Amana Katika Uislam

Amana Katika Uislamu

 

www.alhidaaya.com

 

 

Baada ya kumhimidi na kumshukuru Allaah Aliyetukuka Ambaye Ametuneemesha na fursa hii ya kukutana ili kunasihiana na kukumbushana. Swalah na salamu zimfikiye hashimu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba zake, ahli zake na Waumini wote mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Maudhui yetu ya leo ni muhimu sana katika zama zetu za leo na matatizo mengi tunakumbana nayo kwa sababu ya kukosekana. Hiyo ni maudhui ya amana.

 

Huenda mmoja wetu akauliza: Amana ina maana gani katika Dini yetu ya kweli? Suala hilo limejibiwa na Imaam al-Qurtwubiy (Allaah Amrehemu) pale aliposema: Amana inajumlisha shughuli zote za Kidini. Amana ndio faradhi ambazo kwayo Allaah Aliyetukuka Amewapatia waja Wake.

Na wametofautiana katika tafsili, hivyo kukawa na kauli nyingi. Baadhi yake ni:

 

Pakasemwa: Hiyo ni kuweka amana ya mali na nyengineyo.

 

Na pakasemwa: Katika kila faradhi, na iliyo nzito ni amana ya mali.

 

Na pakasemwa: Ni katika amana, kwa alichoaminiwa mwanamke kwa utupu wake, asiitumie katika uzinifu.

 

Na wakasema wengineo: Kuoga josho la janaba ni katika amana.

 

Na pakasemwa: Amana ni Swalah, pia Swawm na kuoga josho la janaba.

 

Na pakasemwa: Hana Imani asiye muaminifu.

 

Na pakasemwa: Hii ni amana ambayo Allaah Aliyetukuka Aliipatia mbingu, ardhi, majabali na viumbe katika dalili za Uungu Wake.

 

Na ametaja Ibn al-Jawziy amenukuu kutoka kwa baadhi ya Wafasiri wa Qur-aan kuhusu amana katika Qur-aani Tukufu imegawanyika sehemu tatu:

 

 

Ya kwanza: Ni Faradhi, na miongoni mwayo ni kauli ya Aliyetukuka:

 

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَخُونُواْ اللّهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُواْ أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ﴾ (الأنفال 27).

 

Enyi walioamini! Msimfanyie khiyana Allaah na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua” (8: 27).

 

 

Ya pili: Kurudisha, na miongoni mwayo ni kauli ya Aliyetukuka:

 

﴿إِنَّ اللّهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤدُّواْ الأَمَانَاتِ إِلَى أَهْلِهَا﴾ (النساء 58).

 

Hakika Allaah Anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe” (4: 58).

 

 

 

Ya tatu: Ni utwahara na usafi, na miongoni ni kauli ya Aliyetukuka:

 

﴿إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ ﴾ (القصص 26).

 

Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu” (28: 26).

 

 

Ndugu zangu katika Imani, jueni kuwa amana ni sifa miongoni mwa sifa za Manabii na Waumini wema kama Alivyotuambia Allaah Aliyetukuka katika Kitabu Chake.

 

Amesema Aliyetukuka kuhusu Nuwh (‘Alayhis Salaam):

 

﴿كَذَّبَتْ قَوْمُ نُوحٍ الْمُرْسَلِينَ. إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ نُوحٌ أَلَا تَتَّقُونَ. إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ. فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ﴾  (الشعراء 105 – 108).

 

Kaumu ya Nuwh waliwakadhibisha Mitume. Alipowaambia ndugu yao, Nuwh: Je, Hamuwi wachaji? Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. Basi Mcheni Allaah, na nitiini mimi” (26: 105 – 108).

 

Na kuhusu Nabii Huwd (‘Alayhis Salaam) Anatuambia Aliyetukuka:

 

﴿كَذَّبَتْ عَادٌ الْمُرْسَلِينَ. إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ هُودٌ أَلَا تَتَّقُونَ.  إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ. فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ﴾  (الشعراء 123 – 126).

 

Kaumu ya Huwd waliwakadhibisha Mitume. Alipowaambia ndugu yao, Huwd: Je, Hamuwi wachaji? Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. Basi Mcheni Allaah, na nitiini mimi” (26: 123 – 126).

