43-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Wajibu Wa Mwanamke Kumhudumia Mumewe

 

Ninasema: baadhi ya Hadiyth zilizotajwa zinaonyesha dhahiri wajibu wa mwanamke kumtii na kumhudumia mumewe madamu anao uwezo, na hakuna shaka kwamba jambo la kwanza linaloingia humu ni huduma za nyumba na yote yanayohusika humo kama kulea watoto na kadhalika. Maulamaa wamekhitilafiana katika mas-ala haya, kwa mfano Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika 'Al-Fataawa' (2/234-235),

 
"Maulamaa wamekhitilafiana katika mas-ala haya kama inampasa kumhudumia kama kushughulika na fenicha za nyumba na kutayarisha chakula na vinywaji, kusaga unga na kupika chakula kwa ajili ya watumwa wake na kuwalisha farasi na kadhalika. Kuna wengine wanaosema, Huduma hii sio lazima. Kauli hii ni dhaifu, kama ilivyo udhaifu wa kauli za wale wanaosema kuwa mume haimpasi kumtendea wema au kujimai naye. Kwa vile hii haitokuwa ni kumfanyia wema, kama ni rafiki katika safari…Ikiwa hatomsaidia maana yake ni kuwa hajamtendea wema.

Na inasemekana: Na hii ndio sawa, kwamba kumhudumia ni wajibu kwa vile mumewe ameitwa ni bwana wake katika kitabu cha Allaah سبحانه وتعالى katika Sunnah ya Mjumbe wa Allaah  na mtumwa na mateka wanapaswa kuhudumiwa na kwa sababu hivyo ndivyo inavyojulikana sana.
Kisha kuna waliosema, Huduma nyepesi ya kawaida ni wajibu na wapo waliosema, ni wajibu kufanya wema na hili haswa ndio la sawa sawa.

 
Hivyo basi ni juu yake ahudumie katika mema ya kawaida ya mfano wake, hali hii inatofautiana na anuai za shughuli, kwa mfano mwanamke wa kibedui anatofautiana na mwanamke wa kijijini kwa anuai za shughuli na huduma anayotoa, kadhalika mwanamke mwenye nguvu atatofautiana na mwanamke dhaifu.

Nasema na hii ni Swahiyh Insha-Allaah, na ni usemi wa Maalik na Asbigh kama ilivyo katika 'Al-Fat-h' (9/418) na Abuu Bakar ibn Abu Shaybah na wengineo kama Al-Atwazijaariy wa Hanbali kama ilivyo katika 'Ikhtiyaaraat' (Ukurasa 145) na kundi la Maulamaa wa zamani na wa sasa kama ilivyo katika 'Az-Zaad' (4/46) na hatuoni dalili yoyote ya kufaa inayosema kuwa jambo hili halina uwajibu.

Na wengine wanasema: Kufunga ndoa kunahitaji starehe kufaidiana na sio kuhudumika rai hii imetupwa kwa sababu suala la starehe ni la wote.

 

Kama tunavyojua kuwa Allaah سبحانه وتعالى Amemuwajibisha zaidi mwanamume katika kumpatia mahitaji yake mke kama nguo, maskani na kumtimizia mahitajio yake. Kwa hiyo vile vile yeye mke pia anayo yaliyozidi kuwa wajibu kwake na hakuna zaidi ila ni kumhudumia. Khaswa kwa vile mume ndiye mwenye mamlaka ya mke, kwa hiyo ikiwa hatomhudumia, itabidi yeye mume amhudumie mke katika nyumba na hii itamfanya mke awe na mamlaka badala yake, jambo ambalo ni kinyume na Aayah ya Qur-aan kama ilivyo wazi. Kwa hiyo ni wajibu wa mke amhudumie mume.

 

Vile vile kuhudumu kwa mume kutaleta hali mbili zenye kugongana kwamba mume atazuilika kutafuta rizki na mahitajio mengine ambayo alipaswa kufanya na mwanamke atabakia nyumbani bila ya kufanya lolote.

