20-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Hali Chakula Cha Haramu

Alikuwa akihiyari kufunga mawe tumboni pake, yamsaidie asihisi njaa kuliko kuingiza tumboni mwake chakula cha haramu.

Katika Swahihul Bukhaariy imeelezwa kuwa;

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)alikuwa na mfanyakazi, kijana mdogo, na siku moja kijana huyo alikuja na chakula na kumkaribisha Khalifa wa Waislamu (Radhiya Allaahu ‘anhu)aliyekipokea na kula.

Yule kijana akamuuliza Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)

'Unajuwa kitu gani ulichokula ewe Khalifa wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza;

'Kitu gani?"

Yule kijana akajibu;

"Hapo zamani, zama za ujahilia (kabla ya kuwa Muislamu), niliwahi kumtabiria mtu, na mimi sijui chochote kuhusu utabiri wakati huo, nilimdanganya tu, na tokea siku ile sijaonana na mtu huyo isipokuwa leo, akanipa zawadi yangu (malipo yangu), na 'zawadi yenyewe ni hicho ulichokula."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)akaingiza mkono wake kinywani na kuanza kujitapisha kwa nguvu, na yule kijana akamwambia;

'Allaah Akurehemu! Yote haya (unafanya) kwa sababu ya tonge moja tu?'

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)a kamwambia;

'Wa-Allaahi kama haiwezekani kukitoa mpaka niitoe roho yangu basi nitafanya hivyo, maana nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema; "Sehemu yoyote ya mwili iliyojengeka kwa mali ya haramu basi Motoni ndipo panapostahiki kuingizwa mwili huo, na mimi naogopa isiongezeke sehemu yoyote ya mwili wangu kwa tonge hili".

 

Wakati majeshi ya Waislamu yalipokuwa yakisonga mbele kuyashinda majeshi ya Kirumi na kuteka nchi baada ya nchi, huku mali nyingi za ngawira zikiletwa Madiynah, Abu Bakr hakuyumbishwa wala kubabaishwa na yote hayo, bali aliendelea kuhukumu kwa uadilifu na kuishi maisha yale yale na kuvaa nguo zile zile na kula chakula kile kile alichokuwa akila kabla ya kuwa Khalifa.

Alipofariki dunia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwacha vitu vifuatavyo;

Ngamia aliyekuwa akimbebea maji, chombo cha kukamulia maziwa ya mnyama, na jokho alokuwa akilivaa anapopokea wajumbe kutoka nje, na alipoviona vitu hivyo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alilia sana kisha akasema:

"Wa-Allaahi umekwisha wapa taabu kubwa watakaokuja kuhukumu baada yako."

Alikuwa akisema;

Siku ile alipobashiriwa Pepo na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr (RadhiyaAllaahu ‘anhu) alisema;

"Wallahi siamini kuwa nitaepukana na adhabu ya Allaah, hata kama mguu wangu mmoja utakuwa ushaingia Peponi, huenda nikawa nimemkosea huyu au yule, kisha uje kutolewa mguu wangu Peponi na kuingizwa Motoni."

Rabi'ah Al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema;

"Siku moja nilikuwa nikijadiliana na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), akaniambia neno lililonichukiza, kisha akajuta na kuniambia;

'Ewe Rabi'ah nirudishie kama nilivyokwambia, upate kulipa kisasi chako'

'Nikamwambia;

Sitofanya hivyo'

Akenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na mimi nikamfuata, hata watu wakashangaa wakasema;

'Vipi huyu mtu, yeye anakukosea kisha anakwenda kukushitaki?"

Nikawambia, 'Huyu ni Abu Bakr …'

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza;

'Ewe Rabi'a,h kuna nini baina yako na Abu Bakr?'

Nikamwambia;

'Ee Mtume wa Allaah, yeye aliniambia neno lililonichukiza akataka nimrudishie ili nimlipize kisasi, nikakataa'.

Mtume akaniambia;

'Ahsante (umefanya vizuri) ewe Rabi'ah, usimrudishie, lakini sema;

'Mungu akusamehe ewe Abu Bakr'

Nikasema, ' Mungu akusamehe ewe Abu Bakr', Abu Bakr akaondoka huku analia".

Musnad Imam Ahmad

Khaalid Muhammad Khaalid katika kitabu cha 'Khulafaar Rasuul', anasema;

"Neno moja tu ulimi uliteleza akalitamka. Halikuwa neno ovu, kwa sababu Abu Bakr haiwezekani atamke neno ovu, lakini neno hilo lilimchukiza Rabia likamsituwa na kumhuzunisha Abu Bakr aliyeshikilia kuwa lazima alipizwe kisasi.

Na kwa nini asifanye hivyo wakati aliwahi kumuona Mtume wa Allaah akifanya hivyo hivyo siku ile alipokuwa akiwapanga majeshi ya Waislamu katika vita, na kwa bahati mbaya alimpiga mtu mmoja kwa nguvu tumboni  pake, na alipohisi kuwa pigo hilo limemuumiza mtu huyo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)a lipandisha nguo yake na kulifunua tumbo lake na kumtaka mtu yule amrudishie kama alivyompiga."

 

Share