 

Na kuhusu Muwsaa (‘Alayhis Salaam), Anasema Aliyetukuka:

 

﴿قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ﴾ (القصص 26).

 

Akasema mmoja katika wale wanawake: Ee baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu” (28: 26).

 

Na kuhusu Yuwsuf (‘Alayhis Salaam), Anasema Aliyetukuka:

 

﴿وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ أَسْتَخْلِصْهُ لِنَفْسِي فَلَمَّا كَلَّمَهُ قَالَ إِنَّكَ الْيَوْمَ لَدَيْنَا مِكِينٌ أَمِينٌ (يوسف 54).

 

“Na mfalme akasema: “Nileteeni (Yuwsuf) nimteue mahsusi kwangu.” Basi aliposema naye, akasema: “Hakika wewe leo kwetu umetamakani kwa cheo na umekuwa muaminiwa.” (12: 54).

 

Ama Waumini watendao mema, Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

﴿وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ (المؤمنون 8).

 

Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao” (23: 8).

 

 

Allaah Aliyetukuka Ametuamuru kuwa waaminifu na kutekeleza amana kama Alivyotuambia:

 

 ﴿وَإِن كُنتُمْ عَلَى سَفَرٍ وَلَمْ تَجِدُواْ كَاتِبًا فَرِهَانٌ مَّقْبُوضَةٌ فَإِنْ أَمِنَ بَعْضُكُم بَعْضًا فَلْيُؤَدِّ الَّذِي اؤْتُمِنَ أَمَانَتَهُ وَلْيَتَّقِ اللّهَ رَبَّهُ وَلاَ تَكْتُمُواْ الشَّهَادَةَ وَمَن يَكْتُمْهَا فَإِنَّهُ آثِمٌ قَلْبُهُ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ (البقرة 283).

 

“Na mkiwa safarini na hamkumpata mwandishi, basi (mdai) akabidhiwe rahani. Na ikiwa mmoja wenu amewekewa amana na mwengine, basi airudishe yule ambaye ameaminiwa amana ya mwenzake; na amche Allaah, Rabb wake; na wala msifiche ushahidi; na mwenye kuuficha basi hakika moyo wake ni wenye kutenda dhambi. Na Allaah kwa mnayoyatenda ni Mjuzi.” (2: 283).

 

Hapa tunapata kuwa hata katika safari ambapo hakuna shahidi, Muislamu anatakiwa awe muaminifu na asimkhini yeyote kwa chochote kile. Na shahidi naye ikiwa atakuwepo anafaa asifiche ushahidi kwani kuficha ni utovu wa amana. Na Muislamu anafaa afahamu kuwa yote anayofanya yanafahamika kwa Allaah Aliyetukuka, hivyo kufanya khiyana kutamweka mahali pabaya. Na Amesema Aliyetukuka:

 

﴿إِنَّ اللّهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤدُّواْ الأَمَانَاتِ إِلَى أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُواْ بِالْعَدْلِ إِنَّ اللّهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ إِنَّ اللّهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا (النساء 58).

 

Hakika Allaah Anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini Allaah ni mazuri sana. Hakika Allaah ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona” (4: 58).

 

Pia Mtume (صلى الله عليه وسلم) ametuamuru kutekeleza amana katika hali zote na hilo lilifahamika hata kwa wasikuwa Waislamu wa zama zake hata wa sasa pia. Imepokewa na ‘Ubaydullaah bin ‘Abdillaah kuwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنهما) alimpasha habari:

أخبرني أبو سفيان أن هرقل قال له سألتك ماذا يأمركم؟ فزعمت أنه أمركم بالصلاة والصدق والعفاف والوفاء بالعهد وأداء الأمانة. قال: وهذه صفة نبي.

 

Alinieleza Abu Sufyaan (رضي الله عنه) kuwa Heraclius (Hiraql) alimwambia nilikuuliza (huyu Mtume) anawaamuru nini? Ukadai kuwa anawaamuru msimamishe Swalah, muwe wakweli, muwe safi (siozini), kutekeleza ahadi na amana. Akasema: Hizo ni sifa za Nabii (Al-Bukhaariy).

