Mama Wa Waumini Khadiyjah (رضي الله عنها)

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

Nasaba Yake

Anaolewa na Atiyq bin Aidh

Anaolewa na Abu Halah

Hakupata kulisujudia sanamu

Anamuajiri Muhammad

Rudi naye Makka haraka sana

Sifa za aliyetakaswa

Lakini umri wangu mkubwa

Anaolewa na Muhammad

Kuzaliwa kwa Qassim

Sikubali kuachana naye

Aliy (Radhiya Llahu anhu)

Anakwenda Ghaari Hiraa

Zammiluni zammiluni

Mpe Khadija salamu

Kufariki kwa Bibi Khadija

Baadhi ya sifa zake

Mafunzo 

 

Nasaba yake

Jina lake ni Khadija binti Khuwaylid bin Asad bin Abdul Uzza Qusay bin Kilab anayetokana na kabila la Kikureshi aliyezaliwa katika mwaka wa 68 kabla ya Hijra yaani mwaka 556 baada ya Nabii Issa (Alayhis Salaam).

Wazee wake walimlea kwa heshima na adabu ya hali ya juu na alikuwa akijulikana kwa jina la ‘Aliyetakasika’ hata kabla ya kuja kwa Uislamu.

Anaolewa na Atiyq bin Aidh

Imepokelewa kuwa siku moja vijana wa kabila la Kikureshi walipokuwa wamekaa karibu na Al Kaaba wakizungumza, aliinuka mmoja wao anayeitwa Al Harith akasema:

“Enyi ndugu zangu nimetia nia ya kuowa”.

Mmojawao akamwambia:

“Uamuzi mzuri huo, kwani tokea alipofariki mama yako na baada ya baba yako kuowa mke mwingine umekuwa unaishi peke yako”.

Mwengine akasema:

“Umefanya vizuri kuamua kuoa, kwani kila mwanamke anatamani kuolewa na mtu kama wewe, maana baba yako ni katika watu wanaoheshimika katika kabila la Kikureshi, na wewe unamiliki mali nyingi sana, sidhani kama yupo mwanamke atakayekukataa”.

Al Harith Akawatizama wenzake kwa muda, kisha akasema:

“Nyinyi mnadhania hivyo kwa sababu ni rafiki zangu, lakini mnakosea”.

“Tunakosea vipi?  Hebu tufahamishe”.

Akawaambia:

“Nilitaka kumuowa Khadija, lakini baba yake alinikatalia kwa sababu eti anasema kuwa kabila langu ni duni kuliko kabila lake”.

Wenzake wakasema:

“Bila shaka hiyo, kwani Khadija ni binti wa Khuwaylid bin Asad naye ni mtu mtukufu miongoni mwa mabwana wa kabila la Kikureshi mwenye kumiliki mali nyingi sana na nyumba kubwa ambayo daima inapokea wageni mbali mbali wanaokuja Makka”.

Mwengine akasema:

“Na Khadija binti yake ni uwa katika mauwa ya Makka, kwani yeye ni mzuri wa umbo na mbora wa mwenendo na tabia, na sifa zake njema pamoja na hekima na uhodari wa kuyapima mambo katika akili yake, vyote hivyo vinajulikana na kila mtu”.

Walipokuwa katika hali ile alipita mbele yao mtu mrefu, mwingi wa haiba aliyevaa nguo zilizoshonwa vizuri na kupambwa, pamoja na kilemba, na nyuma yake kundi la watu lilikuwa likimfuata.

Watu wote walinyamaza kimya huku wakimtazama mtu huyo alipokuwa akipita, kisha mmoja wao akasema kwa sauti ndogo hafifu:

“Huyu ndiye Khuwaylid baba yake Khadija, na walio nyuma yake ni watu wa kabila lake”.

Mwengine akasema:

“Amekuja kutufu Al Kaaba kama kawaida yake ya kila siku”.

Baada ya kutufu Al Kaaba, Khuwaylid akatafuta mahala karibu na Al Kaaba ili aweze kukaa na kujipumzisha, na alipokuwa katika hali ile, kijana mmoja aliiunuka na kwenda kumkabili.

Kijana huyo alikuwa mwenye sura na umbile la kupendeza ambaye kutokana na vazi lake alionyesha kuwa ni mtu tajiri sana, na nyuma yake pia kundi la watu lilikuwa  likimfuata kwa heshima na adabu.

Mtu huyo alikuwa ni Atiq bin Aidh, mmoja katika watu wanaoheshimika miongoni mwa matajiri wakubwa wa kabila la Kikureshi.anayetokana na kabila la Bani Makhzum.

Mmoja katika wale vijana akasema:

“Mtizameni vizuri! Mtu huyu anapigiwa mifano katika ushujaa na ukarimu”.

Baada ya kumkabili Khuwaylid bin Asad, Atiq akamwambia:

“Asubuhi njema ewe Khuwaylid”.

Khuwaylid akamjibu:

“Njema kwako pia ewe Atiq”.

Atiq:

“Nimekuja kwa ajili ya mazungumzo na wewe ewe mwana wa ami yangu, lakini mazungumzo yenyewe hayafai kuzungumzwa hapa penye Al Kaaba mbele ya watu”.

Khuwaylid akamwambia:

“Karibu nyumbani kwangu”.

Siku ya pili yake Atiq akamwendea nyumbani kwake na kumwambia:

“Nimekuja kumposa binti yako ewe bin ami yangu”.

Khuwaylid akamuuliza:

“Umekuja kumposa Khadija au Hala?”

“Bali nimekuja kumposa Khadija ewe bin ami yangu”.

“Vyema, lakini itabidi kwanza nimuulize Khadija mwenyewe ili nijuwe rai yake."

Atiq akasema kwa mshangao:

“Lakini wewe ni baba yake na unanijuwa mimi vizuri na unaijuwa daraja yangu katika kabila la Kikureshi pamoja na mwenendo na tabia zangu”.

Khuwaylid akamjibu:

“Bila shaka ewe bin ami yangu natambuwa yote hayo, natambua vizuri pia kuwa anakustahikia mwanamke yeyote wa Kikureshi, isipokuwa mimi siwezi kuamua lolote juu ya Khadija mpaka kwanza nimuulize mwenyewe na aridhike.”

Atiq akaondoka huku akisema kumwambia Khuwaylid:

“Vyema, fanya hivyo na mimi nitasubiri”.

