Vipi Kuepukana Na Kuikabili Mitihani

 

Vipi Kuepukana Na Kuikabili Mitihani

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaikum, mimi nawa andikia nikiwa mgeni katika dini hiyi ya ALLAAH ninayo mswali ambayo ningelipenda kujua majibu yake kwani yatachangia kuniweka sawa na kuifuata vyema dini ya ALLAAH

 

Mja Anapokabiliwa  Na  Mitihani Jee  Afanye Nini Ku Ipuka Mitihani Hiyo?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani kwa ndugu yetu aliyeuliza swali hili zuri hasa katika enzi hizi ambazo mitihani kwa Muislamu ni kitu cha kawaida. Ni lazima tufahamu kuwa mitihani ni lazima imfikie Muumini akiwa katika dunia hii, kwani dunia ni jela kwa Muumini. Katika jela yoyote ipo mitihani mingi ambayo mwanadamu kwa ujumla anakumbwa nayo na hivyo anafaa avumilie. Daraja ya Imani yake ni kwa kupita mitihani ambayo itamfikia kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa). Muislamu hafai kuomba afikwe na mitihani kama vile hafai kuomba kukutana na adui. Ni hakika kuwa katika vita huwa mtu anayeshiriki ana mtihani mkubwa; je, ataweza kusimama imara au atakimbia? Ikiwa atasimama imara basi atakuwa amefaulu lakini akikimbia atakuwa amefeli kwani kukimbia katika uwanja wa vita ni miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم ۖ مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ ۗ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ ﴿٢١٤﴾

Je, mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali bado haijakufikieni (mitihani) kama ya wale waliopita kabla yenu? Iliwagusa dhiki za umasikini na maafa ya magonjwa na njaa na wakatetemeshwa mpaka Rasuli na wale walioamini pamoja naye wanasema: Lini itafika nusura ya Allaah? Tanabahi! Hakika nusura ya Allaah iko karibu. [Al-Baqarah: 214].

 

Na Anasema:

 أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾

Je, Mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali Allaah Hakudhihirisha wale waliofanya jihaad miongoni mwenu na Akadhihirisha wenye kusubiri? [Aal 'Imraan: 142].

 

Pia:

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾

Je, wanadhani watu kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao ndio wasijaribiwe? Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao, ili Allaah Awatambulishe wale walio wakweli na ili Awatambulishe walio waongo. [Al-Ankabuwt: 2 – 3].

 

Katika walio kumbwa na mitihani mizito ni Manabii kisha wafuasi wao na walio chini yao katika Imani. Kila unapokumbwa na mitihani basi Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anakupenda.

 

Kwa kuwa mitihani haina budi kumkabili Muislamu, swali muhimu ambalo inafaa sisi tujiulize na tuweze kufahamu ni je tutaikabili vipi mitihani hiyo? Mitihani inaweza kukabiliwa tu kwa njia sahihi alizotufundisha Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Bila ya kufanya hivyo basi tutakuwa tunafanya kazi ya bure. Miongoni mwa maandalizi ni:

 

1.   Kujitahidi katika Ibaadah kama Swaalah kwa wakati wake pamoja na kutekeleza nguzo zake, Swawm, Zakah, Hijjah, kumdhukuru Allaah. Mbali na zile Ibaadah za faradhi inafaa pia tujitahidi katika Sunnah za Ibaadah hizo. Mfano funga ya Jumatatu, Alkhamisi na kadhalika, Swaalah za Sunnah za qabliyah na baadiyah. Kuhusu Swaalah tunapata katika Qur-aan 2: 45, Funga 2: 183.

 

2.   Kusoma Qur-aan kwa kuzingatia maana yake na kufanya juhudi katika kutekeleza amri zake.

 

 

3.   Kumtii Allaah na Rasuli Wake (Qur-aan 4: 13).

 

4.   Kusuburi na kuwa mvumilivu. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45].

 

5. Kumtegemea Allaah Aliyetukuka katika mambo yako. Huko ni kuamini kuwa hakuna linaloweza kukukumba isipokuwa kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka. Imani hiyo itakufanya usitingishike na lolote hapa duniani. Hakuna anayeweza kukubabaisha. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpatia nasaha Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) na hivyo kutupatia sisi pia pale alipomwambia:

 

"…Ukimuomba muombe Allaah; ukitaka msaada taka kwa Allaah. Na ujue ya kwamba hakika lau watu wakusanyike ili wakunufaishe wewe kwa jambo lolote, hawawezi kukunufaisha ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah; na wakikusanyika ili kukudhuru kwa jambo lolote, hawawezi kukudhuru ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah. Kalamu zimeinuliwa na kurasa zimekauka…" [At-Tirmidhiy]

 

6.  Kuamini Qadari (mipango) ya Allaah.

  

7.  Imani ya kuwa siku moja utasimama mbele ya Allaah na Atakuhukumu kwa uadilifu. Kwa mema zawadi yako ni Pepo na kwa maovu ni Moto.

 

8.  Kusoma visa vya Rusuli na watu wema na mitihani waliyokumbana nao na jinsi walivyoweza kufaulu.

 

9.  Soma mada zenye kichwa cha habari 'Usihuzunike' ambazo ziko katika 'Nasiha Za Ijumaa' humu AL HIDAAYA kwenye viungo vifuatavyo:

 

Mada hizi zimetaja fadhila za kusubiri katika mitihani na pia zinamburudisha kila mwenye kukumbwa na mitihani na taabu ya aina yoyote.

 

Usihuzunike! Baada Ya Dhiki Faraja

Usihuzunike! Unaposubiri Mitihani Ya Mola Wako Ni Kheri Kwako

Usihuzunike! Subira Katika Mitihani Ina Malipo Mema

USIHUZUNIKE! Kwa Mambo Yasiyostahiki Ya Dunia Bali Huzunika Na Mambo Ya Akhera

USIHUZUNIKE! Na Maudhi Ya Dunia, Kuwa Na Taqwa Ikufae Akhera

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share