Hekima Ya Kutokufunga, Kuswali Wakati Wa Hedhi, Na Tawassul
SWALI
Assalam aleikum warahmatullah wabarakatu,
Inshaallah ulifunga mwezi wa ramadhan kwa kheri na barka. Ya rabi atutakabaliye saumu zetu na dua zetu na atughufuriye dhambi zetu, Amin.
I just have couple questions and will appreciate if you can help me out inshaallah.
Why is that when a woman is on her periods, she is not allowed to fast, read or even touch qur'an? I understand it's because one is not considered to be "clean" during that time. However, si ni mngu mwenyewe ndiye alieumba wanawake kupata periods? Why can we not
pray to him then when we are on our periods? Why then do we also have to pay back for the days that we didn't fast?
Is one allowed to recite (read) "Tawasul" when they are on their periods? Some people read it every thursday night and usually even at "taaziya's". Mtu akifa, jamaa husoma tawassul alafu wakamtiliya maiti fatha. Also, for example, I have it on tape and I would usually play it in the car and my children and I will follow along.
Saa nyengine hujaribu kuwaelezea non muslims how certains things are perceived in Islam but mara nyengine hushindwa kwa vile mimi
mwenyewe huwa sina jawabu.
Nitashukuru sana kama utaweza kunielezea zaidi juu ya habari hii.
Fil amanillah
JIBU:
AlhamduliLLah, Waswalaatu Was-salaam 'alaa Rasuli-Llah صلى الله عليه وآله وسلم Amma ba'ad,
Kwanza:
Muumini inampasa ajisalimishe katika sheria za Allaah سبحانه وتعالى na akubali zote hata kama hajui sababu zake hizo sheria, bali imtosheleze kuwa hiyo ndio amri ya Allaah سبحانه وتعالى na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))
((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake Wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi)) [Al-Ahzaab: 36]
)) إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ))
((وَمَن يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّهَ وَيَتَّقْهِ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْفَائِزُون))
((Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumetii! Na hao ndio wenye kufanikiwa))
((Na wenye kumtii Mwenyeezi Mungu na Mtume Wake, na wakamuogopa na kumcha Mwenyeezi Mungu, basi hao ndio wenye kufuzu)) [An-Nuur: 51-52]
Pili:
Muumini inampasa aamini kwa yaqini kuwa Allaah سبحانه وتعالى Ni Mwenye Hikma na kwamba Anapoamuru jambo lolote, basi Huamuru kutokana na Hikma yenye upeo wa hali ya juu kabisa, na Haamrishi jambo ila litakuwa kwa sababu lina manufaa kwa binaadamu na Hakatazi jambo pia ila litakuwa kwa sababu lenye kuwahifadhi binaadamu kutokana na mauovu na madhara.
Ibn Kathiyr amesema katika kitabu chake 'Al-Bidaayah Wan-Nihaaya 6/79' kwamba: "Sheria ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni sheria iliyokamilika kabisa, haikuacha jambo lolote jema lililojulikana na wenye hikma (werevu) isipokuwa ameliamrisha. Na hakuacha jambo lolote lillilokua ovu na ambalo limejulikana na wenye hikma isipokua amelikataza. Hakuamrisha jambo na watu wakasema "Laiti kama asingeliamrisha". Na Hakukataza jambo wata wakasema "Laiti kama asingelikataza"
Majibu ya maswali tutayaweka kwa mpangilio kama yalivyokuja maswali yenyewe:
1. Kwa nini mwanamke akiwa katika hedhi haruhusiwi kusoma Qur'aan :
Maulamaa wamekubaliana kwamba mwanamke anaruhusiwa kusoma Qur'aan anapokuwa katika siku za hedhi. Ikhtilaaf imekuja katika mas-ala ya 'kugusa' Qur'aan ambayo nayo pia Maulamaa wengi wameona kwamba hedhi sio kizuizi cha kumzuia mwanamke asiguse Qur'aan.
Kwa kupata maelezo zaidi ya Swali hili, tafadhali ingia katika kiungo hiki kiufatacho katika Alhidaaya ambako tumelijibu kwa kirefu zaidi.
