Kumuoa Mkristo Bila Ya Ridha Ya Wazazi Wake Inafaa Ikiwa Mke Mwenyewe Anataka Kusilimu?

 

SWALI:

 

Mimi nina swali kuhusu ndoa. Ikiwa kama nimepata msichana asiye kuwa muislam tukakubaliana kwa ridhaa yake kubadili dini kisha tuoane, lakini wazazi wake ambao ni manasara hawako radhi kwa kusilimu binti yao wala kuolewa na muislamu, ndoa hii itafungwaje na itaswihi  wakati hakuna ridhaa ya wazazi wala walii alopewa idhini na wazazi na hali mtoto wa kike yupo radhi kutengana na wazazi wake ili mradi asilimu na kuolewa na muislam?

Akhsante naomba hikma ya suala hili.

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu ndoa. Mambo ya ndoa si mambo ya mchezo kama tunavyofikiria. Kabla ya kuingia katika kiini cha suala lenyewe tungependa awali ya yote kukupa nasaha kuhusu suala hilo. Ni vyema baada ya kusilimu kwa msichana umpeleke sehemu afundishwe Dini ya Kiislamu mpaka imkolee kwani kuna visa vingi vya wasichana baada ya kuolewa kutoshika Dini hiyo ya Uislamu au kuritadi kabisa. Mara nyingine wanakimbia hata na watoto mliozaa pamoja.

Kwa hiyo, kumfundisha yanayotakiwa katika Uislamu ni muhimu kabla ya kufunga ndoa. Itatakiwa umpe fursa ya kama miezi mitatu au zaidi kwake kuweza kujifunza Uislamu. Ikiwa ataridhika kwa hilo nawe ukaweza kuvumilia mnaweza kwenda katika hatua inayofuata.

Tufahamu mzazi asiyekuwa Muislamu hawezi kuwa walii wa msichana aliyesilimu. Lakini kwa kuwa Uislamu ni Dini ya maumbile na imekuja kwa maslahi ya wanadamu inachunga sana kuweza kuwavutia wengine. Mbali na kuwa wazazi hawataki ndoa hiyo ifanyike ni wajibu wenu kwenda kwa wazazi wa atakayekuwa mkeo na kuwapasha habari ya hiyo ndoa. Hii ni kuwapatia heshima yao na pia ni njia mojawapo ya Da‘wah kwao. Huenda mioyo yao ikalainika mbali na kuwa walikuwa ni maadui kwenu na hawataki jambo hilo. Ikiwa wamebaki na ukali wao mtakwenda kwa Qaadhi kama sehemu hiyo yupo na ikiwa hayupo utakwenda kwa Imaam au Shaykh ili afunge nikaha (Nikaah).

Kwa kuwa msichana huyo hana walii basi Qaadhi, Imaam au Shaykh atasimama mahali pa mzazi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Qaadhi ni walii kwa asiyekuwa na walii”.

Nchi nyingine kama Tanzania na Kenya ili wenye kuozesha kujiepusha na balaa za wazazi ambao wanaweza kwenda mahakamani kushika kuhusu hilo humuhitajia msichana aandike affidavit ambayo atatia sahihi kuwa yu tayari kuolewa na kijana huyo wala hakutendeshwa nguvu katika hilo. Baada ya kufanya hivyo Qaadhi, Imaam au Shaykh atafungisha nikaha.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share