10-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Baadhi Ya Sifa Alizopewa Na Mtume Wa Allaah ( سبحانه و تعالى)

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) sifa nyingi sana, na zifuatazo ni baadhi chache sana ya sifa hizo;

 

Hakusita Wala Hakurudi Nyuma

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;

"Mikono yote iliyotunyoshea tushailipa, isipokuwa wa Abu Bakr, msaada alioutowa ni Allaah tu ndiye Atakayemlipa".

"Wote niliowaita katika Uislamu walisita kwanza isipokuwa Abu Bakr, yeye hakusita wala kurudi nyuma, hapo hapo alisilimu."

[Al-Haakim].

 

Usiponikuta, Mwendee Abu Bakr

Mwanamke mmoja alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na shida fulani, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa na shughuli nyingi sana wakati ule akamwambia;

"Nenda urudi siku nyingine".

Yule bibi akamuuliza;

"Nisipokukuta je?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

"Mwendee Abu Bakr'.

[Al-Bukhaariy]

 

Milango Yote Iliyoelekea Msikitini Ifungwe Isipokuwa Wa Abu Bakr

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya Mimbari na baada ya kumshukuru Allaah na kumpwekesha akasema;

"Allaah Alimshauri mja wake achaguwe iwapo anaitaka dunia au anataka yaliyo kwa Mola wake (anataka kwenda kwa Mola wake), na mja huyo akachagua yaliyo kwa Mola wake."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposikia maneno hayo akalia sana huku akisema;

"Kwa baba yangu na mama yangu nakufidia ewe Mtume wa Allaah".

Maswahaba waliohudhuria walishangazwa na kilio chake hicho wakawa wanasema;

'Vipi mtu huyu! Kipi kinachomliza wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuhadithia juu ya mja aliyeshauriwa achague baina ya dunia na baina yaliyo kwa Mola wake na akachagua yaliyo kwa Mola wake?'

Hawakuwa wakijua kuwa aliyeshauriwa ni Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwamba alitakiwa achague baina ya kwenda kwa Mola wake au abaki nao duniani, na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amechagua kwenda kwa Mola wake.

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema;

"Katika watu walonisaidia sana kwa hali na mali ni Abu Bakr, ingelikuwa naweza kumchagua Khalil (Rafiki), basi angekuwa Abu Bakr, lakini ni undugu katika Uislamu na kupendana. Milango yote iliyoelekea msikitini ifungwe isipokuwa wa Abu Bakr".

[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hizi Ni Sifa Za Watu Wa Peponi

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza;

"Yupi kati yenu asubuhi ya leo amefunga?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi".

Kisha akauliza tena;

"Yupi katika yenu aliyehudhuria mazishi siku ya leo?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza tena;

"Yupi kati yenu aliyemlisha masikini siku ya leo?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi."

Akauliza tena;

"Yupi katika yenu aliyemtembelea mgonjwa?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi."

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

"Hayajumuiki yote haya kwa mtu, isipokuwa ataingia Peponi."

[Muslim]

 

Wewe Ni Swahibu Wangu Penye Hodhi Na Peponi

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Umar kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Wewe ni Swahibu yangu penye Hodhi na sahibu yangu wa Pangoni."

[At-Tirmidhiy]

 

Nani Aliye Bora Baada Ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Siku moja Muhammad bin Hanafiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni Mtoto wa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimuuliza babake;

"Nani aliye bora baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ?"

'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu ;   Abu Bakr

Akauliza tena ;  Kisha nani

Akajibu ;           Kisha 'Umar

A[l-Bukhaariy]

 

Leo Mnataka Kumuacha Mkono Swahibu Yangu?

Siku moja Abu Bakr na 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhumaa) walijadiliana wakakhitalifiana, na Abu Bakr alimkasirisha 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhumaa) kwa kumwambia maneno yasiyomridhisha. Abu Bakr alimtaka msamaha 'Umar, lakini 'Umar alikataa Kumsamehe, kisha Abu Bakr akenda kumsikitikia Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Allaah keshakusamehe ewe Abu Bakr".

Wakati huo huo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyejuta kwa kutomsamehe Swahibu yake, alikuwa akimtafuta ili amtake yeye msamaha na akatokea wakati Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) amekaa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa amekasirika alipiga magoti mara baada ya kumuona 'Umar, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hali ile akamwambia;

"Mimi ndiye niliyemkosea ee Mtume wa Allaah."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kumwambia 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Allaah Alinituma kwenu nyote, na nyote mlinikadhibisha hapo mwanzo isipokuwa Abu Bakr. Yeye alisema "Swadaqta", basi leo mnataka kumwacha mkono Swahibu yangu?"

Anasema 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Tokea siku ile hapana mtu aliyethubutu kumkasirikia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)".

[Al-Bukhaariy]

 

Tulia Ewe Uhud

Siku moja Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya Jabali Uhud na jabali likatingishika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauweka mkono wake mtukufu juu ya jabali hilo huku akiliambia;

"Tulia ewe Uhud! Kwa hakika juu yako yupo Mtume, na Aliyesadiki (Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu)), na mashahidi wawili ('Umar na 'Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhumaa))".

[Al-Bukhaariy]

('Umar na 'Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum), wote walikufa  mashahidi).

 

Na Amchaye Allaah

Allaah Anasema;     

“Na Amchaye (Allaah) ataepushwa nao (Moto).

Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa.

Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe anamlipa.

Isipokuwa (anafanya haya) kwa kutaka Radhi ya Mola wake Mtukufu.

