Skip navigation.
Home kabah

Mungu Hana Mshirika

 

 

   Abdallah Bin Eifan
(Jeddah, Saudi Arabia)



 (1)  Salaam zangu natuma, ziwafike Afrika,
        Mungu Awape hekima, mzidi kuneemeka,
        naomba Zake rehema, zivuke zote mipaka,
        Mungu Hana mshirika, Hana mwana wala mama.

 (2)   Hana mwana wala mama, Mungu Hana mshirika,
        Hana mke Amesema, Hana baba wala kaka,
        Tokea zama za zama, pekee Ametajika,
        Mungu Hana mshirika, Hana mwana wala mama.

 (3)   Kaunda ardhi na mbingu, peke Yake Msifika,
        Kawaumba binadamu, iblisi na malaika,
        Tupate kumuabudu, ibada Anavyotaka,
        Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (4)  Kutoka kwenye mchanga, binadamu kaumbika,
       atarudia mchanga, mauti yakimfika,
       atoke kwenye mchanga, wakati wa kufufuka,
       Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (5)  Kamuumba iblisi, kwenye moto unawaka,
       na hapo atajilisi, motoni atachomeka,
       adui wetu halisi, lazima kumuepuka,
       Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama.

 (6)  Malaika kwenye nuru, Amewaumba Rabuka,
       maisha hawakufuru, ibada wameishika,
       Mungu Anavyoamuru, upesi wanaridhika,
       Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (7)  Riziki ipo mbinguni, huko ndiko inatoka,
       ipo Mwake mikononi, tena imeshagawika,
       tuwe tuna shukurani, bila ya kulalamika,
       Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (8)  Yupo macho Maulana, hukuti Akizeeka,
        kila kitu Anaona, yote yanayotendeka,
        hakuna ya kufichana, Kwake vinaeleweka
        Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (9)  Yupo karibu na sisi, dua Kwake zinafika,
        ili zifike upesi, tuzidi Kumkumbuka,
        tuache yote maasi, tuyaache kwa haraka,
        Mungu Hana Mshirika, Hana mwana wala mama.

(10)  Mungu Atupe uzima, hapa mwisho kuandika,
        Atupe nguvu na hima, radhi Zake tunataka,
        Atupe nzuri hatima, dhambi zipate futika,
        MUNGU HANA MSHIRIKA, HANA MWANA WALA MAMA.




Bismilahi awali,Kauli

Bismilahi awali,Kauli naitamka,
Iliyo jaa amali,Na furaha kuoneka,
Naye wetu JALALI,Utukufuka anataka,
Imefika Afrika,Nashukuru Abdallah.

Nashukuru Abdallah,Dua yako kwetu sisi,
Hiyo ni tunu ya ALLAH,Nakutoa wasiwasi,
Na kila lenye madhillah,kwetu pia atughasi,
Allah akuzidishiye,Kheri zake kwako pia.

Abdallah Bin Eifan,Pokea nawe ujumbe,
Na uweka shairini,Kama mpini wa jembe,
Sote tupo Duniani,tukwepe sana uzemnbe,
Allah akuzidishiye,Busara nazo khekima.

Nakubali kauliyo,ALLAH hana mshirika,
Nawala sinayo choyo,Umenena la kushika,
Ya dhihiri khekimayo,Ushari kufunika,
Allah akuzidishiye,Utulivu hadi KESHO.

Funzolangu naandika,IBADA nazungumza,
Waja sasa twapotoka,Kusali tunapuuza,
Ndiyo maana natamka,Ukimya kuukatiza,
UMMA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

Waja twatenda machafu,Kifo tumesahau,
Tumeacha uongofu,Mafunzo tunadharau,
Hili lanipa upofu,Asili kuzisahau,
WAJA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

Ibada KAUMU zote,Toka mzawa Adamu,
Wamefanza watu wote,Kwa machungu na matamu,
Sisi twafanza ubwete,Sasa twaiona sumu,
WAJA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

MTUNE wetu mkama,Alitutetea sana,
Hamsini akasema,Kwetu hizi ngumu sana,
Naye wetu ALLAHUMA,Akazipunguza sana,
WAJA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

Zikasalizwa tano,Kwa vipindi mbali mbali,
Muda wa dakika tano,Tunaona ni kabali,
Twaona bora mavuno,Mashamba yetu ya mbali,
WAJA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

Tuikumbuke kauli,MTUME aliyo nena,
Kwa kila mwenye akili,Kaburi yake kufana,
Ni kuijenga awali,Uzima bado wa puna,
WAJA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

Ibada inayo raha,Duniani tukitoka,
Tena nikubwa staha,Pepo zetu kufunguka,
Inayo nyingi buraha,Motoni tutachomeka,
WAJA TUFANZE IBADA,NDIYO SABABU KUUMBWA.

Ibada nahitimisha,waja tunakumbushana,
Mazuri kufurahisha,Sisi tunaambiana,
Mabaya yakukarisha,Pia tunakatazana,
TUJAZE HOFU KWA ALLAH,WAJA TUFANZE IBADA.

(1) Salaam ndugu Mateno,

(1) Salaam ndugu Mateno, hujambo u hali gani ?
Nimeyasoma maneno, na dua zenye thamani,
Ninakushukuru mno, Aitikie Manani,
Naitikia "Amin", Udumu Mshikamano.

(2) Udumu mshikamano, udugu katika dini,
Tuwe mmoja mkono, asitushinde shetani,
Akitaka mapambano,tumshinde tumlaani,
Naitikia "Amin", Udumu Mshikamano

(3) Mizuri yote mifano, tuonyeshe Waumini,
Nguzo za dini ni tano, tuzishike kwa makini,
Swala zetu pia tano, tuziswali msikitini,
Naitikia "Amin", Udumu Mshikamano

(4) Beti nne sio tano, nimefika kikomoni,
Ni mwanzo wa muungano, na kupeana maoni,
Na mambo yawe "mswano", tuwe "mbuya" maishani,
Naitikia "Amin", Udumu Mshikamano.