Baada ya Atiq kuondoka, Khuwaylid akaingia kwa binti yake Khadija na kumjulisha juu ya Atiq, akamwambia:

“Ewe Khadija, kwa hakika Atiq amekuja kukuposa, nini rai yako?”

Khadija akasema kumwambia babake:

“Nini rai yako wewe kwanza ewe baba yangu?”

Baba yake akamwambia:

“Yeye ni bwana katika mabwana wa Kabila la Bani Makhzum na ana mali nyingi sana”.

Bibi Khadija akasema:

“Baba yangu, mimi sikuulizi juu ya sifa hizo, bali nataka kujuwa juu ya sifa zake nyingine kama vile ushujaa na ukarimu na kwamba hawafanyii ubakhili wenye kuhitaji wanapomwendea.”

Baba yake akamwambia:

“Atiq bin Aaidh yuko kama ulivyosema ewe Khadija. Yeye ni shujaa, mkarimu anayependa wageni. Hakika sifa zote unazozitafuta anazo mwanamume huyu”.

Bibi Khadija akasema:

“Basi, ikiwa ni hivyo fanya vile unavyoona wewe kuwa ni sawa ewe baba yangu”.

Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akaolewa na Atiq wakapata mtoto waliyempa jina la Hind, na wakaishi kwa wema mpaka alipofariki mumewe jambo lililomfanya Bi Khadija awe na huzuni kubwa.

Anaolewa na Abu Halah

Haukupita muda mrefu bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akaolewa na Nibash bin Zirarah Al Tamimi aliyekuja kujulikana kwa jina la ‘Abu Halah”,  na wakapata watoto wawili waliowapa majina ya Hind na Halah. Waliishi kwa wema mpaka mumewe wa pili naye pia alipofariki dunia, na haukupita muda mrefu baba yake Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) naye pia akafariki dunia, jambo lililozidisha huzuni moyoni mwake. (zipo riwaya zinazosema kuwa baba yake bi Khadija alifariki dunia baada ya binti yake kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba yeye ndiye aliyeifunga ndoa yao. Hata hivyo riwaya zenye nguvu zaidi zinasema kuwa alifariki kabla ya bibi Khadija kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba aliyefunga ndoa ya bibi Khadija na Mtume (Swalla Laahu alayhi wa sallam)alikuwa kaka yake anayeitwa Amru bin Khuwaylid.

 

Baada ya misiba hiyo iliyofuatiliana, Bibi Khadija aliyerithi mali nyingi sana kutoka kwa baba yake na kutoka kwa waume zake waliofariki, aliamua kujitenga na watu akawa anajishughulisha na ulezi wa wanawe.

Watu wengi walipeleka posa kutaka kumuoa, lakini Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliwakataa kwa sababu alihisi kuwa wote hao walikuwa wakimtaka kwa ajili ya tamaa ya mali yake na uzuri wake.

Hakupata kulisujudia sanamu

Baada ya kupatwa na misiba miwili hiyo, (kufiwa na mumewe wa pili na kufiwa na baba yake) Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliishi akiwa mwingi wa huzuni na mwingi wa kutafakari. alijitenga mbali na watu na aliacha hata kwenda kutufu Al Kaaba kama alivyokuwa akifanya hapo mwanzo.

Inajulikana kuwa Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu yaliyokuwepo hapo, na hii ni siri aliyomjulisha bin ami yake maarufu Waraqah bin Noufel aliyekuwa akifuata dini ya Manasara.

Waraqah bin Noufel huyu alikuwa mcha Mungu sana na alikuwa akisoma sana vitabu vilivyotangulia na kwa ajili hiyo alikuwa akijulikana sana miongoni mwa waarabu wa Makka kwa ucha Mungu wake na wema wake.

 

Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akiwa na uso uliojaa huzuni alikwenda kumtembelea bin ami yake huyo aliyemuuliza:

“Kuna nini binti ami yangu, mbona nakuona una huzuni nyingi?”

Bibi Khadija akamwambia:

“Sijaiona tena furaha tokea alipofariki baba yangu, na mali nyingi niliyoirithi haikuweza kuziba pengo lake”.

Waraqah akamwambia:

“Usihuzunike ewe binti ami yangu, utakuja kuonana naye Akhera”.

Bibi Khadija akashangaa:

“Akhera? Ni kitu gani hicho kinachoitwa akhera ewe bin ami yangu?”

Waraqah:

“Hayo ni maisha baada ya kifo, na katika maisha hayo kila nafsi itapata jaza yake kutokana na yale yaliyotanguliza mikono yake”.

Bibi Khadija akauliza huku akitetemeka:

“Ina maana kuwa baba yangu hivi sasa yuhai?”

Waraqah akamwambia:

“Ndiyo, roho yake iko hai, isipokuwa mwili wake ushachanganyika na udongo wa ardhi”.

Bibi Khadija akaanza kusema huku mwili wake ukiwa unamtetemeka:

“Bin ami yangu, nataka kukupa siri niliyoizuwia moyoni mwangu tokea nilipokuwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka sita”.

Waraqah akasema:

“Sema ewe binti ami yangu wala usiwe na khofu”.

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akasema:

“Nilipokuwa na umri wa miaka sita hivi, nilikwenda siku moja pamoja na baba yangu penye Al Kaaba nikamuona akisimama mbele ya masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe kisha anayakabili na kukiinamisha kichwa chake kwa kuyaheshimu. Nikamuuliza:

“Nini haya masanamu ewe baba yangu?”

Akaniambia:

“Hii ni miungu tunayoiabudu”.

Nikashangazwa nikiwa bado mdogo, vipi watu wanayaabudu mawe yasiyoweza kudhuru wala kunufaisha?”

Waraqah akamtizama Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) huku akitabasamu, kisha akamwambia:

“Uliwahi kumhadithia mtu yeyote katika watu wa nyumbani?”

Bibi Khadija akasema:

“Abadan, abadan. Sijapata kumhadithia mtu yeyote, kwani nilikuwa nikiogopa sana, nikaificha siri hii mpaka nilipokuja kukuhadithia wewe sasa hivi. Nini rai yako ewe bin ami yangu?”

Waraqah akamwambia:

“Huo ndio ukweli wenyewe. Yale ni mawe tu yasiyodhuru wala kunufaisha. Na atatokea katika zama zetu hizi Mtume anayesubiriwa atakayeyavunja masanamu haya na kuondoa ushirikina na uonevu katika ardhi”.

Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akauliza:

“Na lini atakuja Mtume huyo?”

Waraqah akasema:

“Mwenyezi Mungu ndiye Anayejuwa zaidi, isipokuwa vitabu vinasema kuwa; atatokea Mtume katika wakati huu wetu na yeye ndiye atakayekuwa mwisho wa mitume”.

Bibi Khadija akauliza:

“Na katika kundi lipi atatokea mtume huyo?”

Waraqah akasema:

“Allahu aalam, lakini Mayahudi wanasema kuwa atakuwa katika wao, na vitabu vinasema kuwa atakuwa miongoni mwa Waarabu”.

Bibi Khadija:

“Na uliyajuaje yote haya ewe bin ami yangu?”

Waraqah:

“Haya yameandikwa katika Tuarati kitabu cha Mayahudi na katika Injili kitabu cha Manasara”.

Bibi Khadija akaondoka hapo huku mawazo yake yote yakiwa juu ya huyo Mtume mpya aliyebashiriwa na bin ami yake atakayeuondoa ushirikina na dhulma na jeuri iliyopindukia mipaka, lakini wakati huo huo mazungumzo hayo yalimsaidia sana katika kupunguza uzito uliokuwepo kifuani pake na huzuni aliyokuwa nayo, na kwa ajili hiyo akaanza tena kufanya shughuli zake za kawaida pamoja na za kibiashara.

Anamuajiri Muhammad

Katika shughuli zake za kibiashara bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) alikuwa akiwaajiri wanaume wawili kila mwaka. Mmoja kwa ajili ya kwenda Sham wakati wa Kusi na mwengine kwa ajili ya kwenda Yemen wakati wa Kaskazi. Na hivi ndivyo yalivyokuwa maisha ya kibiashara Bara ya Arabu yote.

Wakati huo huo Muhammad bin Abdillah (Swalla Laahu alayhi wa sallam) (kabla ya kupewa utume) alikuwa akiishi pamoja na ami yake Abu Talib baada ya kufariki kwa babu yake Abdul Muttalib, na alikuwa akimsaidia ami yake katika shughuli za kibiashara na katika kuchunga kondoo na mbuzi mpaka alipofikia umri wa miaka ishirini na mitano, na kutokana na  uaminifu wake na ukweli wake, watu wa Makka walikuwa wakimuheshimu sana.

Hii ukijumuisha pia kuwa Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu waliyokuwa wakiyaabudu na kuyaogopa wala hakupata kunywa pombe, na hakuwa akijishughulisha na anasa wala starehe ya aina yoyote ile katika starehe walizokuwa wakijishughulisha nazo vijana wa wakati ule.

Alikuwa mwema, msema kweli, muaminifu, mwenye tabia na mwenendo mwema uliompendeza kila mtu, na alikuwa na haiba kubwa sana pale Makka hata akawa maarufu miongoni mwao kwa jina la ‘Al Swaadiqul Amin’, bimaana Mkweli Mwaminifu.au ‘Muhammad Al Amin’, na maana yake ni Muhammad muaminifu.

 

Sifa zote hizo zilikuwa zikimfikia bibi Khadija aliyekuwa mfanya biashara maarufu pale Makka pamoja na sifa nyingine mbali mbali, na pia zilikuwa zikimfikia habari za kusafiri kwake pamoja na ami yake Abu Talib katika shughuli za kibiashara kwenda nchi ya Sham, na kwamba ami yake alikuwa akipata faida kubwa sana tokea alipoanza kushirikiana naye katika shughuli hizo.

Habari hizo zikawa zinamshughulisha sana bibi Khadija na usiku mmoja katika siku za joto alipokuwa amekaa juu ya dari la nyumba yake pamoja na mwanamke mmoja aitwae Nafisa binti Munabih, bibi Khadija alikuwa akitazama chini sana huku akitafakari, jambo lililomfanya Nafisa amuulize:

“Unatafakari juu ya nini ewe Khadija?”

Bi Khadija:

“Natafakari juu ya jambo la ajabu sana”.

Bi Nafisa:

“Unanificha mimi?”

Bi Khadija:

“Mimi siwezi kukuficha kitu ewe Nafisa, jambo lenyewe linahusiana na Muhammad bin Abdillah!”.

Bi Nafisa:

“Ah! Muhammad Muaminifu. Unataka nini kwake?”

Bi Khadija:

“Muhammad Muaminifu husafiri baadhi ya wakati kwa ajili ya shughuli za kibiashara pamoja na ami yake Abu Talib, ningefurahi kama angekubali pia kushughulikia biashara zangu maana yeye ni mtu wa pekee ninayeweza kumuaminisha katika mali yangu. Lakini sijuwi vipi nitaweza kumjulisha?”

Nafisa:

“Mimi, mimi ndiye nitakayemjulisha ewe Khadija, lakini nitazungumza na ami yake Abu Talib maana naona haya kumkabili Muhammad juu ya jambo hili.”

Abu Talib akalikubali ombi hilo na akamnasihi Muhammad akubali pia, na Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akamwambia ami yake:

“Ikiwa wewe unaona sawa, basi na mimi nimekubali”.

Bibi Khadija alifurahi sana alipojulishwa kuwa Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) amelikubali ombi lake, akatayarisha msafara wa biashara na kumtaka mtumishi wake Maysara afuatane na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) kwa ajili ya kumhudumia na kumshughulikia katika safari ndefu hiyo.

Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akafanikiwa kuuza bidhaa zote za bibi Khadija katika masoko ya Sham na akarudi akiwa amempatia faida kubwa sana kuliko alivyowahi kupata miaka yote iliyopita.

Rudi naye Makka haraka sana

Tokea waliporudi kutoka safari ya Sham yule kijana Maisara aliyevutiwa sana na tabia na mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alouona walipokuwa safarini, akawa anamuhadithia bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) juu ya yale aliyokuwa akiyaona safarini walipokuwa wakienda na walipokuwa wakirudi na baadhi ya miujiza iliyokuwa ikitokea.

Bibi Khadija naye aliyekuwa wakati wake wote anawaza juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kila mara kuhadithiwa juu ya sifa zake hizo, na siku moja alipokuwa amekaa pamoja na mtumishi wake huyo, akamwambia:

“Enhe! Hebu nihadithie vizuri juu ya safari yako na Muhammad”.

