Nina Dhiki Na Nina Woga Sana Nifanyeje?

SWALI:

Naomba ndugi zangu mnisaidie na masuali yangu mimi ni nina dhiki sana na husoma sana qurani na mara nyingi huwa naogopa na naogopa sana kusafiri ikifika wakati wasafari mimi huwa nina ogopa sana na inabidi kusafiri kwenda kuona waze wangu na huwa na khofu sana  na shindwa ni fanye nini naomba kama mutaweza kunisaidia kwa sababu naona kama sio kawaida ya binadamu kuwa hivi na uoga mwingi wa kila kitu nina mengi ya kuuliza kwa leo naomba  masuali haya kama mutaweza nisaidia na mimi ndugi zangu  shukran mngu awajazi muzidi kutusaidia masalam.


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwa na dhiki na uwoga wakati una safari. Mas-ala ya uwoga kwa mwanadamu ni kitu cha kawaida. Wapo wenye kuogopa wadudu, au bahari, au kuwa sehemu ya juu kama katika ghorofa au ndege, au mnyama yeyote yule au kitu kingine chochote kile.

 

Uwoga au wasiwasi kawaida mtu huwa anatiwa na Shaytwaan kwa njia moja au nyingine. Na kutoa uwoga inabidi Muislamu awe akijikinga kwa Allaah Aliyetukuka kwa kusema A‘udhu Billaah minash Shaytwaanir Rajiym. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

Na uchochezi wa Shetani ukikuchochea basi omba ulinzi wa Allaah. Hakika Yeye ni Msikizi, Mjuzi. Hakika wale wamchao Mungu, zinapowagusa pepesi za Shetani, mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki” (7: 200 – 201).

 

Uwoga pia hupatikana kwa wanadamu kwa kufikiria mambo ya mustakbali au kutaka kushindana na Qadar ya Allaah Aliyetukuka. Tufahamu kuwa ni Allaah Aliyetukuka pekee Ndiye Mwenye kujua mambo ya mustakabali. Na uwoga huu huenda ukawa unatokea kwa mtu kuwa alipata ajali barabarani hivyo kila akiingia katika gari fikra ya ajali huwa ukirudi na ukawa ni mwenye kuitia akilini au ni maumbile tu ya mtu. Katika hali zote Uislamu umetupatia ufumbuzi mzuri sana kwa kutuekea du’aa za kusoma na kujikinga za kila wakati. Hivyo, kuondoa uwoga ulio nao, pindi unapokuwa katika safari na ukaingia katia gari au aina yoyote ya usafiri basi soma du’aa ifuatayo:

 

اللهُ أكبَر ، اللهُ أكبَر ، اللهُ أكبَر، سُـبْحانَ الَّذي سَخَّـرَ لَنا هذا وَما  كُنّا لَهُ مُقْـرِنين،  وَإِنّا إِلى رَبِّنـا لَمُنْقَـلِبون، اللّهُـمَّ إِنّا نَسْـأَلُكَ في سَفَـرِنا هذا البِـرَّ وَالتَّـقْوى، وَمِنَ الْعَمَـلِ ما تَـرْضى، اللّهُـمَّ هَوِّنْ عَلَـينا سَفَرَنا هذا وَاطْوِ عَنّا بُعْـدَه، اللّهُـمَّ أَنْـتَ الصّـاحِبُ في السَّـفَر، وَالْخَلـيفَةُ في الأهـلِ، اللّهُـمَّ  إِنّـي أَعـوذُبِكَ مِنْ وَعْـثاءِ السَّـفَر، وَكَآبَةِ الْمَنْـظَر، وَسوءِ الْمُنْـقَلَبِ في المـالِ وَالأَهْـل.

 Allaahu Akbar x 3, Subhaana Lladhiy sakhkhara lanaa hadhaa wa maa kunnaa lahu muqriniyna wa innaa ila Rabbinaa lamunqalibuuna. Allaahumma innaa nas’aluka fi safarinaa hadhaa al-birra wat-Taqwaa wa minal ‘amali maa tardhwaa. Allaahumma hawwin ‘alayna safaranaa hadhaa watw-wi ‘annaa bu‘dahu. Allaahumma Antasw-swaahibu fis safari wal Khaliyfatu fil ahli. Allaahumma inniy a‘udhu bika min wa‘thaa’ as-safari wa kaabatil mandhari wa suuu’i al-munqalabi fil maali wal ahli”.

 

 “Allaah ni Mkubwa,  Allaah ni Mkubwa, Allaah ni Mkubwa, Ametakasika Ambaye Ametudhalilishia sisi hiki (chombo au huyu mnyama) na hatukuwa sisi kwacho ni wenye uwezo, na sisi kwa Mola wetu tatarejeshwa.  Ee Allaah hakika sisi tunakuomba katika safari  yetu hii wema na ucha Mungu, na katika matendo Unayoridhia, Ee Allaah, ifanye nyepesi safari yetu hii, na ufupishe umbali wake, Ee Allaah, Wewe ndiye Mwenzangu katika safari na Mchungaji wa familia yangu.  Ee Allaah, hakika mimi najilinda Kwako kutokana na ugumu wa safari na ubaya  wa mtizamo na uovu wa kubadilikiwa katika mali na familia”

 

 

Na wakati unaporudi kutoka katika safari utasema:

 

آيِبُـونَ تائِبُـونَ عابِـُدونَ لِرَبِِّـنا حـامِـدُونَ

Aaibuuna taa’ibuuna ‘aabiduuna Lirabbina haamiduuna” (Muslim).

 

“Tunarudi hali ya kuwa tunatubia, tunaabudu, na Mola wetu tunamsifu”

Adhkaar zinasaidia sana na huenda ya kuwa huwa una safari tu bila kusoma du‘aa tuliyoitaja au nyingine yoyote.

 

Pia ipo du‘aa ya kujikinga pamoja na kujilinda na wasiwasi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha du‘aa ifuatayo pindi utakapokuwa na wasiwasi:

 

 

أَعـوذُبِكَلِمـاتِ اللّهِ التّـامّـاتِ مِن غَضَـبِهِ وَعِـقابِهِ ، وَشَـرِّ عِبـادِهِ  وَمِنْ هَمَـزاتِ الشَّـياطينِ وَأَنْ يَحْضـرون.

 

A‘udhu bikalimaati Llaahi at-Taammaati min ghadhwabihi wa ‘iqaabihi wa sharri ‘ibaadihi wa min hamazaati ash-Shaytwaani wa an yahdhwuruun” (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

 

“Najilinda na maneno ya Allaah, yaliotimia kutokana na hasira Zake na adhabu Yake na shari ya waja Wake na vioja vya mashetani na kunijia kwao”

 

Uwoga ni aina ya mtihani, hivyo inabidi usubiri na kuvumilia hadi utakapoweza kuuondosha kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri” (2: 155).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share