 

Enyi ndugu zangu watukufu, khiyana ya amana ni miongoni mwa alama za unafiki. Ametufahamisha hayo mkweli, mwenye kusadikiwa katika Hadith ya ‘Abdullaah bin ‘Amr bin al-‘Aasw (رضي الله عنهما) kuwa Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema:

 

}أربع من كن فيه كان منافقا خالصا ومن كانت فيه خصلة منهن كانت فيه خصلة من النفاق حتى يدعها: إذا اؤتمن خان وإذا حدث كذب وإذا عاهد غدر وإذا خاصم فجر{ متفق عليه.

 

Mtu yeyote akiwa na mambo manne atakuwa mnafiki hasa (kamili), na kama atakuwa na moja katika hayo manne atakuwa na sifa ya unafiki mpaka aliache. Akiaminiwa hufanya hiyana; na akizungumza anaongopa; na apotoa ahadi huvunja na anapogombana anaiacha haki na kuwa jeuri” (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na amesema Abu Hurayrah (رضي الله عنه):

 

بينما النبي صلى الله عليه وسلم في مجلس يحدث القوم جاءه أعرابي فقال: متى الساعة؟ فمضى رسول الله صلى الله عليه وسلم يحدث فقال بعض القوم سمع ما قال فكره ما قال وقال بعضهم بل لم يسمع حتى إذا قضى حديثه قال: }أين السائل عن الساعة؟{ قال: ها أنا يا رسول الله قال: }إذا ضيعت الأمانة فانتظر الساعة{ قال: كيف إضاعتها؟ قال: }إذا وسد الأمر إلى غير أهله فانتظر الساعة{

 

Alipokuwa Mtume (صلى الله عليه وسلم) alipokuwa anakhutubia kikao cha watu, mara akaja Mbedui na kuuliza: “Qiyaamah kitakuwa lini?” Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) akaendelea na mazungumzo yake. Hapo wakasema baadhi ya watu: “Amesikia alichoulizwa, lakini akachukia kukatizwa”. Na wengine wakasema: “Bali hajasikia”, mpaka alipomaliza mazungumzo yake, akasema: “Yuwapi muulizaji kuhusu Qiyaamah?” Akajibu: “Nipo hapa, ewe Mtume wa Allaah”. Akasema: “Inapopotezwa amana (kukawa na khiyana) basi ngojeeni Qiyaamah”. Akaulizwa: “Na itapotea vipi?” Akasema: “Pindi uongozi unapopatiwa watu wasiostahiki basi ngojeeni Qiyaamah” (Al-Bukhaariy).

 

Mvurugiko na machafuko mengi yanayotokea na yanayoendelea kutokea hivi sasa ni kwa sababu ya khiyana na kuchaguliwa kwa wasiofaa katika madaraka tofauti ya uongozi. Inabidi kama Waislamu tushikane barabara na muongozo wa Dini yetu Tukufu, miongoni mwayo ikiwa ni kutekeleza amana na kuwarudishia wanaostahiki.

 

Na kupotea kwa amana pia kumetabiriwa na Mtume (صلى الله عليه وسلم) kwa kiasi ambacho katika kijiji au mji hakutakuwa na waaminifu wenye kuchunga na kudhibiti amana ila wachache. Allaah Aliyetukuka Atujaalie tuwe wenye kuichunga amana.

 

Pia tufahamu kuwa yule mwenye sifa hiyo ya khiyana hatokuwa ni mwenye kutazamwa Siku ya Qiyaamah na Allaah Aliyetukuka. Kila mmoja ajiulize, Ikiwa Hutotazamwa na Allaah Aliyetukuka Utakuwa Wapi? Kila mmoja wetu atajijibu mwenyewe. Imepokewa na Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kuwa Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema:

 

(قال الله ثلاثة أنا خصمهم يوم القيامة رجل أعطى بي ثم غدر ورجل باع حرا فأكل ثمنه ورجل استأجر أجيرا فاستوفى منه ولم يعطه أجره) رواه البخاري.

 

“Allaah Anasema: Nitakuwa dhidi ya (watu) watatu Siku Ya Qiyaamah; mtu anayefunga fungamano kwa jina langu kisha akafanya  usaliti, na anayemuuza mtu huru (kama mtumwa) na kula thamani yake, na anayemuajiri mtu akafanyiwa kazi zake kwa ukamilifu lakini hamlipi ujira wake.” (Al-Bukhaariy).

 

Share