Uharibifu/ufisadi huu upo dhahiri kabisa katika sheria ya Kiislamu, sheria ambayo imeweka usawa baina ya mume na mke katika haki mbali mbali, si hivyo tu bali pia umemfadhilisha mwanamume katika daraja na ndio maana Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakusikiliza malalamiko ya bintiye Faatwimah. Tunasoma malalamiko hayo katika Hadiyth ifuatayo,

 
“Faatwimah alikwenda kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kushitakia ugumu wa kazi za mikono nyumbani kwake, ingawaje hakumkuta babake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم lakini alimuachia maagizo Ummul Muuminina ‘Aaishah. ‘Aliy anahadithia kuwa (baada ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kupata salamu zile) Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikwenda kwao na wakati huo walikuwa wameshapanda kitandani yeye na mkewe kulala, ‘Aliy anasema, ‘Tulitaka kusimama (baada ya kumuona Mtume صلى الله عليه وآله وسلم) lakini akatukataza na kutuambia, “Hapo hapo mlipo” Akakaa katikati yetu pale kitandani kiasi nikahisi ule ubaridi wa miguu yake tumboni mwangu. Akutuambia, “Je, nikujulisheni jambo zuri zaidi kuliko lile mliloomba?” Mnapoingia kitandani semeni "Subhaana-Llaah' mara thelathini na tatu, 'Alhamduli-Llaah' mara thelathini na tatu na 'Allaahu Akbar' mara thelathini na nne, kwani hiyo ni bora kuliko kuwa na mtumishi”[1]

Kwa hiyo mnaona kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakumwambia 'Aliy, kuwa hana haja ya kukuhudumia bali inambidi (Faatwimah) amhudumie mumewe. Na yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakupendelea watu fulani katika kutoa sheria kama alivyotaja Ibn Al-Qayyim. Na anayetaka kujua zaidi kuhusu mas-ala haya basi asome kitabu chake cha thamani "Zaadul-Ma'aad' (4/45-46).

Majukumu ya mke kwa mumewe hayakatazi au kuzuia mume kumsaidia mke wake katika kazi zake. Hakuna kitu cha kudai mapendeleo ya usaidizi wa mume kwa mkewe ikiwa atapata wakati, bali hiyo ni mojawapo wa kutendeana wema baina ya mke na mume, na ndiyo mama wa waumini ‘Aaishah رضي الله عنها alisema: "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akihudumia familia yake na Swalah ilipowadia alikuwa anakwenda kuswali"[2]

 
Na imenukuliwa katika 'Ash-Shamaa'il' (2/185) kutoka isnaad nyingine kwa maneno: "Mwanamume alikuwa akishughulikia nguo zake mwenyewe, akikamua kondoo maziwa, na akijihudumia mwenyewe". Na usimulizi wake ni Swahiyh na nyinginezo kidogo ni dhaifu.  Lakini Ahmad na Abu Bakar Ash-Shaafi'y wamenukuu kwa isnaad iliyo na nguvu kama nilivyoonyesha katika 'Silsilatul-Ahaadiythis-Swahiyhah' (Namba 670) na kufuzu ni kutokana na tawfiki ya Allaah سبحانه وتعالى.

Huu ni mwisho wa yale Aliyoniwezesha Allaah سبحانه وتعالى kuandika kuhusu ‘Adabu za Ndoa na Sherehe za Harusi’ katika kitabu hiki.

 

 

 

سُبْحـانَكَ اللّهُـمَّ وَبِحَمدِك، أَشْهَـدُ أَنْ لا إِلهَ إِلاّ أَنْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتوبُ إِلَـيْك
 

 

Subhaanaka Allaahuumma Wa Bihamdika, Ash-Hadu An Laa Ilaaha Illa Anta, Astaghfiruka Wa Atuubu Ilayka.

 


[1] 'Aliy amesema: "Sikuiacha tena baada ya hapo". Ilisemwa:  Hata usiku wa Siffiyn? Akasema: "Hata   usiku wa Siffiyn" (imehadithiwa na Al-Bukhaariy 9/417-418)

 

[2] Imehadithiwa na Al-Bukhaariy (2/129 na 9/418), At-Tirmidhiy (3/314) ambaye amekiri ni Swahiyh, Al-Mukhlis katika 'Al-Mukhlisiyaat' (1/66) na Ibn Sa'ad (1/366)

 

Share