawezi kumzungumzia mtu huyu. Ninachoweza kukisema ni kuwa yeye hakukulia katika mazingira ya kisalafiya, lakini pamoja na hivyo, amekuwa ni katika walinganiaji wakubwa wa usalafiya, na kufanya mambo kwa mujibu wa Sunnah, na kutahadharisha mambo ya bid'ah. Hata Shaykh wetu ‘Abdullah Ad-Duwaysh anayezingatiwa kuwa ni katika wahifadhiji wachache sana katika enzi yetu na ambaye alifariki akiwa kijana, anasema: "Tokea karne nyingi, hatukumuona mtu kama Shaykh Naaswir kutokana na mengi aliyoyaandika na kuyaelezea, na uhakiki wake ulio bora kabisa. Na baada ya As-Swuyuutwy hadi hivi leo, hakuna aliyeifanyia uhakiki taaluma ya Hadiyth kwa kiasi kikubwa na usahihi kama Shaykh Naaswir.

 

MUFTI WA ZAMANI WA SAUDIA MWANACHUONI MKUBWA SHAYKH MUHAMMAD BIN IBRAAHIYM AAL SHAYKH (ALLAAH AMREHEMU)

Anasema kuhusu Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu): "Yeye ni mwana Sunnah, mpiganiaji haki, na mwenye kupambana na watu wasiofuata haki".

 

MWANACHUONI MKUBWA SHAYKH ZAYD BIN FAYYAADH (ALLAAH AMREHEMU)

Hakika Shaykh Muhammad Naaswiru-ud-Diyn Al-Albaaniy ni katika Maulamaa wakubwa waliochomoza katika enzi hii. Yeye alizishughulikia Hadiyth, njia zake, wapokezi wake na kiwango chake cha kuwa ni sahihi au si sahihi. Na hii ni kazi kubwa ya kheri iliyomaliziwa masaa na kutolewa juhudi kubwa. Na yeye ni kama Maulamaa wengineo wanaopata na kukosea. Lakini kubobea kwake katika taaluma hii tukufu, kumeufanya ubora wake ujulikane, na yeye ashukuriwe kwa kuitilia maanani.

 

MWANACHUONI MKUBWA SHAYKH MUQBIL AL-WAADI'IY (ALLAAH AMREHEMU)

Hakika katika taaluma ya Hadiyth, hakuna mtu kama Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Na Allaah Amenufaisha kwa elimu yake na kwa vitabu vyake mara nyingi zaidi kuliko yale wanayoyafanya wale wenye hamasa na Uislam bila kuwa na elimu ya kutosha, na wasio na msimamo. Na lile ninaloliamini na ambalo ni deni kwangu mbele ya Allaah ni kuwa Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni katika waipigao msasa Dini na ambao wanasadikishwa na neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Allaah Hutuma kwa Ummah huu mwanzoni mwa kila miaka mia mtu wa kupiga msasa mambo ya Dini Yake)). [27]

 

MWANACHUONI MKUBWA WA MISR MUHIBUD-DIYN AL-KHATWIYB (ALLAAH AMREHEMU)

“Na katika walinganiaji wa Sunnah ambao wametoa maisha yao yote kuihuisha hiyo Sunnah ni ndugu yetu Muhammad Naaswir-ud-Diyn Nuuh Najaatiy Al-Albaaniy.

 

MWANACHUONI MKUBWA WA HADIYTH INDIA SHAYKH ‘ABDUS-SWAMAD SHARAFUD-DIYN (ALLAAH AMREHEMU)

Katika moja ya barua walizokuwa wakiandikiana na Shaykh Al-Albaaniy katika masuala ya kitafiti ya Hadiyth, alikiri kuwa Shaykh Al-Albaaniy ni mwanachuoni mkubwa kabisa wa Hadiyth.

 

MWANACHUONI MKUBWA HAMUUD BIN ABDULLAH AT-TUWAYJIRIY (ALLAAH AMREHEMU)

Al-Albaaniy kwa sasa ni bendera juu ya Sunnah. Kumkosoa yeye ni kama kuikosoa Sunnah. Na mara moja katika mnasaba wa kutolewa Tuzo la Kimataifa la Mfalme Fayswal alisema: "Hakika Shaykh Naaswir ndiye anayestahiki zaidi kupewa tuzo hili kwa kuitumikia kwake Sunnah".

 

PROFESA AMIYN AL-MISRIY (ALLAAH AMREHEMU) ALIYEKUWA MKUU WA KITENGO CHA MASOMO YA JUU KATIKA CHUO KIKUU CHA KIISLAM

Ni moja kati ya mikosi ya dunia hii kuchaguliwa watu kama sisi wenye shahada ya udaktari wa falsafa (PhD). ili kufundisha somo la Hadiyth katika Chuo Kikuu, nailhali yuko mtu anayestahiki hilo kuliko sisi kwa namna ambayo hatufai sisi kuwa ni wanafunzi wake katika taaluma hii. Lakini huu ndio mfumo ulivyo na desturi.