Maisarah akasema:

“Sikupata kuona mtu bora wa kusafiri naye kuliko yeye. Alikuwa mtulivu, hana kiburi, mkarimu na mpole sana. Nilikuwa ninapoumwa ananishughulikia na ninapochoka ananisaidia, na alikuwa akigawana na mimi sawa sawa chakula chake na maji yake. Kwa hakika alikuwa akinitendea kama kwamba ni ndugu yake.

Lakini jambo lililonistaajabisha zaidi ewe bi Khadija,” akaendelea kusema: “kulikuwa na kiwingu kilichokuwa kikimfuata wakati wote tokea tulipoondoka mpaka tuliporudi. Kilikuwa kikimfuata na kumkinga na juwa kali wala hakuwa akihisi joto hata kidogo wakati wote wa safari.

Isitoshe, Muhammad hapendi kusema sana, na kila tunaposimama kwa ajili ya kupumzika alikuwa akijitenga peke yake na alikuwa akipenda kutizama mbinguni kwa khushuu na mdomo wake ulikuwa daima ukitikisika huku akisema maneno yasiyosikika”.

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa na shauku ya kutaka kujuwa zaidi habari za Muhammad akasema:

“Enhe! Kisha? Endelea, nini kilichotokea baadaye?”

Maisarah akasema:

“Tulipokuwa tukirudi Makka, tulisimama mahali muda mdogo kwa ajili ya kujipumzisha, na mimi nikaondoka kwenda kutafuta chakula cha ngamia, na mahali hapo palikuwa na mti mkubwa sana na Muhammad alikaa chini ya mti huo huku akitizama mbinguni kama kawaida yake kama kwamba anatafuta kitu, na karibu na mahali hapo palikuwa na hekalu la mcha Mungu mmoja aitwae Nastwur aliyenijia mimi na kuniuliza:

“Nani huyu kijana aliyekaa chini ya mti ule?”

Nikamwambia;

“Huyu ni kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kikureshi”.

Akaniambia:

“Umeona lolote lisilo la kawaida kutoka kwake?”

Nikamwambia:

“Nimeona kiwingu kikimfuata kikimkinga kutokana na jua kali tokea tulipoondoka na wala hakikumuacha abadan”.

Akauliza tena:

“Macho yake yakoje?”

Nikamjibu:

“Meusi na makubwa na katika weupe wake umo wekundu khafifu ndani yake”.

Akasema:

“Kijana huyu atakuwa na shani kubwa, rudi naye Makka haraka sana, kwani hakupata kukaa chini ya mti huu isipokuwa Nabii”.

Maneno haya yalimtia kizunguzungu bibi Khadija na tokea alipoondoka hapo akawa usiku na mchana hana analowaza isipokuwa juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).

Sifa za aliyetakaswa

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akaanza kufikiri huku akikumbuka na kuunganisha maneno ya Maisarah na maneno aliyoambiwa na bin ami yake Waraqah bin Noufel, akawa anajisemesha:

“Kwa nini isinipitikie wakati wote huu? Huyu ndiye kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kikureshi anayejulikana kwa ukweli na uaminifu na upole na ukarimu, na Makureshi wote wanamuheshimu na kumtukuza kutokana na kujitenga kwake mbali na tabia zote mbaya walizokuwa nazo vijana wa kabila la Kikureshi na wengineo.

Na huyu ndiye kijana aliyesafiri na mali yangu na kunipatia faida kubwa sana, na huyu ndiye kijana ambaye kiwingu kilikuwa kikimkinga kutokana na juwa kali tokea alipoianza safari yake mpaka aliporudi. Na huyu ndiye kijana ambaye mcha Mungu Nastwur amesema juu yake kuwa atakuwa na shani kubwa akamtaka Maisarah arudi naye Makka haraka sana”.

Bibi Khadija akawa anawaza na kukumbuka yote hayo mpaka akawa na uhakika ndani ya moyo wake kuwa sifa kama hizi haziwezi kumuandama mtu wa kawaida.

Sifa njema kama hizi ambazo si kila mtu anaweza kuwa nazo hazipatikani isipokuwa kwa watu waliochaguliwa na kutakaswa.

Kutokana na yote haya, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akazidi kujishughulisha na kuwaza juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).

Lakini umri wangu mkubwa

Baada ya kuwaza na kufikiri muda mrefu, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akafikia uamuzi wa kutaka kuolewa na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).

“Kwa nini nisimtake Muhammad aniowe? Inagawaje fikra hii ni mfano wa ndoto, lakini ni jambo linalowezekana. Lakini vipi? Nani atakayekubali kunifikishia ombi langu?”

Alipokuwa katika hali ile, mlango ukagongwa.

“Nani anayegonga mlango?”

“Mimi dada yako Halah.”

Bibi Khadija akamkaribisha dada yake.

“Ahlan wa sahlan, karibu ewe Halah”

Halah:

“Ahsante Khadija vipi hali zenu?”

Khadija:

“Hatujambo, ziara hii ya ghafla naona.”

Khadija:

“Bila shaka ewe dada yangu, kwani nimekuja kukujulia hali yako tu”.

Khadija:

“Kuijua hali yangu tu! Mbona unasema maneno ya kiajabu, au kuna jambo unataka kunificha?”

Halah akamtizama dada yake mtizamo wa kuchunguza, kisha akamwambia:

“Abadan, hakuna la kukuficha isipokuwa mchana wa leo ulinichukuwa usingizi nikakuota unatembea mfano wa mtu aliyepotea katika njia ya kiza na nyuma yako sauti inakwambia: “Nenda mbele, nenda mbele”. Nikaona bora nije kukujulia hali yako, ingawaje sijuwi ndoto hiyo tafsiri yake nini”.

Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akatabasamu kidogo kisha akasema:

“Kusema kweli mimi siku hizi ninaishi ndani ya mawazo mengi sana.”

Halah:

“Unawaza juu ya nini na wewe upo katika neema kubwa kama hii?”

Khadija:

“Muhammad, ewe dada yangu. Nafikiri juu ya sifa zake na utukufu wake ambao hajapata kuufikia hata mmoja katika watu wa kabila la Kikureshi.”

Halah:

“Na nini mwisho wa fikra hizo?”

Khadija:

“Nataka aniowe”.

Halah:

“Basi muombe akuowe”.

Bibi Khadija akamjibu kwa uoga:

“Naogopa asije akanikataa, kwani yeye ni kijana anayeheshimika kupita vijana wote”

Halah:

“Na wewe pia dada yangu ni mtu mtukufu unayeheshimika na watu wote”.

