Akienda Kazini ndio talaka Yake – Mume Hamhudumii yeye wala watoto wake Afanyeje?

 

SWALI:

InshaAllaah mungu akulipeni kheri duniani na akhera kwa msaada wenu. Mimi nina rafiki yangu mume wake amimuabia akitoka kuenda kazini ndio talaka yake, na huyo mume wenyewe hamtizami kwa chochote si yeye wala watoto na pia kuna wazee wake wanamtegemea. Wamembiwa wazee waseme naye lakini msimamo wake uko pale pale. Je, afanye nini?



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa tumekuwa tukilizungumzia suala hili mara kadhaa. Hili ni tatizo ambalo limezagaa katika jamii yetu kwa kiasi kikubwa sana. Hili tatizo linarudi kwa wazazi na pia wanandoa ambao wameshindwa kufuata muongozo wa Kiislamu katika kuchagua mwenzi wa maisha.

Uislamu umetuekea sifa za kuchagua mwenza ambaye mtasaidiana kwa hali na mali, furaha na huzuni, shida na raha. Kukosa kufanya hivyo na kutoafikiana hapo mbeleni ndio kunatokea matatizo aina hii. Lau mke angekuwa ni mwenye kuweka masharti yanayokubaliwa katika ndoa mushkeli kama huu haungekuwa ni wenye kutokea na lau ungetoka basi ingekuwa rahisi kusuluhisha. Kwa hali zote tatizo tayari limetokea kwetu ni kutoa nasaha ili hali za wanandoa ziwe njema na nzuri.

Hilo ni tatizo la unyumba na mume ameacha majukumu aliyopewa na Allaah Aliyetukuka. Hivyo, ni vyema kutumia njia zilizopangwa na sheria ili kutatua tatizo hilo. Jambo la kwanza ambalo mke anafaa kufanya ni kujaribu kukaa kitako yeye na mumewe ili wazungumze ki-uanandoa na kutatua tatizo hilo dogo sana. Ikiwa haikuwezekana basi mke itabidi aitishe kikao ambacho kitajumlisha kuwepo yeye, mumewe, wawakilishi wa mume na mke ili wajadili suala hilo kwa kutaka suluhisho. Ikiwa kweli nia ni kutaka kutatua mushkeli basi Allaah Aliyetukuka Ataleta suluhisho la kudumu baina yao. Lau kila mmoja atavutia kwake basi tatizo hilo litabakia nao mpaka waache na kila mmoja apate mwingine mwenye kheri naye.

Ikiwa hilo halikuleta natija yoyote, basi itabidi uende mbele ukashitaki kwa Qaadhi kwa kumuelezea yote yanayojiri. Sijui kama hapo mnapoishi wapo ma-Qaadhi au vipi? Ikiwa hawapo basi unaweza kwenda kwa Shaykh anayetegemewa na muadilifu umweleze shida yake yote. Qaadhi au Shaykh huyo atamwita mumeo nawe pia utakuwepo ili apate kusikiliza pande zote mbili na baada ya hapo kutoa uamuzi muafaka. Suala la kutoa nafaka kwa mke ni suala ambalo Qaadhi anaweza kumuachisha mke kutoka kwa mume wake.

Twatumai kwa kufuata hayo yaliyo juu atapata ufumbuzi wa suala hilo na tatizo lake kusuluhishwa kwa njia nzuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share