 

NA KATIKA WALIOMSIFU BAADA YA KUFA KWAKE NI:

WAZIRI WA MASUALA YA KIISLAMU, AL-AWQAAF, ULINGANIO NA UONGOZI SHAYKH SWAALIH BIN ‘ABDUL-‘AZIYZ BIN MUHAMMAD AALU SHAYKH

Alisema: "Shukrani ni za Allaah kwa hukumu Zake na uwezo Wake ((Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea)). [28] Hakuna shaka kwamba kumpoteza Mwanachuoni Mkubwa Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni msiba. Kwani yeye ni katika wanachuoni wakubwa wa Ummah na mabingwa wa Hadiyth. Kwa Maulamaa hao (Shaykh Al-Albaaniy), Allaah Mtukufu Ameilinda Dini hii na Akaieneza Sunnah kupitia kwao…."

 

KATIBU MKUU WA SHIRIKISHO LA ULIMWENGU WA KIISLAMU HUKO MAKKAH AL-MUKARRAMAH SHAYKH DKT. ‘ABDULLAH BIN SWAALIH AL-‘UBAYD

Hakuna shaka yoyote kwamba kufariki Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni hasara kubwa kwa Ummah wa Kiislam. Vielelezo vya ushahidi na michango yake ni mingi na mikubwa kupitia elimu yake katika taasisi kubwa za Kiislam kama vile Chuo Kikuu cha Kiislam Madiynah na taasisi nyinginezo kubwa za Kiislam. Shaykh Naaswir (Allaah Amrehemu), alikuwa ni mtu wa kuthaminiwa na kuheshimiwa na kila Muislam, mashirika, makundi na mataifa. Hilo lilivikwa koja kwa kupewa Tuzo la Mfalme Fayswal kwa mchango wake mkubwa kuhusiana na tafiti zinazohusiana na Hadiyth.

 

TUME YA KUDUMU YA TAFITI ZA KITAALUMA NA UTOAJI FATWA SAUDI ARABIA

SWALI: Siku hizi watu wanazungumza sana juu ya mmoja kati ya Maulamaa wenye kufanya kazi ya kuinusuru Dini hii. Si mwingine bali ni Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Wanamtuhumu kwamba yeye ni mtu asiye na elimu, na ameibuka tu ili kuzusha mkorogano baina ya watu. Kuna mtu aliyesema: "Hakika mimi nimeanza kumchukia kwa ajili ya Allaah". Basi je, kazi hii anayoifanya Shaykh huyu Mtukufu si kazi inayoufaa Uislam na Waislam?! Nizingatiwe kuwa mimi sina kasumba naye, kwani kumheshimu yeye hakumaanishi kwamba mimi nina kasumba kwa mtu yeyote kijingajinga tu. Tutawaambia nini watu wasemao: "Watu wanakufa huko Syria na Afghanistan na yeye bado anahangaika na Hadiyth sahihi na dhaifu. Mnatuambia nini kuhusu Ustaadh huyu?

 

JIBU: Mtu huyu anajulikana kwetu kwa elimu yake, mchango wake, kuitukuza kwake Sunnah na kuitumikia. Pia anajulikana kwa kuunga kwake mkono madhehebu ya Ahlus-Sunnah wal Jama’ah katika kutahadharisha ukasumba, na ufuataji bila dalili, na vitabu vyake vyenye faida. Lakini yeye kama walivyo Maulamaa wengineo, si mtu aliyetakaswa na makosa. Yeye anakosea na kupatia. Tunamtarajia alipwe thawabu mbili katika alilolipatia, na thawabu moja ya kujitahidi akikosea kama ilivyothibiti toka kwa Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuhukumu anapohukumu akajitahidi na akapatia, basi ana thawabu mbili, na anapohukumu akajitahidi na akakosea, basi ana thawabu moja)). Tunamuomba Allaah Atupe sisi tawfiyq, nyinyi na yeye, tuweze kusimama imara mbele ya haki na kuepukana na vipotoshi vya fitna. Kwa Allaah ndio tawfiyq. Na Rehma ziwe juu ya Nabii wetu Muhammad, Ahli zake na Maswahaba wake. [29]

 

TENZI KUMHUSU SHAYKH AL-ALBAANIY

 

Hakika anayeinusuru Sheria ya Mola wetu,

hunusuriwa kama ulivyosema wahyi.

 

Na hakika tumemwona mhakiki wa enzi yetu,

naye ni mwanachuoni wa Hadiyth Naaswir Al-Albaaniy.

 

Ni yule ambaye wewe umekamia kumpinga,

ewe dhalimu, achana na uasi.