Khadija:

“Lakini umri wangu mkubwa unaokaribia miaka arubaini, na nishaolewa mara mbili, wakati yeye bado ni kijana mwenye umri wa miaka ishirini na mitano na bado hajapata kuowa. Vipi Muhammad atakubali kumuowa mwanamke aliye na umri sawa na mama yake aliyekwisha olewa mara mbili na ana watoto?”

Halah akasema:

“Nani aliyekujulisha na Muhammad mara ya mwanzo hata ukaweza kumpa mali yako aifanyie biashara?”

Khadija:

“Rafiki yangu mmoja anayeitwa Nafisa”.

Halah:

“Basi Nafisa huyo huyo ndiye atakayeweza kukufikishia ombi lako hilo”.

Kisha Halah akamuaga dada yake na kuondoka

Anaolewa na Muhammad

Ziara ya Hala ilikuwa mfano wa ufunguo wa kheri katika nafsi ya bibi Khadija (Radhiya Llahu anha), kwani siku ya pili yake Nafisa alipokuja kumtembelea bibi Khadija, akamhadithia juu ya mazungumzo yaliyopita baina yake na baina ya dada yake Halah, na Nafisa akakubali kuchukuwa jukumu la kulifikisha ombi hilo kwa Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Alipoondoka, Nafisa alielekea moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Talib alipokuwa akiishi Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na alipomuona akamwambia:

“Ewe Muhammad, wewe una umri wa miaka ishirini na tano na mpaka sasa bado hujaowa.”

Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akashangazwa sana na maneno hayo, akamuuliza:

“Kipi kilichokufanya ujishughulishe na jambo hili ewe Nafisa?”

Nafisa:

“Bibi anayeheshimika anataka umuowe, nini rai yako?”

Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

“Bibi gani huyo?”

Nafisa:

“Bibi huyo ni Khadija binti Khuwaylid, na wewe unamuelewa vizuri juu ya heshima yake na utukufu wake na sifa zake zote njema”.

Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:

“Naam, hakika yeye ni mtu anayeheshimika, lakini mimi sina mali hata niweze kumuowa.”

Nafisa;

“Yeye hana haja ya mahari, kwani unajuwa vizuri kuwa yeye hana shida ya mali na anao utajiri mkubwa”.

Muhammad:

“Mimi utajiri haunishughulishi, kwani mali inakuja na kuondoka, na Khadija pia ni mwanamke mzuri wa umbo na tabia na mwenendo, lakini niache nimshauri ami yangu kwanza juu ya jambo hili”.

Ami yake akamwambia:

“Ewe Muhammad, hii ni bahati iliyokujia kutoka mbinguni. Naapa kuwa Khadija ni mwanamke aliyetakasika kupita wote katika Makka na mwenye akili na uwezo wa kupima mambo kupita wote, na mwenye hekima kupita wote na anayetokana na ukoo bora kupita wote. Wangapi wenye mali na jaha walitaka kumuoa akawakataa, na leo anakutaka wewe wakati huna mali yoyote, hii ni bahati kubwa.

Kubali ewe mwana wa ndugu yangu, kwani asingekutaka isipokuwa amekuwekea heshima kubwa sana”.

Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akakubali, na bibi Khadija akafanya arusi kubwa sana iliyohudhuriwa na watu wengi, na wanyama wengi sana wakachinjwa siku hiyo na kila muhitaji alifaidika.

Kuzaliwa kwa Qassim

Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) alizaa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) watoto sita. Wanaume wawili na wanawake wanne. Watoto wa kiume aliwapa majina ya Qassim na Abdullah, aliyekuwa akijulikana pia kwa jina la Al Taher. Na watoto wa kike ni Ruqayyah na Zeinab na Ummu Kulthum na Fatima (Radhiya Llahuu anhunna).

 

Katika mwaka wao wa mwanzo tokea kuoana walijaaliwa kupata mtoto wa kiume waliyempa jina la Qassim, wakafurahi sana, na kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawa anajulikana kwa jina la ‘Abal Qassim’, na maana yake ni 'baba yake Qassim'.

Lakini Qassim hakuishi muda mrefu, kwani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka miwili, na wazee wake walihuzunika sana, lakini walisubiri na kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Kisha akazaliwa Abdullah aliyefariki pia akiwa mtoto mchanga, kisha Zeinab, kisha Ruqayah aliyefanana na mama yake, kisha akazaliwa Ummu Kulthum, kisha akazaliwa Fatima aliyefanana sana na baba yake hasa katika mwendo na sauti.

Sikubali kuachana naye

Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) aliingia nyumbani akiwa amemshika mkono mtoto mdogo, akamkabili Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kumwambia:

“Mtoto huyu nakupa zawadi, mchukuwe, atakusaidia na kukuhudumia”.

Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamtizama mtoto yule machoni akaona dalili ya hekima ndani yake, akamuuliza:

“Jina lako nani na ilikuwaje ukatekwa?”

Mtoto akajibu:

“Jina langu ni Zeid bin Harithah, natokana na kabila la Kalbin na nilikamatwa na kundi la mabedui walionileta katika soko la Akadha na kuniuza huko”.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akafurahishwa naye, akawa anampenda na kumkirimu sana, na Zeid naye alikuwa akimpenda sana Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na katika nyakati za usiku pale Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) anapojishughulisha na kutafakari na kuomba, mtoto huyo alikuwa karibu yake kwa ajili ya kumtumikia.

Baba yake Zeid alipopata habari za kutekwa kwa mwanawe na baada ya kuulizia ulizia na kujulishwa kuwa mwanawe alikuwa amemilikiwa na Muhammad bin Abdillah, akaifunga safari ya kuelekea Makka na alipowasili alisimama mbele ya Al Kaaba akasema kwa sauti kubwa:

“Enyi watu wa Makka! Nyinyi ni watu wakarimu mnaohudumia mahujaji na mnaowasaidia mateka. Nimekujieni kwa ajili ya mwanangu aliye mikononi mwenu nataka munirudishie mwenyewe”.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposikia maneno hayo akatangulia mbele na kumkabili Harithah huku akiwa amemshika mkono Zeid, akainama na kumuuliza:

“Unawajua ni nani hawa?”

Zeid akasema:

“Ndiyo. Huyu ni baba yangu na yule ni ami yangu”.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)akamwambia:

“Basi wazee wako hawa wamekuja kukuchukua ili urudi nao”.

Kisha akamuacha mkono na kumtanguliza mbele yao.

