Udenda Ni Najisi?

 

SWALI:

 

Je, udenda ni najisi?

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu udenda. Tulivyofahamu kwa neno ulilotumia lina maana ya mate mazito yanayomtoka mtu mdomoni na haswa anapokuwa amelala, ikiwa maana yake ni hiyo basi udenda ni twahara na hatujapata ushahidi wa kuunajisisha. Tunavyofahamu ni kwamba asili ya vitu vyote ni twahara, na kwamba havihamishwi toka kwenye asili yake ila kwa kihamisho sahihi cha kutolea hoja, kisichopingana na kile chenye kutiliwa nguvu au kuwa sawa nacho. Na ikiwa tutalipata hilo, basi ni vizuri. Na kama hatukulipata hilo, itatulazimu tusimame msimamo wa kumpinga anayedai kuwa ni najisi. Kwani kudai huku kunamaanisha kwamba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) Amewajibisha kwa waja Wake kuviosha vitu hivyo vinavyodaiwa kuwa ni najisi, na kwamba kuwepo kwake kunazuia kuswali navyo.

 

Hali hiyo ya udenda ni sawa na ya matapishi na mfano wa vitu kama hivi, hakikuthibiti kwa njia sahihi (ya kuaminika) chenye kuyahamisha toka kwenye utwahara wa asili.

 

Japo umetaka kujua kuhusu udenda lakini si vibaya kukuongezea faida kuhusu matapishi kwani vitu hivyo viwili vinakuwa kwenye maswali yanayoulizwa mara kwa mara.

 

Imepokelewa kuhusu matapiko kauli ya  'Ammaar akisema:

"Hakika utaosha nguo yako iliyoingiwa na mkojo, kinyesi, matapishi, damu na manii".

 

Lakini kauli hii ni dhaifu haitolewi hoja. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

Na imethibiti toka kwa Abu Ad-Dardaa akisema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua na akatawadha. [Abu Daawuud, na At-Tirmidhiy, Ahmad na wengineo].

 

Katika maelezo haya, hakuna kiashirio chochote juu ya unajisi wa matapishi, na wala hakuna dalili juu ya ulazima wa kutawadha akitapika mtu, na wala hayaonyeshi kuwa wudhuu unatenguka kwayo, bali lengo lake ni kusunisha mtu atawadhe anapotapika. Kwani kwa kitendo tu cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakuonyeshi kuwa ni wajibu.

 

Pamoja na hayo, si kila chenye kutengua wudhuu kinahesabiwa kuwa ni najisi. Na Ibn Hazmi amelielekea hili na akalichagua Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyah katika ‘Al-Fataawaa’.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share