Akiokota Tunda Shambani Mwa Mtu Ni Halaal Kwake?

Akiokota Tunda Shambani Mwa Mtu Ni Halaal Kwake?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Masheikh wangu wa alhidaaya nataka muniwekee bayana hasa juu ya hili suali langu kwani linanipa mashaka sana juu ya kutaka kulifahamu na kuweza kuliwacha au kuendelea nalo. Hii ni kwa sababu baadhi ya masheikh ambao tayari nimewafika baadhi yao wanasema yakuwa si halali na wengine hulijuzisha kwa kusema kwamba (Milatul-biladi sharia). Swali: Mtu kupita katika shamba la watu na akakuta matunda yameanguka je, anayohaki ya kuchukua na kula hali ya kua ni halali kwake matunda hayo au si halali? Upande wowote uwao, naomba kupatiwa ushahidi kutoka katika kitabu na sunna za Mtume (s.a.w)

 

 

JIBU:

 

 AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ‘ibaadha na ‘ibaadah   inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

 

Hakika inayokubaliwa na kila mmoja wetu ni kuwa shamba si la anayetunda tunda lililoanguka bali ni la mtu mwengine. Lau lingekuwa ni shamba lake basi hangehitaji ruhusa kwa sababu ni miliki yake.

 

Ikiwa kitu si chako kisheria na hata kiakili huwezi kuchukua ila upawe idhini na mwenye shamba. Kwa hali hiyo ya ki Shariy’ah haitakuwa halali kwako kuchukua tunda lililoanguka katika shamba la mtu mwengine.

 

Hata hivyo, 'Urf (ada na desturi) ni miongoni mwa chimbuko la Shariy’ah katika Dini yetu tukufu. Ikiwa inafahamika na ni ada katika mji au kijiji unachoishi kuwa yafaa kwako kuchukua tunda lililoanguka basi kutakuwa hakuna tatizo lolote unapofanya hivyo, kwani hiyo itakuwa ni ada isiyopingana na Shariy’ah yetu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share