Kushika Na Kusoma Qur-aan Katika Hedhi, Nifaas Na Janaba
2. Kwa nini mwanamke akiwa katika hedhi haruhusiwi kufunga.
Kama tulivyoelezea mwanzo kwamba kila maamrisho na makatazo ya Mola wetu na Mtume Wake ni amri zinazotupasa tuzikubali bila ya kutaka kujua kwa nini, na bila shaka huwa ni kutokana na hikma fulani zenye aidha manufaa au madhara kwetu. Tunaweza kuzifahamu sababu zake, na tunaweza tusizifahamu, na kufichwa kwake ni Ujuzi Wake Pekee Allaah سبحانه وتعالى
Na wataalamu hujitahidi kujua sababu zisizotajwa kwa kadiri ya jitihada yao. Na kuhusu mas-ala haya wamesema yafuatayo:
a) Wengine wameona kuwa sababu haijulikani kwetu ila na Mwenyewe Allaah سبحانه وتعالى .
b) Imam wa Al-Haramayn amesema: "Hatujui kwa nini Swawm haifai kwa sababu Twahaarah hapa sio sharti yake" [Al-Majmu'u 2/386]
c) Wengine wamesema kuwa ni Rahma kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى kwa wanawake, kwani wanapopoteza damu nyingi katika hedhi huwafanya wawe dhaifu. Kwa hiyo atakapofunga mwanamke akiwa katika hedhi atazidi kuwa dhaifu kutokana na hedhi na kufunga na hii itakuwa ni jukumu lenye kuzidi uwezo wake na huenda likamletea madhara. [Shaykhul-Islaam ibn Taymiyah katika Maj'muu Al Fataawa 25/234]
d) Mwanamke anapokuwa katika hedhi anakuwa katika hali ya kuumwa, na hatudhani kama mwanamke yeyote atapenda kuwa katika taabu mbili; ya kuumwa kwa kumwagikwa na damu ambayo inamdhoofisha hali yake, na kukaa na njaa na kiu siku siku zote hizo.
Vile vile hedhi ni kutokwa na damu chafu, kwa hiyo ni katika njia mojawapo ya kusafisha sehemu ya kizazi cha mwanamke. Na kufunga (Swawm) vile vile ni njia mojawapo ya kusafisha mwili mzima pamoja na umeng'enyaji chakula (digestive system). Kwa hiyo kusafishwa mwili kwa njia mbili hizi huenda zikawa ni ngumu na tabu kufanyika kwa wakati mmoja, kwa hiyo pengine ni Rahma Yake Allaah سبحانه وتعالى kumuacha mwanamke asifunge wakati huu, Subhana Allaah!
3. Na kwa nini basi inabidi tulipe deni za siku tusizofunga?
Ama kulipa deni la Swawm ni amri kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kama ilivyothibitika katika Hadiyth zifuatazo, na kama tulivyosema mwanzo kuwa Muumini anatakiwa awe menye kutii amri ya Mola Wake na Mtume wake bila ya kutia shaka jambo:
عن عَائِشَة رضي الله عنها (( كُنَّا نَحِيضُ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَنُؤْمَرُ بِقَضَاءِ الصَّوْمِ , وَلا نُؤْمَرُ بِقَضَاءِ الصَّلاةِ )) . مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ .
Kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها ((Tulikuwa katika hedhi wakati wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na tuliamrishwa kulipa funga lakini hatukuamrishwa kulipa Swalah)) [Al Bukhaariy na Muslim]
عن أَبُو سَعِيدٍ : قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم : (( أَلَيْسَ إحْدَاكُنَّ إذَا حَاضَتْ لَمْ تُصَلِّ وَلَمْ تَصُمْ , فَذَلِكَ مِنْ نُقْصَانِ دِينِهَا )). رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
Kutoka kwa Abu Sa'iyd, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Je, Haijakuwa kwamba mmoja wenu anapokuwa katika hedhi haswali wala hafungi? Hii ndio maana ya kuwa mmepungukiwa (wanawake) na dini (yaani shuruti za dini)) [Al-Bukhaariy]
Vile vile mwanamke anatakiwa kulipa deni lake wakati akiwa katika hali ya afya ambayo itakuwa sio tabu kwake kulipa. Na kulipa deni la Swawm ni jambo lisilokuwa la kufanyika kila mwezi kama ingelikuwa hali ya Swalah, bali ni jambo la mara moja.
