Zingatio: Weka Matumaini Kwa Allaah

 

Zingatio: Weka Matumaini Kwa Allaah

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakika kalimah ya Uislamu ambayo tunaiamini Waislamu, ndio ufunguo wa Jannah. Kalimah ambayo yatakiwa kutamkwa kwa ulimi, kuwekwa ndani ya moyo na kusadikishwa kwa vitendo. Kalimah hiyo ni Laa ilaaha illa Allaah Muhammadun Rasuulu Llaah – Hakuna Rabb Apasaye Kuabudiwa ila Allaah na Muhammad ndiye Rasuli Wake.

 

 

Kinachotakiwa hapo ni kumsadikisha Rabb Mlezi kwa vitendo sio kwa kutamkwa kama ambavyo wengi wanafanya. Hapo ndipo tutapata salama Siku ya Hisabu In shaa Allaah. Ni kawaida ya wanaadamu kumkosea Muumba na ndio maana akaitwa kuwa ni insaan – mwenye kusahau. Wahenga wanatwambia ya kwamba: kutenda kosa (kwa kusahau) sio kosa ila kurudia kosa ndio kosa. Bado wakati wa kuweka matumaini Kwake Muumba upo, alimuradi tu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hajazichukua roho zetu na kuviweka viwiliwili vyetu kwenye maisha ya barzakh. Izingatie vizuri siku hiyo ya kutoka roho pamoja na kulazwa kwenye maisha mapya ya kaburini.

 

 

Hata kama tutakuwa na vitendo viovu na makosa ya hapa na pale, bado (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaweza kututakabalia toba zetu na kutufungulia milango ya khayr. Kitu kikubwa kinachohimizwa hapa ni kutomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kiumbe chochote kama ambavyo imekuja kwenye Hadiythul-Qudsiyy, Allaah Mtukufu wa Mbingu na Ardhi, Amesema:

 

 

"Ee Mwana wa Aadam utakaponiomba na kuweka matumaini kwangu, basi Nitakusamehe makosa uliyoyafanya na sitojali. Ee Mwana wa Aadam kama dhambi zako zingefika mawingu ya mbingu na wewe ukaomba msamaha Kwangu, Ningekusamehe.  Ee Mwana Wa Aadam kama ungelinijia na dhambi kubwa kama dunia na ukanikabili bila ya Kunishirikisha Nitakupa maghfira." [Imesimuliwa na Anas na kupokelewa na At-Tirmidhy na Ahmad]

 

 

Rahma Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Zimetawala ndani ya maisha yetu, kwani bila ya shaka hakuna neema kubwa tuliyopatiwa kuliko uhai. Neema ambayo inapokatika hairudi tena. Kilichokusanywa ndicho kinachopokelewa. Hakuna tunachoweza kukiongeza baada ya hapo ila yale mambo matatu yanayomfaa Muislamu baada ya kutoka roho (swadaqah yenye kuendelea, mtoto anayekuombea na elimu yenye manufaa). Tujitahidi kuwa na himma ya diyn yetu hii tukufu kwa kuweka matumaini yetu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Share