Njia Kumi Za Kuhifadhi Qur-aan - 2

 

Imekusanywa Na Ukht Haliymah ‘Abdullaah

 

Kutoka Kitabu

 

كيف تحفظ القرآن في عشر خطوات – حسن أحمد بن أحمد همام

 

 

 

2. HATUA YA PILI

 

UMUHIMU WA KUPOKEA NA KUISIKIA KUTOKA MDOMONI

 

Qur-aan Tukufu siyo kama vitabu vingine ambayo inatosha kutazama na kuisoma ambayo mtu anajitegemea nafsi yake kwani huwezi kutazama katika Mus-haf na kutamka lafdhi bali inahitajika katika kuisoma Qur-aan na Kuihifadhi kuipokea na kusomeshwa kutoka kwenye mdomo wa wasomi na wajuzi wa Tajwiyd (elimu iliyopokelewa kutoka kwa Mtume [Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam]).

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

“Na hakika wewe unafundishwa Qur-aan inayotokana kwa (Allaah) Mwenye hikima, Mjuzi.” An-Naml: 6

 

Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) akiwatamkisha Maswahaba zake Qur-aan, Imekuja kutoka kwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa aliwaambia Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Hakika Mtume wa Allaah anawaamrisha, asome kila mmoja wenu kama alivyofundishwa.”

 

Na hakuna yeyote aliyehifadhi Qur-aan kwa jitihada zake binafsi bila ya kuchukua kwa Mashaykh ila atakuwa mwenye kukosea katika kisomo chake, tuchukulie Mus-haf ya Rasm (mchoro/ maandishi) ya ‘Uthmaaniy haisomwi kama ilivyoandikwa baadhi ya herufi mfano neno “Asw-Swallawaata, Az-Zakawaata” hiyo waaw haitamkwi bali inasomwa “Asw-Swallaata, Az-Zakaata” hivyo katika masharti ya kisomo Sahihi ni kuisoma kutoka kwa Shaykh au Mwalimu.

 

 

3. HATUA YA TATU

 

UMUHIMU WA KUIHIFADHI KWA TAJWIYD

 

Anasema Ibn Jawziy:

 

“Na kuisoma kwa Tajwiyd ni jambo la lazima, na asiyeisoma Qur-aan kwa Tajwiyd anapata madhambi.”

 

Na maana ya Tajwiyd ni kuchunga hukmu za kisomo zilizopo katika vitabu vya Tajwiyd katika Idghaam, Idhwhaar, Ikhfaa, Ghunah, Madda na kuchunga sehemu za kutoa herufi na nyinginezo. Kwani Qur-aan Kariym inatofautiana na vitabu vingine, ni Maneno ya Allaah na kwa mpangilio huu amepokea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) kutoka kwa Jibriyl kutoka kwa Mola Mtukufu na hivyo ndivyo ilivyotufikia.

 

Imepokewa kutoka kwa Ibn Mas’uud alikuwa mtu anamsomea neno lake Allaah:

 

    At-Tawba: 60إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء

 

Alisoma neno “Al-Fuqaraa لِلْفُقَرَاء” bila ya kuvuta Madda, akasema Ibn Mas’uud sivyo hivyo alivyonifundisha Mtume wa Allaah akamwelekeza avute Madda baada ya herufi ya raa.

 

Haina maana uzame katika elimu ya Tajwiyd kwa undani kupita kiasi, muhimu uweze kuisoma Qur-aan kwa hukmu na kujua Tafsiyr yake ili uweze kuifanyia kazi.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

“Wale katika (Ahlul Kitaab) tuliowapa Kitabu (Taurati, Injili, Zaburi…) wakakisoma kama ipasavyo kukisoma (bila ya kupotea Tafsiri yake wala kutoa hili na kutia lile), hao huiamini hii Qur-aan wakasilimu). Na wanaokikanusha (hicho Kitabu chao wakapinduapindua tafsiri yake na wakaongeza na wakapunguza), basi hao ndio wenye hasara.” Al-Baqarah: 121

 

 

4. HATUA YA NNE

 

KUCHAGUA WAKATI NA SEHEMU MUNAASIB KWA KUHIFADHI

 

Kuweka wakati munaasib kwa kuhifadhi ni njia muhimu inayosaidia kuhifadhi. Na wakati wa kuhifadhi inatofautiana kati ya mtu na mtu kuna anayefadhilisha wakati wa Alfajiri au wakati wa Sahar (kabla ya alfajiri) au baada ya Maghrib.

 

Inapasa uchunge yafuatayo:

 

1. Kupangilia muda maalum mfano saa moja au masaa mawili muhimu udumu na muda uliojipangia usipunguze.

 

2. Kuwa na faragha kamili katika muda uliojipangia ukate mahusiano na wengine ushughulike na kuhifadhi tu bila ya kuathiriwa na chochote mfano simu makelele au sauti za juu.