Pia kama tulivyofundishwa katika Qur'aan na Sunnah kuwa Swawm ina manufaa kwa binaadamu kwani inamuweka mtu katika 'Taqwa' (Ucha Mungu) kwa hiyo kulipa deni na kuwa katika hali ya Swawm ni jambo jema lenye manufaa kwa nafsi zetu.
4. Kwanini hatuswali tunapokuwa katika hedhi?
Hii vile vile ni Hikma Yake Allaah سبحانه وتعالى ya kumuondoshea mwanamke mwenye hedhi jukumu la Swalah tano wakati yuko katika hali ya kumwagika damu. Hedhi ni 'adhaa' (uchafu, dhara) kama ilivyokuja katika aya:
((وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُواْ النِّسَاء فِي الْمَحِيضِ ((
((Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi)) [Al-Baqarah: 222]
Kwa hiyo ni Rahma na Hikma ya Allaah سبحانه وتعالى kumuondoshea mwanamke mwenye hedhi wajibu wa Swalah.
5. Kwa nini hatulipi Swalah?
Mwanamke halipi Swalah kwa sababu ni jambo linalotokea kila mwezi kwa hiyo kulipa Swalah zote za siku taqriban za siku saba kila mwezi, itakuwa ni jukumu gumu kulitimiza, na ndio maana akapata rukhsa hii kutokana na Upole na Rahma Yake kubwa Allaah سبحانه وتعالى kwa viumbe vyake.
6. Je, anaruhusiwa mtu kusoma 'Tawasul' anapokuwa katika hedhi?
Anaruhusiwa mwanamke kusoma tawassul na aina yoyote nyingine ya dhikr (ukumbusho) wa Mwenyeezi Mungu kama Du'aa, istighafaar na kadhalika, kwani ikiwa anaruhusiwa mwanamke kusoma Qur'aan katika hedhi hakutokuwa na shaka kwa jambo hili la tawasul na dhikr.
Jambo muhimu la kuzingatia
Kusoma tawassul na Adhkaar zozote lazima kwanza ahakikishe mtu kama ziko katika mafundisho ya Sunnah na sio mafundisho ya watu waliopita, kama mfano kuna baadhi ya watu wanashikilia sana kusoma tawassul ya Nabahani na hali haipo katika misingi sahihi maana kuna maneno yasiyofaa ndani yake, na husoma kila siku kila mara na kuacha zile alizotufundisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم.
Kufanya hivi kunadhihirisha mapenzi ya watu kuwa yako zaidi nyoyoni mwetu kuliko mapenzi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم .
Ukumbusho ulio bora kabisa ni kusoma maneno ya Mwenyeezi Mungu (Qur'aan). Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundisha adkhaar za asubuhi na jioni, na za kumtaja Allaah سبحانه وتعالى wakati wote.Tujiulize, je, Tunazitimiza hizi kwanza? Ikiwa Muislamu atajishughulisha na ukumbusho huu basi atakuwa amefanya ibada isiyo na shaka kabisa kwani ndizo zilizothibiti katika sheria ya Kiislamu. Pia atakuwa na uhakika wa kujipatia thawabu zake kamili. Ama kujishughulisha na ukumbusho usio katika mafundisho ya Sunnah ni jambo la kumuingiza mtu katika mambo ya uzushi kwani mara nyingi ukumbusho huo humtaka mtu asome siku fulani, wakati fulani kwa idadi fulani na kadhalika na hata wakimwombea maiti, bila ya kuwa na dalili yoyote kutoka katika Qur'aan na Sunnah. Kwa hiyo ni muhimu kuepukana nayo.
Mafundisho ya Sunnah yalio Sahihi ya ukumbusho wote taqriban yamo katika kitabu cha 'Hiswn Al-Muslim' na kinapatikana katika Alhidaaya kwenye kiungo hiki kifuatacho,
Wa Allaahu A'alam.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