Zeid (Radhiya Llah anhu) akamkabili baba yake na kumwambia:

“Baba yangu, mimi sikubali kuachana na mtu huyu abadan, huyu ni mtu adhimu mwenye moyo mkubwa uliobarikiwa, na kama mmoja wenu ataishi naye siku moja tu, basi hatokubali kuachana naye maisha yake yote.”

Kisha akamkabili Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kumwambia:

“Sitomchaguwa mwengine isipokuwa wewe tu. Wewe ndiye baba yangu na wewe ndiye ami yangu”.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alitokwa machozi ya furaha, akamshika mkono Zeid huku akiyafuta machozi yake, kisha akasogea naye mpaka penye uwanja wa Al Kaaba na kusema kwa sauti kubwa:

“Shuhudieni kuwa Zeid ni mwanangu, ananirithi na mimi namrithi”.

Maneno haya yalimfurahisha sana hata Harithah baba yake Zeid kwa kujuwa kuwa mwanawe si kama ameachwa huru tu, bali amekuwa mwana wa Muhammad Mkweli Mwaminifu. Na hii ilikuwa ndiyo kawaida iliyokuwa ikitumika wakati ule.

 

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana Zeid (Radhiya Llah anhu) hata akawa anajulikana kwa jina la Zeid bin Muhammad mpaka pale ilipoteremshwa aya ya nne ya Suratul Ahzab iliyoharamisha mtu kuitwa kwa ubini usiokuwa wa baba yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

“Waiteni kwa (ubini wa) baba zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na kama hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu”.

Kisha Mwenyezi Mungu akaharamisha pia mtu kurithiwa na mwanawe wa kupanga (adopted child) katika aya ya 75 ya Suratul Anfal aliposema:

“Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (katika kurithiana). (Ndivyo ilivyo) Katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.”

Aly (Radhiya Llah anhu)

Katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwepo mtoto mwingine wa kiume naye ni Hindu mtoto wa bibi Khadija kwa mume wake wa  pili ’Abu Halah’, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana na akamlea malezi bora, akamuonyesha mapenzi na huruma na alikuwa akimtendea kama anavyowatendea wanawe.

Alipotimia miaka minane, Aly (Radhiya Llah anhu) naye akachukuliwa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kulelewa katika nyumba ya bibi Khadija (Radhiya Llah anha) kwa ajili ya kumpunguzia ami yake Abu Talib mzigo wa ulezi baada ya ami yake kupata shida mbali mbali.

Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) alimpokea Aly (Radhiya Llah anhu) kwa furaha na akamlea na kumuenzi kama anavyowalea na kuwaenzi wanawe.

Anakwenda Ghaari Hiraa

Siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alimwambia bi Khadija (Radhiya Llah anha) kuwa anahisi moyoni mwake kama kwamba anatakiwa ende penye pango linaloitwa Ghaari Hiraa nje kidogo ya mji wa Makka.

Bi Khadija (Radhiya Llah anha) akamwambia:

“Haya nenda, lakini pango hilo liko nje ya mji na mimi nakuogopea wewe kubaki huko peke yako”.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

“Usiogope Khadija, kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami”.

Baada ya bibi Khadija (Radhiya Llah anha) kumtayarishia chakula pamoja na baadhi ya mahitajio yake, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaondoka na kuelekea Ghaari Hiraa kwa ajili ya kukaa huko na kutafakari juu ya Mwenyezi Mungu.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kwenda pangoni hapo na kukaa kimya huku akitazama juu mbinguni. Alikuwa akiziangalia nyota na sayari, juwa na mawingu, mvua na upepo huku akitafakari na kujiuliza:

“Nani aliyevitengeneza vyote hivi? Bila shaka ipo nguvu kubwa yenye uwezo wa kuumba uhai pamoja na kuvitengeneza vyote hivi”.

Akawa anaendelea katika hali hii ya kutafakari wakati mkewe bi Khadija (Radhiya Llah anha) akibaki nyumbani na kuendesha shughuli zake. Lakini bibi Khadija alikuwa kila anapomfikiria mumewe akiwa peke yake pangoni tena nje ya mji alikuwa wakati wa mchana hana raha na wakati wa usiku hapati usingizi.

Alikuwa kila siku akimtuma mtu kwenda pangoni huko ili amletee habari za Muhammad na pia kwa ajili ya kumpelekea maji na chakula na baadhi ya mahitajio yake, na mara nyingine alikuwa akienda yeye mwenyewe.

Siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alirudi nyumbani kutoka pangoni akiwa na hofu kubwa sana, na bibi Khadija alipomuona katika hali ile akamuuliza:

“Kuna nini Muhammad?”

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

“Ewe Khadija! Nilipokuwa nikitembea huku na kule juu ya jabali, ghafla nikaona nuru iking’ara juu yangu kisha nikasikia sauti ikiniita:

“Ewe Muhammad, ewe Muhammad”.

Bibi Khadija akamuuliza:

“Na umeweza kujuwa sauti hiyo inatokea wapi ewe Abal Qassim?”

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

“Sikuweza kujuwa ewe Khadija, na nilikuwa kila ninapoisikia sauti ninageuka huku na kule kumtafuta mwenye sauti hiyo na wala simuoni mtu, nikaingiwa na hofu na kuamua kurudi nyumbani”.

Bibi Khadija akafanya haraka kumwendea bin ami yake Waraqa bin Noufel na kumhadithia yote aliyohadithiwa na Muhammad, na Waraqah akamwambia:

“Ewe binti wa ami yangu, hizi ni bishara njema kutoka mbinguni, mpe hongera zangu Muhammad na mwambie awe mvumilivu”.

Zammiluni zammiluni

Muhammd (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akawa anaendelea kwenda Ghaari Hiraa, na bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akawa anaendelea kumshughulikia kwa kuwatuma watumishi wampelekee vyakula na mahitajio yake ya kila siku na wakati mwingine yeye mwenyewe alikuwa akienda kumtembelea mumewe pangoni mpaka ilipofika siku ile aliporudi nyumbani Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akiwa anatetemeka huku meno yake yakigongana na kumwambia mkewe:

Zammiluni zammiluni’ – na maana yake (nifunikeni, nifunikeni). Bibi Khadija akamlaza mumewe kitandani kisha akamfunika huku akimpangusa  jasho lililokuwa likimtoka kwa wingi kichwani na huku akimwambia maneno ya kumtuliza mpaka usingizi ulipomchukuwa.

