Bandari Wanayotumia Mahujaji Saudia Inaitwaje?

 

SWALI:

 

Bandari wanayotumia mahujaji wote Saudia inaitwaje?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo. Tufahamu kuwa siku hizi bandari huwa hazitumiwi sana kwani watu hasa wale wanaotoka mbali wanatumia ndege. Kwa hiyo, wao huwa wanafika kwenye uwanja wa ndege kabla ya kufunga safari yenyewe kuelekea Makkah. Viwanja vya ndege ambavyo vinatumika ni vile vya Jeddah, Madiynah n.k.

Hata hivyo, hadi wakati huu wetu wa sasa wapo wengine ambao wapo karibu na Saudia kama wananchi wa Misri, Jordan, Sudan, Ethiopia ambao wanatumia meli kuelekea Hijjah huwa wanatia nanga bandari ya Jeddah ambayo ndio bandari kubwa zaidi katika nchi ya Saudi Arabia. Hata hivyo, zipo bandari nyingine kama Dhiba, Yanbu, Dammaam, Jubayl na Jizan. Bandari za Jeddah, Dhiba, Jizan na Yanbu zipo katika Bahari Nyekundu ilhali Dammaam na Jubayl zipo katika Ghuba ya Uajemi.

Kwa ukaribu wa mji mtukufu wa Makkah ni bandari ya Jeddah ikifuatiwa na ile ya Yanbu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share