Swalah Ya Mgonjwa Anayeswali Kwa Kuketi Akiwa Kavaa Viatu Inafaa?

 

SWALI:

Assalam alaikum napenda kuuliza swali kuhusu jambo hili la swala, kuna mtu anaumwa na maradhi aliyonayo hawezi kusujudu sasa mimi nimkuta anasali amekaa juu ya kiti lakini pia nilimkuta wakati anasali alikua na viatu vyake je hii inafaa kusali mtu akiwa amevaa viatu?



 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani nyingi na za dhati kwako kuhusu suala la kuswali na viatu. Natumai kwa yale tunayokupatia yatakinaisha moyo wako kuhusu suala hilo.

 

Mwanzo inatakiwa ieleweke kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiswali katika Msikiti Mtukufu wa Madinah (wa Mtume) wakiwa wamevaa viatu. Suala la kutovaa viatu limekuja baadaye baada ya kuwa Misikiti yetu ulimwengu mzima kuanzia karne nyingi imekuwa ikitandikwa mazulia. Kwa ajili hiyo, desturi na ada zinahitajia kuwa tusiwe ni wenye kuvaa viatu. Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ulikuwa hauna zulia wala mkeka, nao ulikuwa ni mchanga mtupu. Dalili za kuvaa viatu katika Swalah ametufundisha mwenyewe Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kutoka kwa Abu Sa‘iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) anatuhadithia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivua viatu akiwa ndani ya Swalah na wakavua watu waliokuwa nyuma yake. Alipomaliza Swalah, aliwauliza, “Kwa nini mumevua viatu vyenu?” Walijibu: “Tumekuona wewe ukifanya hivyo”. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Jibriyl alikuja kwangu na kunieleza kuwa viatu vyangu vina najisi. Kwa hiyo, mmoja wenu akija Msikitini, avivue viatu vyake na kuviangalia. Ikiwa mmoja wenu ataviona vina najisi avisugue na mchanga kisha aswali navyo (Ahmad, Abu Daawuud, al-Haakim, Ibn Hibbaan na Ibn Khuzaymah, naye akasema ni sahihi).

 

Na si hivyo tu kuwa inafaa kuswali na viatu bali ikiwa umevaa viatu baada ya kuchukua wudhuu huna haja ya kuvivua, inatosha kwako kupangusa juu yake. Na hili pia ni muhimu kwa mgonjwa kujua ili asiwe ni mwenye kushika maji kila wakati wa Swalah. Hilo huenda likampunguzia madhara mengi zaidi. Ikiwa mgonjwa ni mkaazi wa hapo mahali anaweza kupangusa juu ya viatu au soksi kwa masaa 24 pekee, baada ya hapo inabidi avue kwa ajili ya kuyatia maji miguu lakini ikiwa maji yanamdhuru kwa ushauri wa daktari inatosha kwake kufanya tayamum. Hadiyth za kupangusa ni kama zifuatazo:

 

1.     Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), alikwenda kwenye jaa la taka la raia na kukojoa akiwa amesimama. Hudhayfah alikwenda zake, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuita (ili arudi). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alichukua wudhuu na kupangusa juu ya viatu vyake (“Jama‘ah” yaani imenukuliwa na Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).

 

2.     ‘Amr bin Umayyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akipangusa juu ya kilemba chake na viatu vyake” (Ahmad, al-Bukhaariy na Ibn Maajah).

 

Hivyo, hili ni suala ambalo halina utata wala shida katika Uislamu, mgonjwa huyo anaweza kuendelea na kuswali na viatu bila tatizo lolote. Na hasa kwa kuwa yuko nyumbani, viatu kuingia najisi ni jambo ambalo si rahisi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share