Aliamka akiwa bado uoga unaonekana usoni pake na bibi Khadija akamuuliza:

“Una nini ewe Abal Qassim?”

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

“Nilikuwa nimekaa pangoni, ghafla nikaona nuru juu yangu iliyonipitia kama umeme, kisha nikamuona mtu anateremka kutoka mbinguni huku akinikaribia. Nikaingiwa na khofu, lakini mtu huyo akaninyanyua na kunibana kwa nguvu kifuani pake kisha akaniacha, kisha akaniambia:

Iqra-a” – (‘soma’)

Nikamjibu kuwa mimi sijuwi kusoma. Akaninyanyua tena na kunibana kwa nguvu zaidi kifuani pake kisha akaniacha na kuniambia tena:

“Iqra-a”

Nikamwambia:

Maa – ana biqaarii – (Mimi sijuwi kusoma).”

Kisha akaninyanyua tena mara ya tatu na kunibana tena kifuani pake kisha akaniacha akaniambia tena:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1} خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2} اقْرَأْ وَرَبُّكَ

الْأَكْرَمُ {3} الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4} عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}

(Soma kwa jina la Mola wako Aliyekuumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako ni Karimu sana. Ambaye amefundisha kwa msaada wa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui).

Al Alaq – 1-7

Maneno hayo yalimshituwa sana bibi Khadija, akamtaka Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) avae nguo haraka na afuatane naye mpaka kwa Waraqah bin Noufel ili amhadithie mwenyewe yale aliyoyaona, na Waraqah akamwambia:

“Huyu ndiye Malaika mkubwa ‘Jibril’ ambaye Mwenyezi Mungu aliwateremshia Musa na Issa, yareti kama ningeliishi mpaka pale watu wako watakapokutoa nchini kwako”.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuuliza:

“Hivyo watakuja kunitoa?”

Waraqah akasema:

“Ndiyo, hapana aliyekuja na haya uliyokuja nayo wewe isipokuwa lazima atafanyiwa uadui, na nikijaaliwa kuishi mpaka siku hiyo, basi nitakusaidia mpaka utakapopata ushindi”.

 

Bibi Khadija akarudi nyumbani haraka akiwa amefuatana na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) huku moyoni mwake akiona fahari kubwa kuwa baraka za utume zimeangukia nyumbani kwake.

Siku moja bibi Khadija aliingia nyumbani kwake na kumuona Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akitetemeka mwili mzima juu ya tandiko lake huku akisema:

“Khadija. Jibril amenijia tena, akaniambia:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ {1} قُمْ فَأَنذِرْ {2} وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ {3} وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ {4}

وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ {5} وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ {6} وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ {7}

“Ewe uliyejifunika maguo. Simama uonye (viumbe). Na Mola wako umtukuze. Na nguo zako uzisafishe. Na mabaya yapuuze. Wala usiwafanyie ihsani(viumbe) ili upate kujikithirishia (wewe hapa duniani). Na kwa ajili ya Mola wako fanya subira (kwa kila yatakayokufika).”

(Suratul Mudathir aya ya 1 mpaka 7)

Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akainua uso wake kutizama juu mbinguni huku akimshukuru Mola wake, kisha akamtizama Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyekuwa akionyesha kuwa amechoka sana na kumwambia:

“Tulia upumzike ewe Muhammad”.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

“Zimekwisha zama za kupumzika ewe Khadija. Na umewadia wakati wa jihadi. Jibril keshanijia na ananitaka niianze kazi ya kuufikisha kwa watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu utakaouondoa ushirikina pamoja na uchupaji wa mipaka.”

Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akamwambia mumewe:

Labbayka ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mimi ni wa mwanzo kukuamini”.

Akasilimu bibi Khadija pamoja na wanawe wote wakiwemo Aly na Zeyd (Radhiya Llah anhum), lakini haukupita muda mrefu Waraqa bin Noufel alifariki dunia kabla ya kupewa utume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) jambo lililomhuzunisha sana bibi Khadija, kwani Waraqah alikuwa akiwasaidia sana katika kumliwaza Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wakati wa hofu, na kwa ajili hiyo bibi Khadija akahisi kuwa mzigo huo sasa umemuangukia yeye.

Hata hivyo bibi Khadija alikuwa akimsaidia sana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pale anapoona dhiki, hasa katika zile siku ambazo wahyi unakatika na Jibril anachelewa kumshukia, hapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) humwendea bibi Khadija na kumsikitikia na bibi Khadija kwa upande wake humpoza na kumwambia:

“Hapana ewe Muhammad. Wallahi Mwenyezi Mungu hawezi kukuhizi abadan, kwani wewe ni mkweli muaminifu, uliyetakasika mwenye kuwaendea watu wako na mwenye kuwasaidia wenye kuhitaji na kumuokoa mwenye dhiki”.

Mpe Khadija salamu

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akawa anaendelea kwenda pangoni kwa kufanya ibada zake, na mara nyingi Jibril (Alayhis Salaam)  alikuwa akimjia.

Imepokelewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa asubuhi moja bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alipokuwa njiani kuelekea pangoni alikutana na mwanamume mmoja aliyemsalimia na kumuuliza juu ya Muhammad. Bibi Khadija hakumjibu mtu huyo akihofia asije kuwa adui anayeweza kumdhuru Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam). Ikajulikana baadaye kuwa huyo alikuwa Jibril katika sura ya kibinadamu. Kwani Jibril alitangulia kufika pangoni kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kumwambia:

“Khadija sasa hivi atawasili akiwa amebeba chakula na maji kwa ajili yako. Atakapowasili mpe salamu zitokazo kwa Mola wake na mpe bishara njema juu ya nyumba aliyokwishajengewa Peponi”.

Baada ya kutaabika njiani, bibi Khadija aliwasili pangoni na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alimpokea kwa furaha huku akimwambia:

“Bishara njema kwako ewe Khadija. Amenijia Jibril hivi punde na amenipa salamu zitokazo kwa Mola wako Anayekupa bishara njema juu ya nyumba uliyokwishajengewa huko Peponi”.

