Amepatiwa Kazi Na Aliye Na Mahusiano Yasiyo Halaal Na Dada Yake- Je Kazi Hiyo Ni Halaal Kwake?

SWALI:

 

Asalam alaikum warahmatullahi wabarakatu sheikh nauliza mnisaidie naomba mnijibu haraka kwa kuwa kazi yenyewe nimeambiwa kuanza baada ya wiki ni hivi dada yangu alikuwa na mpenzi wake ambae ni kinyume na dini yetu tukufu sasa dada yangu alishasafiri siku nyingi takriban miaka mitatu sasa nimekutana na yule mpenzi wake nimemuomba anitafutie kazi amekubali na ameshanipatia kazi je? Kazi hiyo itakuwa halali kwangu? Au haram naomba nijibiwe upesi ili nisijekuanza

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutafuta na kupata kazi.

Kazi ni njia nzuri ya Muislamu kutafuta na kufanya. Na sharti ya kazi ambayo Muislamu anafaa afanye ni ile ambayo ni halali kisheria.

 

Mapenzi ambayo huyo bwana anafanya na dada yako ni makosa na madhambi watapata wao. Lako ni kujaribu kuzungumza na dada yako aache dhambi hilo kwani zinaa ni miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu. Kwa hivyo, ikiwa kazi ambayo utamfanyia ni ya halali hakuna ubaya wowote wako kufanya ili upate ajira.

 

Makosa aliyofanya dada yako na huyu bwana ni tofauti na kazi ya halali utakayomfanyia upate chumo la halali. Lakini pia kumbuka kuwa kumfuata mtu kama huyo mwenye kushiriki haraam na dada yako, ni kumpa nguvu ya kuendeleza maasi yake na pia wewe kujiduniza zaidi kwake na kuonesha kuridhia kwako na mahusiano yao ya haraam hadi kumfuata yeye akusaidie ilihali ndiye anayemuharibu dada yako. Lazima wewe uwe ni mtu mwenye msimamo, na suala hilo hata asiyeshikamana na Dini hatoweza kulikubali kuona mtu anacheza na dada yake. Na ikiwa ushaanza kazi kwake au kwa njia yake, basi unaloweza kufanya ni kumpa nasaha huyo bwana aache maasi yao na mfahamishe madhara yake na madhambi makubwa yanayopatikana katika mahusiano hayo yao na mtake arejee kwa Mola wake na afanye toba. Na hilo laweza kufanikiwa zaidi ikiwa wewe ni mtu wa msimamo na unatekeleza mafundisho ya Dini yako, lakini ikiwa wewe mwenyewe huna mwelekeo na ni mtu ovyo ovyo kama wao, basi ujue hakuna taathira yoyote itakayopatikana.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share