 

3. Kuchagua sehemu maalum yenye utulivu na isiyokuwa na chenye kukushawiwishi mfano picha, vitabu, majarida na vinginevyo vinavyoathiri.

 

 

5. HATUA YA TANO

 

KUPANGILIA MWANZO WA HIFDHI (KUHIFADHI)

 

Kusudio je mwanzo wa kuhifadhi utakuwa mwanzo wa Mus-haf (Al-Faatihah na Al-Baqarah) au mwisho wa Mus-haf (An-Naas), na hili linatofautiana kutokana na uwezo wa mtu ikiwa mtu ana uwezo mzuri wa kusoma bora aanze mwanzo na ikiwa yupo mwanzo katika kusoma bora aanze na Surat An-Naas.

 

Natija ya wote wawili kwa Uwezo wa Allaah ni kufikia katika kuhifadhi Kitabu cha Allaah, wangapi wameanza na Surah ndogo na wamefanikiwa kufika mwisho.

 

 

6. HATUA YA SITA

 

KUWEKA IDADI YA AAYAH

 

Uwezo wa kuhifadhi ni Kipaji kutoka kwa Allaah na inatofautiana uwezo huu kati ya mtu na mtu kikubwa kinachonasihiwa mwanzo wa kuhifadhi ni kuweka idadi kamili hata kama una uwezo zaidi.

 

Kuna mtu anaweza kuhifadhi katika kikao kimoja ukurasa mzima katika Mus-haf kisha siku ya pili ameshasahau baadhi ya Aayah alizohifadhi na kuna mwengine anahifadhi kila siku Aayah tano hazidishi na inakuwa Hifdhi yake ni yenye nguvu.

 

Amepokea Abu ‘Umar Ad-Daaniy katika “Al-Bayaan” kutoka kwa ‘Uthmaan na Ibn Mas’uud na Ubay bin Ka’ab kwamba:

 

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akiwafundisha Aayah kumi hazidishi zingine mpaka wajifundishe yaliyomo na kuifanyia kazi, Anawafundisha Qur-aan na kuifanyia kazi kwa wakati mmoja.”

 

Kutoka kwa Abu ‘Abdir-Rahmaan As-Sulamiy anasema:

 

“Tulikuwa tukijifundisha Aayah kumi katika Qur-aan hatuchukui zingine baada yake mpaka tujue halali yake na haramu yake, amri yake na makatazo.”

 

Na katika kuweka idadi ya Aayah ni kutokana na kutofautiana urefu wake. Mfano tuchukulie “Aayatud-Dayn” ambayo ni Aayah ndefu kuliko zote katika hali hii inapendekezwa kuhifadhi Aayah kuendana na idadi ya mistari. Ama ikiwa Aayah ni ndogo ndogo mfano Suratul As-Swaaffaat, ‘Abasa, At-Takwiyr na zinginezo jiwekee Aayah kumi au tano katika kikao kimoja.

 

Na ukisoma Tafsiyr kuhusu maana ya maneno ni jambo litakalokusaidia katika kuhifadhi.

 

 

7. HATUA YA SABA

 

NAMNA YA KUHIFADHI AAYAH

 

Fuata hatua zifuatazo:

 

-         Pangilia idadi ya Aayah unayotakiwa kuhifadhi iwe Aayah tano mfano.

 

-         Soma Aayah mbili za mwanzo tu katika Mus-haf mara nyingi pamoja na kuzingatia sana.

 

-         Funga Mus-haf na usome Aayah mbili kwa kichwa mara nyingi.

 

-         Utakapohisi umekosea au kusahau katika neno fungua haraka Mus-haf tazama kisha funga Mus-haf.

 

-         Rudia Aayah mbili bila kutazama Kitabu mara kadhaa mpaka upate matumaini katika uliyohifadhi.

 

-         Anza kuhifadhi Aayah zilizobaki kwa njia uliyofuata katika Hifdhi ya mwanzo.

 

-         Soma kila Aayah bila kutazamia na utakapohisi kosa au umesahau fungua Mus-haf na utazame neno ulilokosea au ulilosahau.

 

-         Kariri kisomo kila Aayah mara tatu au zaidi mpaka ufike kiwango kinachohitajika.

 

-         Sikiliza Aayah hizi kutoka katika kanda ya Qur-aan pamoja na kusoma nayo.

 

 

8. HATUA YA NANE

 

KUUNGANISHA BAINA YA AAYAH

 

Kuunganisha hapa inakusudiwa baina ya Aayah ulizohifadhi na Hifdhi mpya. Aayah zinazofuatia unatakiwa kuzingatia hatua zifuatazo:

 

-         Baada ya kumaliza kuhifadhi Aayah zilizopita na kuhifadhi Aayah mpya soma kwa mkupuo mmoja.

