Zingatio: Chenye Mwanzo Kina Mwisho Wake

 

Naaswir Haamid

 

 

Maelezo yaliyotolewa ndani ya Qur-aan, yamekubaliana bila ya pingamizi na uchunguzi walioufanya wanasayansi kwamba; Yeye ndie Muumba wa huu Ulimwengu ulioanza kwa chembe ndogo tu iitwayo atom miaka bilioni 15 iliyopita. Na bila ya shaka, huu Ulimwengu ni kiumbe cha Mola Mlezi kama tulivyo sisi wanaadamu. Hivyo, umepangiwa kanuni zake za kuishi na wakati wake maalum wa kufikia kikomo. Asili ya Ulimwengu imeelezwa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwamba:

 

{{Yeye ndiye Muumba wa mbingu wa ardhi}} [Suratul-An’aam: 101]

 

Vivyo hivyo, Siku ambayo haina khitilafu yoyote ya kufika ni khatima ya Ulimwengu. Kwani hata mambumbumbu wa elimu ya Mola waitwao wanasayansi, wamekwishabainisha kwamba Ulimwengu nao utafika mwisho.

 

Ajabu ni kuwa tunawaamini wanasayansi lakini tunayaweka nyuma maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ambaye ni Mjuzi na Mtambuzi wa kulla kitu. Tumegeuka mbwa kwa kuramba nyayo za bwana ili tutupiwe mfupa tuungongone, hali ya kuwa Mola wetu Amekwisha bainisha ndani ya Qur-aan kwamba Qiyaamah kipo na wala hakina khitilafu yoyote kutokea kwake.

 

Mapenzi yote baina ya viumbe yataondoka ghafla baada ya kuja sauti kali ya baragumu la Kiyama iumizayo masikio. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameichora taswira ya athari ya baragumu hilo:

 

{{Basi itakapokuja sauti kali iumizayo masikio (sauti ya baragumu la Kiyama). Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye. Na mamaye na babaye. Na mkewe na wanawe.}} [Suratu-‘Abasa: 33-36]

 

Hiyo ni Siku ambayo ardhi itatemeshewe barabara kuliko mfano wa tetemeko lolote tulilopata kulishuhudia kabla. Vilivyo chini ya ardhi vitatoka juu na vilivyo juu vitataka kuingia humo ardhini! Lakini khasara yetu, hatukai kuyafikiria yote haya, bali ni kupiga hisabu za mali na kupoteza muda passing time.

 

Qiyaamah kimebainishwa kwenye tafsiri baadhi ya tafsiyr kama ni msiba. Huu ni msiba mkubwa ugongao nyoyo ya kila mwanaadamu ambao unafaa kufikiriwa kila dakika. Na ni upi huo msiba ugongao nyoyo za wanaadamu? Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajibu:

 

{{Siku ambayo watu watakuwa kama madumadu (watoto wa nzige) waliotawanywa. Na milima itakuwa kama sufi zilizochambuliwa (zikawa zinapeperuka).}} [Al-Qaari’ah: 3-5]

 

Iangalie vyema taswira iliyochorwa ndani ya aya hizo juu, si dhihaka wala upuuzi! Kama binaadamu amefikia hali ya kuikata milima mithili ya vipande vya keki. Kwanini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ashindwe kuipeperusha kama sufi?

 

Hiyo ni siku ambayo jua litakunjwa kunjwa, na nyota zitakapopukutika, milima itakapoendeshwa mithili ya vumbi, bahari zitawashwa moto, kulla kiumbe chenye mimba kitaitoa mimba yake. Ni siku ambayo hata wachungaji wenye hamu ya kupokea vizazi vipya watawakimbia wanyama wao wenye mimba pevu. Na roho za viumbe wote kuanzia Nabii Aadam (‘Alayhi swalaatu was-salaam) hadi wa mwisho kuzaliwa zitaunganishwa na kiwiliwili chake [Rudia Suratut-Takwiyr: 1-8].

 

Mwisho wa yote, ni kuwa kuna mawili kati ya moja ndani ya Siku hiyo. Ama Pepo, Allaah Atujaalie tuwe miongoni mwao. Ama Moto, Allaah Atuepushe nao. Lakini, ‘ukioteshacho ndicho ukivunacho’ Tusitarajie kwamba tukawa tunaishi bila ya utaratibu tuliopangiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), tukategemea kupata hiyo Pepo.

 

Share