Mashaytwaan Na Majini Wanaojiita Sharifu

SWALI:

Assalaam Allaykum

 kwa nini mashetani ya kijini yanapenda kujinasibisha na Uislam? Kama kutumia majina ya sharifu na kusema yametokea Makka au Madina.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa ndugu yetu muulizaji kuhusu mas-ala ya mashetani na majini. Shetani ni kiumbe kilicho asi maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Anaweza kuwa ni binadamu au jinni, na ndio Allaah Aliyetukuka akasema:

((مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ))

 

((الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ))  

 

 ((مِنَ الْجِنَّةِ وَ النَّاسِ))

))Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannas))

((Anayetia wasiwasi katika vifua vya watu)).

((Kutokana na majini na wanaadamu))   [114: 4 – 6 ]

 

Na kuhusu mashetani wa kibinadamu:

 

((وَإِذَا لَقُواْ الَّذِينَ آمَنُواْ قَالُواْ آمَنَّا وَإِذَا خَلَوْاْ إِلَى شَيَاطِينِهِمْ قَالُواْ إِنَّا مَعَكْمْ إِنَّمَا نَحْنُ مُسْتَهْزِؤُونَ))

))Na wanapokutana na walioamini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao na mashetani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu))    [2.14]

Tukirudi katika swali lako ni kuwa majini kama binadamu wanaishi sehemu tofauti na wapo wengine ni Waislamu na wengine Makafiri. Mara nyingi ukiishi sehemu ya Waislamu ni muhali kupata jina la Joseph na Caroline, majina mengi yatakuwa ni Muhammad,  Abu Bakr, 'Umar, 'Uthmaan, 'Aliy, Khadiyjah, 'Aishah, na kadhalika.

Sasa majini wakiwa katika sehemu za Waislamu mara nyingi watajinasibisha na Uislamu na pia kujipatia majina ya Kiislamu. Na ikiwa watajipatia majina hayo basi wanaweza kusema wao wanatoka Makkah au Madiynah. Lakini hizo ni zao kwa ndimi zao na mara nyingi wanakuwa ni waongo kabisa.

Asilimia kubwa wanasema uwongo na nisba ndogo sana ya ukweli.

Mfano mzuri ni ule wa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyepatiwa jukumu la kulinda mali ya Zakaah na Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuja kwake usiku mmoja mtu aliyeanza kuchukua (kuiba) vitu, naye (Abu Hurayrah) akamshika, lakini yule bwana akajitetea ya kuwa ana watu wengi wanaonitegemea. Nilimuonea huruma na nikamuacha kwa ahadi kuwa hatarudi, lakini asubuhi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza kuhusu huyo mtu na akaniambia kuwa amekudang’anya na kuwa atarudi tena. Na siku ya pili na ya tatu alirudi kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipomshika siku ya nne alimuomba asimpeleke kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na badala yake atamfundisha maneno yatakayomsaidia na hapo akamwambia, “Soma Ayatul Kursiy (2: 255) kwani ukisoma aya hiyo Allah atakuekea mlinzi ambaye atakulinda na shetani mpaka asubuhi”. Asubuhi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuhusu mgeni wake naye akamueleza yaliyojiri. Hapo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Hakika amesema kweli japokuwa yeye ni Kadhuub (mwingi wa kusema uwongo)”. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Je, unajua ulikuwa unazungumza na nani kwa siku zote hizo hizo”. Akasema: “Hapana”. Akamwambia (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Ulikuwa unazungumza na shetani” (Al-Bukhaariy).

Hivyo, mara nyingi wanasema uwongo hao mashetani kwa hivo usiwe ni mwenye kuwaamini hata wakisema nini. 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share