Tawbah Ya Kweli Mtu Husamehewa Madhambi Yote

 

SWALI:

Nilikuwa na rafiki yangu tukizungumzia kuhusu mambo ya toba yaani kutubia, mimi nikasema kwamba iwapo mtu utatubia toba ya kweli yaani ya moja kwa moja basi unaweza kusamehewa makosa yako yote na M/mungu.

Nae Rafiki yangu akasema kwamba hatakama ukitubia vipi kama uliwahi kumshirikisha M/mungu na chochote basi kosahilo huwezi kusamehewa, sasa jee ninani ambae yuko sawa na jamba hilo?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho


Toba inahitajika kwa kila dhambi tunalofanya, dogo au kubwa. Allaah سبحانه وتعالى  Anasema:

 

}}وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَا الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ{{

{{Na tubuni nyote kwa Allah, enyi Waumini ili mpate kufaulu}}

An-Nuur :24:31

Pia Amesema:

}}يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا{{

{{Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allah toba ya sawa sawa}}

At-Tahirym   66: 8 .

An-Naswuuh katika toba ina mambo matatu:

1.           Kujumlisha azma bila ya kuwa na kusita sita.

2.           Kuacha madhambi yote.

3.          Kuyamaliza bila ya kubakisha hata doa wala ila. Na kuwa na hofu ya Allaah سبحانه وتعالى na kunyenyekea Kwake na kuwa matumaini kwa aliyo nayo na kuogopa yaliyo Kwake.              

Toba ina masharti yake lau yatapatikana basi Allaah سبحانه وتعالى    atakusamehe dhambi lolote ulilolifanya. Yakiwa maasia ni baina ya mja na Allaah سبحانه وتعالى  hakuna kabisa haki ya mwanadamu basi yatakuwa na masharti matatu:

1.            Kuacha hayo maasia.

2.             Kujuta kwa kufanya hayo maasia.

3.             Kuazimia kutorudia tena milele.

Na ikiwa katika maasia yenyewe ipo haki ya mwanadamu masharti yake yatakuwa manne: Matatu ya juu na kurudisha haki ya mwenziwe na kutaka msamaha kutoka kwake.

Allaah سبحانه وتعالى Ametuelezea kuwa Yeye husamehe madhambi yote maadamu mja hatakufa katika hali ya kumshirikisha Allaah سبحانه وتعالى  au kufanya madhambi yaliyo makubwa. Hebu tusome pamoja Aayah zifuatazo:

}}وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا{{

 }} يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا{{

  }}إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُوْلَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا{{

}} وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّهِ مَتَابًا{{



 
{{Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi Aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara}}

 {{Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka}}.

 {{Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Allaah Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Allaah  ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}}.

{{Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allaah}}   

Al-Furqaan  25: 68 – 71 .

Na Amesema tena:

}}قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَى أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ{{



{{Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Allaah . Hakika Allaah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}}

Az-Zumar 39: 53 .

Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  anatuelezea hayo pia:

((اتق الله حيث ما كنت , واتبع السيئة الحسنة تمحها))  

((Mche Allah popote ulipo na ufuatishe jambo baya kwa zuri, litalifuta (hilo baya))) (at-Tirmidhy, na akasema ni Hadith Hasan na nuskha nyengine ni Hasan Sahiih. Pia imenukuliwa na Ahmad na ad-Daarimi kutoka kwa Abu Dharr na Mu‘adh رضي الله عنه  nayo ni Hadith Sahiih).

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema:

((إن الله يبسط يده بالليل ليتوب مسيء النهار، ويبسط يده بالنهار ليتوب مسيء الليل حتى تطلع الشمس من مغربها   ((رواه مسلم .  عن أبي موسى العشعري رضي الله عنه

((Hakika Allah Aliyetukuka Ananyosha mkono wake usiku kwa wanaotubu kwa makosa yao ya mchana. Na Ananyosha mkono Wake mchana kwa wanaotubu kwa makosa yao ya usiku mpaka jua litoke upande wa magharibi))

 (Muslim kutoka kwa Abi Musa al-Ash‘ariy رضي الله عنه  

Na amesema tena:

((إن الله يقبل توبة العبد ما لم يغرغر)) الترمذي و أحمد وإبن ماجه وصححه إبن حبان

))Hakika Allah Aliyetukuka hukubali toba ya mja maadam roho haijafika kooni (hayuko katika kukata roho)( (at-Tirmidhy, Ahmad na ibn Maajah na ameisahihisha Ibn Hibbaan).

Hizi aya na Hadithi ni dalili tosha ya kwamba toba inakubaliwa kwa madhambi yote maadamu mja atafuata masharti yake. lakini tujue ya kwamba toba haikubaliwi kwa hali hii Aliyoitaja Allaah سبحانه وتعالى :

}}وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّى إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الآنَ وَلاَ الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ أُوْلَـئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا{{

{{ Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale wanao kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu}}

 An-Nisaa 4: 18

Kwa ajili hiyo Allaah سبحانه وتعالى  Aliikataa toba ya Firauni pale alipokuwa anaghariki katika bahari

}}وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا حَتَّى إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لا إِلِـهَ إِلاَّ الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَاْ مِنَ الْمُسْلِمِينَ{{

{{Tukawavusha bahari Wana wa Israili, na Fir'awn na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui. Hata Fir'awn alipo kuwa anataka kuzama akasema: Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliye muamini Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa walio nyenyekea!}}   Yunus 90

Allaah سبحانه وتعالى Akamuuliza Fir'awn wakati anatapatapa na kuomba na kudai kuwa kaamini:

}}آلآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ{{

{{Alaa! Sasa? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa

mafisadi!}}   Yunus 91

Kisha Akaikataa Tawbah yake katika hali hii:

}}فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ{{

{{Leo, basi, tutakuokoa kwa mwili wako, ili uwe Ishara kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara zetu}} Yunus  92

 Aya hizi kuna mazingatio makubwa kwa Waumini hasa na wanaadamu kwa ujumla.

Wa Allaahu A'alam

 

Share