 

-         Utakapokosea neno au kusahau usifanye haraka kufungua Mus-haf lakini jaribu kuzingatia mpaka ukumbuke.

 

-         Usipokumbuka rudia kusoma Aayah kuanzia mwanzo mpaka ufike sehemu uliyosahau.

 

-         Usipokumbuka fungua Mus-haf na utazame neno na urudie mara kadhaa kisha funga na urudie kusoma Aayah zote mara kadhaa. Na hivyo mpaka usome Aayah zote na kwa nja nzuri na Hifdhi yenye kuaminika.

 

 

9. HATUA YA TISA

 

BAADA YA KUMALIZA KUHIFADHI SURAH

 

-         Baada ya kumaliza kuhifadhi Surah kamili usihamie Surah nyingine mpaka uhakikishe unasoma vizuri uliyohifadhi mwanzo.

 

-         Soma Surah kamili ndani ya nafsi yako.

 

-         Soma kwa ndugu yako au rafiki au mwanao au watu wa nyumbani.

 

-         Sikiliza Surah kutoka katika kanda ya kaseti au CD.

 

-         Soma Surah katika Swallah za Sunnah na haswa kisimamo cha usiku (Tahajjud).

 

-         Ukifikia kiwango cha hifdhi inayohitajika mshukuru Allaah na usipofikia endelea kurejea.  

 

 

10. HATUA YA KUMI

 

KUREJEA HIFDHI ILIYOPITA     

 

-         Weka katika wiki siku moja au mbili kwa ajili ya kurejea uliyohifadhi.

 

-         Siku ya kurejea uliyohifadhi usihifadhi Aayah mpya.

 

-         Katika kurejea soma kwa kichwa na uweke Mus-haf mbele yako ili utakapohitaji ufungue kwa haraka na kufunga.

 

-         Sikiliza uliyohifadhi katika kanda ya Qur-aan bila ya kufungua Mus-haf.

 

-         Jaalia siku ya kurejea iwe thabiti isibadilike na uchague wakati maalum mfano iwe baada ya Swallah ya Magharibi ni wakati mzuri.   

 

 

 

TANBIHI MUHIMU

 

TAHADHARI NA KUPUUZIA WAKATI

 

Wakati ni umri wa mwanaadamu na maisha yake katika hii dunia nayo ni Rasilimali na biashara yake na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hivyo jiepushe na Taswiyf (Nita…) na kujishughulisha na Qur-aan na vitu vingine mfano kusema “Kesho nitahifadhi, kesho nitasoma n.k.”

 

Jihadhari pia na kuacha Hifdhi yako ya kila siku na kusema hakuna neno kesho nitahifadhi bali zingatia wakati wako na usiahirishe Hifdhi ili usije ukazoea na ukapoteza wakati wako bure. Fahamu kuhifadhi Kitabu Cha Allaah haikubaliani na kupoteza wakati na kufuata matamanio.

 

 

JIEPUSHE NA VIZUIZI (VIKWAZO)

 

Na katika hivyo ni vifuatavyo:

 

-         Nafsi ambayo inaelemea raha na inachukia kujishughulisha, kujitahidi na kukazana katika jambo.

 

-         Shaytwaan ambaye anakudanganya kwamba kazi hii (Ya kuhifadhi) inahitaji miaka mingi na wewe hutafikia lengo na kuhifadhi ni jambo zito na utasahau uliyohifadhi na anakuwekea vikwazo vingine.

 

-         Marafiki na Ndugu ambao wanakufanya uhisi kwamba umejiharamishia nafsi yako kustarehe nao katika siku yako ya kuhifadhi au wanakufanya uhisi umepitwa na mengi lakini watakuja jua mwishoni nani aliyefaulu na nani aliyepata hasara.

 

 

KUMBUKA KWAMBA…

 

-         Niyah ya kweli na Ikhlaas ni sababu muhimu ya kufaulu.

 

-         Kuwa kwako mwenye kuhifadhi Kitabu cha Mola wako inakujaalia uwe katika Watu Wake Haswa.

 

-         Qur-aan hapewi ila mwenye kufahamu kuzingatia na kuifanyia kazi yaliyomo.

 

-         Jihadhari na maasi kwani ni sababu ya kuanguka na kutofanikiwa.

 

-         Du’aa ni silaha yenye nguvu Kwani hakuna kitu kitukufu Kwa Allaah kama Du’aa.

 

 

Usitusahau katika Du’aa zako, Tunamuomba Allaah Atukubalie, Atuongoze na Du’aa yetu ya mwisho AlhamduliLlaah Rabil-‘Aalamiyn.

 

Share