Kakojolea Maji Ambayo Hayajafika Kullatayn, Na Yakajaa Yakafika Kullatayn, Nini Hukmu Yake?

 

 

SWALI:

Swali langu ni hili... mtu amekwenda kukoga kwenye beseni (bath) ameamua kujaza maji ndani yake, beseni lenye ukubwa wa kullaten na tunavyoambiwa na masheikh wetu maji yakifikia kullaten huwa hayaingii najisi lakini swali langu huyu mtu kabla ya yale maji hayaja jaa kufikia kullaten yeye alikwisha ingia na kukojoa ndani ya yale maji halafu akayawacha yale maji yakajaa tele, je sheikh ile najisi ya mkojo iliondoka au anastahili kujitwaharisha upya kwa maji mengine... natumai utakuwa umenielewa..

Inshaallah na kupata jibu lenye kuridhisha.. ammina..


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola   wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ama kuhusu suala hili hebu tutazame Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema: Abu Sa'iyd al-Khudriy (Radhiya Allahu 'anhu) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"Je, twaweza kuchukua wudhuu katika kisima cha Buda'ah". Akajibu: "Maji ni twahara, hayanajisiki na chochote" (Ahmad, ash-Shaafi'iy, Abu Daawuud, an-Nasaa'iy na at-Tirmidhiy).

Kwa mujibu wa Hadiyth hii maji hayo katika beseni ni twahara ila ikiwa yamebadilika moja katika sifa zake kama rangi, harufu na tamu. Ikiwa sifa yake imebadilika basi maji kama hayo hayataweza kutumika tena kwa kutawadhia.

Hata hivyo, tungependa kuwanasihi ndugu na dada zetu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu kukojoa kwenye maji yasiyotembea ikiwa ni katika beseni, mto, ziwa, kisima, birika na kadhalika. Katazo hilo ni kuwaweka watu wawe mbali na kupatikana na magonjwa au kuudhiwa na harufu mbaya.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share