Kufariki kwa Bibi Khadija

Watu wakaanza kuingia katika dini ya Kiislamu kwa wingi, na Abubakar (Radhiya Llahu anhu) alikuwa wa mwanzo katika wanaume akifuatiliwa na Uthman bin Affan, Al Zubeir bin Awaam, Abdul Rahman bin Auf, Saad bin Abi Waqaas na Talha bin Ubaidullah (Radhiya Llahu anhum). Wote hawa walisilimishwa na Abubakar siku ya mwanzo baada ya kusilimu yeye mwenyewe, akaenda nao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na wote hawa ni katika wale kumi waliobashiriwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) kuwa wataingia Peponi.

Siku iliyofuata Abubakar (Radhiya Llahu anhu) aliwasilimisha vigogo wengine wanne na kuja nao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), nao ni Uthman bin Madha-un, Abu Ubaidah Aamir bin Al Jarraah, Abu Salama na Al Arqam bin Abi l Arqam.

 

Bibi Khadija naye aliitumia mali yake yote katika kuunusuru Uislam, na kwa ajili hiyo nguvu ikaanza kuongezeka kidogo kidogo jambo lililowaghadhibisha sana Makureshi, wakaamua kuwazunguka na kuwapiga pande Waislamu muda wa miaka mitatu na kuwazuwia wasiweze kununua chochote, hata chakula. Ukawapitikia Waislamu wakati mgumu sana mpaka wakawa wanakula majani ya miti.

Waislamu wakahamia katika nyumba za Abu Talib, na bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alikuwa wakati mwingine akihatarisha maisha yake kwa kununua chakula na kuwapelekea kwa siri.

Haukupita muda mrefu tokea kumalizika kupigwa pande huko alifariki dunia Abu Talib ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na miezi miwili baadaye akafariki mama wa Waislamu Bibi Khadija binti Khuwaylid (Radhiya Llahu anha) katika mwaka uliokuja kujulikana kama ‘mwaka wa huzuni’ kwa sababu katika mwaka huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alifiwa na wapenzi wake wawili hao waliokuwa wakimsaidia sana na kumkinga.

 

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akiwa na umri wa miaka sitini na mitano alifariki katika mwezi wa Ramadhani mwaka wa kumi tokea Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) kupewa utume. Zipo riwaya zinazosema kuwa alifariki miaka mitatu kabla ya Hijra na riwaya nyingine zinasema miaka minne na nyingine zinasema mitano, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) mwenyewe ndiye aliyeteremka kaburini na kumzika na wakati huo hakukuwa na Swala ya maiti.

Baadhi ya sifa zake

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) hakupata kumpenda yeyote kati ya wake zake kama alivyompenda bibi Khadija (Radhiya Llahu anha), na hakuoa mke mwingine mpaka alipofariki bibi Khadija.

Ingawaje baadaye alioa wake wengi akiwemo bibi Aisha binti Abubakar (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa akipendwa sana kupita wake wenzake wote, lakini hakupata bahati aliyoipata bibi Khadija.

Hebu tumsikilize bibi Aisha mwenyewe (Radhiya Llahu anha) akituhadithia.

Anasema Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):

“Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa daima akimtaja Khadija, na siku moja alikuja kututembelea Halah dada yake Khadija nyumbani kwetu Madina, na sauti yake ilikuwa imefanana sana na sauti ya Khadija, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alipoisikia tu sauti yake akasema:

“Allahumma huyu ni Halah dada yake Khadija mfungulie mlango upesi”.

Anasema bibi Aisha:

“Nilimuonea wivu Khadija nikasema kumwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu:

“Nakuona unampenda sana Khadija, huachi kumtaja kila siku kama kwamba hapana mwanamke mwengine duniani isipokuwa yeye. Khadija hakuwa na chochote cha zaidi isipokuwa alikuwa mwanamke mzee, na Mwenyezi Mungu amekwishakupa aliye bora kuliko yeye”.

Anaendela kusema bibi Aisha;

“Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alinikiasirikia sana siku hiyo kwa kauli yangu ile akaniambia:

“Hapana wallahi! Hakunipa aliye bora kuliko yeye, kwani yeye aliniamini wakati watu waliponikadhibisha na akanisaidia kwa mali yake wakati watu waliponinyima, na kupitia kwake akaniruzuku watoto”.

Anasema bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):

“Nikajisemea moyoni mwangu; 'sitomsema tena vibaya Khadija.”

 

Na katika hadithi nyingine anasema bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) alikuwa anapochinja mbuzi daima akipeleka nyama kwa marafiki wa Khadija, na siku moja nilimuuliza kwa nini anafanya hivyo, akanijibu:

“Mimi nawapenda wote alokuwa akiwapenda”.

 

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alikuwa wa mwanzo kupita wote kumuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam), na wa mwanzo kusilimu miongoni mwa wanawake na wanaume, na wa mwanzo kuswali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) wakiwa peke yao nyumbani.

Alikuwa mara nyingi akimliwaza na kumtuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) anapodhikika au anapoadhibishwa au kukadhibishwa au kutukanwa au anapopata mateso ya aina yoyote kutoka kwa makafiri wa Makka.

Mafunzo

1- Mtu asivunjike moyo hata kama ana tumaini dogo namna gani, kwani bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliliona tumaini ndani ya Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) pale alipokuwa akizihesabu sifa zake tukufu moja baada ya nyingine, akiwa na tumaini kuwa mtu huyu ndiye atakayekuwa Mtume anayesubiriwa, juu ya kuwa hizo zilikuwa ni fikra njema tu, lakini hatimaye zikageuka kuwa ukweli halisi.

    Alipotamani kuolewa naye, aliliona tumaini lake kuwa mfano wa ndoto, lakini hakuiacha iwe ndoto, bali alizindukana na kuifuatilia ndoto hiyo mpaka ikageuka kuwa kweli.

 

2- Mwenendo wa makafiri wa kuwazunguka Waislam na kuwapiga pande na kuwafanyia vikwazo vya kiuchumi na vya kibiashara na kuwaacha wakiwa na njaa wakidhani kuwa mwisho wake watakuja kuwapigia magoti. Darsi hii inatufundisha kuwa mila za kikafiri ni namna moja tokea wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) mpaka wakati wetu huu.

 

3- Mstahamilivu hula mbivu. Waislamu walistahamili kila aina ya tabu na adhabu, mateso na uadui uliokuja kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu tokea siku ya mwanzo, lakini ustahamilivu wao huo haukupotea bure, kwani hatimaye waliweza kupata dola yao na kupambana na adui zao waliokuja kuwapiga vita kutoka kila pembe ya dunia na kupata ushindi wa nyumba mbili. Nyumba ya dunia na nyumba ya Akhera.

 

Share