 

Watu waliokasumbika na kushabikia madhehebu,

na kwa Manhaj na ‘Aqiydah ya kikuhani…

 

Watu waliokasumbika na kushabikia madhehebu,

na kwa kazi yenye mabaki yasiyosalia…

 

Wote hao wametangaza hasira zao,

kwa kutukana na kuchafulia watu heshima katika ardhi.

 

Qiyaamah chao kimewaka moto na wote wamesimama,

lakini Shaykh Naaswir amesimama imara ngangari.

 

Ameeneza elimu bora kabisa katika enzi yetu,

ameeneza Sheria ya Ar-Rahmaan.

 

Hakulifanyia kasumba wala kulishabikia dhehebu lolote,

bali amewasifu na kuwapa haki zao Maimaam wote waliomtakasia Ar-Rahmaan.

 

Ingawa mahasidi na wenye chuki wamesema mbovu,

lakini hata hivyo, Allaah Amewanufaisha watu kwa elimu yake.

 

Wamesema yeye ni mshairi, mimi nikasema nampenda,

na hususan kwa Naaswir Al-Albaaniy.

 

Ni bendera ya wakati wetu, basi siwezi kuishusha na kuidharau haki yake,

ni Shaykh wa Mashaykh, mwenye akili ya kifani.

 

Yeye ndiye mkarabati wa zama,

na hakika imekuja, habari sahihi inayoishilia kwa aliye karibu.

 

Nyakati zote yeye ni mwalimu,

anayelingania Sheria ya Mola wetu Ar-Rahmaan.

 

Yeye ndiye Imaam kama Maimaam watahesabiwa,

sina shaka kabisa, na naapa kwa Yule Aliyeniumba.

 

Naye ndiye amekuwa ni wa kipekee katika wakati wake,

kwa Fiqh, Hadiyth na Qur-aan.

 

Ameitetea na kuipigania sana Sunnah ya Nabii Muhammad,

mteuliwa na mchaguliwa.

 

Ni Bid’ah ngapi alizozipiga vita,

bid’ah zilizoupakaza uso wa dini yetu kwa adha na fitina.

 

Analingania Tawhiyd na Uchaji Allaah,

ameshasema mara nyingi sana mfuateni Nabii wetu Adnaan.

 

Kwani hiyo ni faradhi, wajibu na lazima,

hatuwezi kuongoka tukimfuata mwingine ikiwa amali zitafaa katika mizani.

 

 

TANBIHI KUTOKA KWA MWANDISHI WA HISTORIA HII

 

Pamoja na kuwa Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) alikuwa ni mwanachuoni wa aina yake, na hoja katika Ummah katika elimu ya Hadiyth, ila ni muhimu tusisahau kuwa alikuwa ni mwanaadam na hupata na kukosea. Hatupaswi kufanya kama wanavyofanya baadhi ya vijana wenye hamasa, kumtukuza kupita kiasi na kuchukua kila linalotoka kwake na kuona kuwa haliwezi kuwa na makosa. Na isitoshe huwakosoa hadi kugombana na wale wasiokubaliana na baadhi ya fatwa za Shaykh. Imefikia hadi baadhi ya wanafunzi na vijana kuwaponda wanachuoni wengine kwa sababu tu wana rai inayotofautiana na Shaykh (Allaah Amrehemu). Huo si msimamo wa haki, na pia si msimamo wa Shaykh mwenyewe. Shaykh (Allaah Amrehemu) alikuwa akipokea haki na dalili japo ziko dhidi yake maadam ni sahihi kuliko zake.

 

Hatutoweza kumsahau kwa wepesi Shaykh wetu huyu mtukufu, kwa elimu yake inayowanufaisha mamilioni leo hii na itakayowanufaisha vizazi kwa vizazi hadi siku ya mwisho. Allaah Amrehemu na Amwandalie nyumba bora huko katika pepo Yake ya Firdaws. Aamiyn

 

 


[1] Ni fani ya Hadiyth inayohusiana na uaminifu wa wasimulizi wa Hadiyth na inakusanya habari zao zinazothibitisha uaminifu au udhaifu wa hao wasimulizi.

 

[2] Sayansi ya Hadiyth

 

[3] Hayaatul Al-Albaaniy, Muhammad Ash-Shaybaaniy. Al-Albaaniy mwenyewe anayeeleza hayo pia kwenye vitabu vyake ‘Mukhtaswar Al-‘Uluww’ na ‘Tahdhiyrus-Saajid’.

 

[4] Kitabu hichi tumekwishakitafsiri kwa Kiswahili na kiko katika kuchapishwa.

 

[5] Kimeshachapwa kwa lugha ya Kiswahili na kinapatikana madukani na pia kipo ndani ya ALHIDAAYA.