Basi atapata la kumridhisha.”

[Al-Layl: 16 – 21]

Maulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa katika aya hizi Allaah anamsifia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu sifa zote zilizotajwa zinakwenda sambamba na mwenendo na tabia zake;

Allaah Anasema;

Na Amchaye (Allaah) ataepushwa nao (Moto).”

Hapana shaka kuwa Maswahaba wote ni wachaji Allaah, lakini ukiendelea kuzisoma na kuzichunguza vizuri zaidi aya zilizofuatilia utaona kuwa Allaah Ameongeza sifa nyingine inayomuelezea zaidi Swahaba huyu mtukufu (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Allaah Anasema;

“Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa.

Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe anamlipa.”

Wasfu huu unakubaliana na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kupita mwengine yeyote kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akitoa mali yake yote kwa ajili ya kuwalisha na kuwavisha masikini pamoja na kuwakomboa Waislam waliokuwa watumwa na kuwaachia huru, yote haya kwa kutaka Radhi za Allaah. Na kisa cha kumkomboa Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni maarufu sana.

 

Sitoshindana Naye Tena

'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema;

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamrisha tutoe Swadaqah, na siku hiyo nilikuwa na Mali (pesa nyingi), Nikasema leo nitamshinda Abu Bakr, nikampelekea Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nusu ya Mali niliyokuwa nayo.

Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza:

“Ahli yako umewabakishia nini?”.

Nikamjibu;

“Nimewabakishia kima kama hiki cha mali (yaani nusu yake)”.

Akaja Abu Bakr na mali yote aliyokuwa nayo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza;

“Umewabakishia nini ahli yako ewe Abu Bakr”.

Abu Bakr akasema;

“Nimewabakishia Allaah na Mtume wake”.

Nikajisemea moyoni mwangu;

“Sitoshindana naye tena”.

[Abu Daawuwd na Ibni Maajah]

 

Oh! Mtamuua Mtu Kwa Sababu Anasema Mola Wake Ni Allaah?

Katika kuifasiri kauli ya Allaah isemayo;

“Na akasema mtu mmoja Mwislamu aliyekuwa mmoja wa watu wa Fir‘auni afichaye Uislamu wake; Oh! Mtamwua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah? Na kwa yakini yeye amekujieni kwa dalili wazi wazi zitokazo kwa Mola wenu!”

[Al-Muumin (Ghaafir): 28]

 

Katika kuifasiri aya hii anasema Imaam Al-Qurtwubiy;

Imepokelewa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim kuwa, Urwa bin Az-Zubayr, amesema;

“Nilimuuliza 'Abdullaah bin 'Amr bin Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu); Hebu nihadithie juu ya kubwa kabisa lililomkuta Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Mushrikina, akasema;

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa nje ya Al-Ka'abah, akamtokelea 'Uqbah hbin Abi Mu'ayitw na kumshika mabega yake, kisha akamzungushia nguo shingoni pake na kumbana kwa nguvu kabisa, akatokea Abu Bakr na kumshika mabega yake ('Uqbah) na kumsukumilia mbali na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akasema;

“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah?”

Hivi ndivyo alivyosimulia Al-Bukhaariy

Ama Hadiyth iliyopokelewa kutoka kwa At-Tirmidhiy inasema;

“Kutoka kwa Ja'afar bin Muhammad, kutoka kwa babake, kuwa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Baada ya kufa kwa Abi Twaalib, ma-Quraysh walikusanyika na kutaka kumuuw Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakamvamia, huyu akimburura na huyu akimsukuma, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anaomba  msaada, hapana aliyethubutu kusogea isipokuwa Abu Bakr, aliwaendea akamvuta huyu na kumsukuma yule huku akipiga kelele na kusema;

“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allah? Wa-Allaahi huyu ni Mtume Wake”.

(Ataqtuluuna rajulan an yaquula Rabbiya LLaah? Wa-Allaahi innahu larasuuluhu)

Imepokelewa kutoka kwa Al Bazaar katika Musnad yake kuwa Muhammad Bin 'Aqiyl (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akikhutubu akasema;

“Enyi watu! Nani shujaa kupita wote?”

Wakasema;

“Wewe ewe Amiri wa Waislam”

'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

“Ama mimi kila niliyepambana naye nimemshinda, lakini (shujaa kupita wote) ni Abu Bakr. Siku moja tulimjengea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hema kisha tukaulizana; ‘Nani atakayebaki na kumlinda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili asije akatokea mmoja katika Mushrikina na kumshambulia, basi Wa-Allaahi hapana aliyeingia isipokuwa Abu Bakr akiunyanyua upanga wake juu ya kichwa cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kila kafiri aliyejaribu kumsogelea Abu Bakr alikuwa akimrukia (na kumkabili, huyu ni shujaa kupita wote.

Na siku hiyo nilimuona pale alipochukuliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ma-Quraysh, huyu akimvuta na huyu akimsukuma, hapana aliyesogea siku hiyo isipokuwa Abu Bakr, alisogea akiwapiga na kuwasukuma, huku akisema;

“Ole wenu  Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah? Wa-Allaahi huyu ni Mtume Wake”.

(Waylukum! Ataqtuluna Rajulan an yaquula Rabbiya LLaah?) Wa-Allaahi innahu larasuuluhu))”

Kisha 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akalinyanyua guo alilokuwa amejifunika nalo na kuanza kulia mpaka ndevu zake zikaroa machozi.

 

 

Share