Zingatio: Vita Vya Panzi Furaha Ya Kunguru

 

Zingatio: Vita Vya Panzi, Furaha Ya Kunguru

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Jamii ya Waislamu Ulimwenguni ni iliyo kubwa na inajulikana kuwa ni yenye imani iliyo tofauti na dini nyengine. Imani ambayo katu hairuhusu riba, ulevi, vazi lisilo la hijaab kwa mwanamke, muziki, uzinifu na mengineyo. Mambo ambayo kwa dini nyengine ni ya kawaida na yanaruhusika wazi wazi.

 

Ni misimamo hii ambayo inasababisha kuwa na mvutano baina ya Uislamu na dini nyengine. Uislamu unazo kanuni zake kamili na lazima ziendane pamoja hata kama mazingira na khulka za watu zitabadilika kuwa sawa na majini. Uislamu hauna ustahamilivu mbele ya dhulma wala haukubali ubepari, ujamaa au mfumo mwengine wowote ambao utamdhalilisha mwanaadamu.

 

Bahati mbaya kwetu sisi Waislamu ni kwamba tumegawika na kupigana vijembe kila kukicha. Ingawa dhulma inaongezeka na kusababisha Waislamu kuwa na wakati mgumu kutimiza kanuni za Muumba wa Mbingu na Ardhi. Huyu yupo kabila lile na yule yupo chama kile. Wengine wanafarikiana kwa mechi za mpira tu! Subhaana Allaah. Tupo katika kuchunguzana na kutoana kasoro badala ya kukaa pamoja na kufikiria namna ya kuishinda dhulma iliyoenea.

 

Tunasahau kwamba wasiokuwa Waislamu wana tofauti zilizo nyingi mno, wamo humo Mabudha, Mahindu, Mayahudi, Manaswara na wengineo kadha wa kadha. Lakini pale Waislamu wanapopata fursa ya kuja juu kidogo, wote wanakusanyika kwa pamoja kurusha mishale ikiwa ni ya kuonekana au isiyoonekana. Hili silo linalofanyika kwa Waislamu pale ambapo kundi moja linapovamiwa na kunyanyaswa.

 

Na tunapokuwa na mgongano wa mawazo baina ya Waislamu, maadui zetu wanapiga kofi zilizo nyingi na kufanya kila hila uendelee ugomvi baina yetu. Wahenga walitufunza kwamba; panzi wakipigana, kunguru hupata ulaini wa kitoweo cha siku hiyo. Ndivyo hali yetu Waislamu wa kizazi cha sasa. Tunafarikiana huku maadui zetu wanapata mwanya mzuri wa kuendeleza dhulma.

 

Tuelewe ya kuwa Tawhiyd inatufunza na kututaka mioyo yetu kuwa kitu kimoja, ikimpwekesha Rabb Mmoja, na Kitabu kimoja na Nabiy wake mmoja na mila moja. Ni imani hii ambayo itatufanya kupendana mmoja kwa mwengine kama alivyotusifu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

Hakika Waumini ni ndugu…, [Al-Hujuraat: 10]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewapigia mfano wa Waumini katika kupendana kwao na kuoneana huruma kama kiwiliwili kimoja, kinaposhtaki kwa maumivu kiungo kimoja, hupelekea mwili wote kukesha na homa.

 

Jamii ya Waumini yatakiwa kuwa ni wamoja kwa kusaidiana kwenye mema, subra na kumcha Allaah. Wakatazane kuachana na maovu, uadui, wote kwa pamoja wafanye aamali njema ili wafuzu radhi za Rabb wao. Na pale ambapo Waislamu wanaposhikana katika tawhiyd, wanakua kama vile Alivyowasifu Rabb wao:

 

 كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ 

Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. [Al-Imraan: 110]

 

Aliyekuwa Qaadhi Mkuu wa Kenya, Shaykh AbduLlaah Swaalih Al-Farsy (Rahimahu Allaah) ametuusia kwamba tuzingatie ya kuwa Rabb wetu Anatutaka tushikamane wote pamoja kwa jina la Dini yetu ya Uislamu. Tusifarikiane kwa jina la miji au kabila au vyama au mengineyo kama ilivyo sasa. Kufanya hivi ni jukumu kubwa kabisa. Na tuache upesi au khatari itakuwa kubwa kabisa na dhambi kubwa kwani Allaah Amekwishatueleza: 

 

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ 

Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane. [Al-Imraan: 103]

 

 

 

Share