 

[6] Daf-u Shubuhaat At-Tashbiyh, uk.237

 

[7] Mawaidha na maswali na majbu ya Silsilatul Hudaa wan Nuur

 

[8] Bid’atut-Ta’aswub Al-Madh-habiy, Shaykh ‘Iyd Al-‘Abbaasiy. Na pia nakala ya mjadala huo unapatikana kwenye mtandao.

 

[9] Tamaamul Minnah Fiy Takhriyj Ahaadiyth Fiqhi As-Sunnah, Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal Haraam.

 

[10] Ibnul-'Aabidiyn katika al-Haashiyah 1/63, na katika inshaa yake Rasm al-Mufti 1/4 kutoka Mkusanyiko wa Insha za Ibnul-'Aabidyin. Shaykh Swaalih Al-Fulaaniy katika al-Iyqaadhw al-Himaam, uk.62. Na hii imeelezewa na Imaam Ibn 'Abdul-Barr kutoka Abu Haniyfah na kutoka kwa maimaam wengine".

 

[11] Ibn 'Abdul Barr katika Jaami'ul Bayaan Al-'Ilm, 2/32, ibn Hazm akinukuu kutoka kwake katika Usuul-Al-Ahkaam 6/149, na hali kadhaalika Al-Fulaaniy, uk.72.

 

[12] Harawiy katika Dhamm Al-Kalaam 3/47/1, Al-Khatwiyb katika Al-Ihtijaaj bi Ash-Shaafi'iy 8/2, Ibn 'Asaakir 15/9/10, An-Nawawiy katika Al-Majmuu' 1/63, Ibn al-Qayyim 2/361, na Al-Fulaaniy, uk.100, usimulizi wa pili ni kutoka Hilyah Al-Awliyaa ya Abu Nu'aym.

 

[13] An-Nawawiy katika Al-Majmuu' 1/63, Ash-Sha'raaniy 1/57, akitoa chanzo chake kama Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na Al-Fulaaniy, uk.107.

 

[14] Al-Fulaaniy, uk.113, na Ibn Al-Qayyim katika I'laam Al-Muwaqi’iyn.

 

[15] Samiyr bin Amiyn Az-Zuhayriy, Muhadith Al-‘Aswr, uk.39.

 

[16] Samiyr bin Amiyn Az-Zuhayriy, Muhadith Al-‘Aswr, uk.30.

 

[17] Shaykh Husayn Al-‘Awaaishah, Swafahaat Baydhwaa Min Hayaati Shaykhina Al-Albaaniy, uk.38

 

[18] Samiyr bin Amiyn Az-Zuhayriy, Muhadith Al-‘Aswr, uk.39.

 

[19] Shaykh Husayn Al-‘Awaaishah, Swafahaat Baydhwaa Min Hayaati Shaykhina Al-Albaaniy, uk.40.

 

[20] Samiyr bin Amiyn Az-Zuhayriy, Muhadith Al-‘Aswr, uk.78.

 

[21] Indama Bakaa Al-Albaaniy (RahimahuLlaah) عندما بكى الألباني ..! [رحمه الله]

 

[22] Munaadhwarah Ma’a Rajul-id-Da’aa An-Nubuwah  مناظرة مع رجل ادعى النبوة

[23] Abu Hudhayfah: 20 Points Regarding Shaykh al-Albaanee

[24] Abu Hudhayfah: 20 Points Regarding Shaykh al-Albaanee

 

[25] Swahiyh Muslim, Mjalada 2, Uk.632 (Mulhaq Al-Aswaalah Fiy Wafaat Mujaddid Al-Qarn Wa Muhadith Al-‘Aswr, 25 Jumaadah Al-Aakhirah 1420, Uk.3.

 

[26] Imepokewa na Abu Daawuud, na imeelezewa kuwa ni sahihi na Al-‘Iraaqiy na wengineo

 

[27] Imepokewa na Abu Daawuud, na imeelezewa kuwa ni sahihi na Al-‘Iraaqiy na wengineo.

 

[28] Al-Baqarah: 156

 

[29] Al-Lajnatud Daaimah Lil-Buhuuth Al-‘Ilmiyah wal-Iftaa, Fatwa Namba 12/244.

 

 
 

 

MAWAIDHA NA MITANDAO YA SHAYKH AL-ALBAANIY (ALLAAH AMREHEMU)

 

Mawaidha Na Fataawa Za Shaykh

http://www.alalbany.net/albany_tapes.php

 

Mtandao Kwa Lugha Ya Kiarabu

http://www.alalbany.net/

 

Mitandao Kwa Lugha Ya Kiingereza

http://www.albani.co.uk

http://www.twtpubs.com/web/  

http://www.shaikhalbaani.wordpress.com 

 

http://www.alalbany.net/albany_eng.php

 

 

 

 

Share