04-Kukata Undugu: Tiba Ya Kukata Undugu

 

TIBA YA KUKATA UNDUGU

 

Tumeona kukata undugu na madhara yake na baadhi ya sababu zinazopelekea hilo.

Ikiwa mambo ni hivyo, hapana budi kwa mwenye akili atahadhari na kukata undugu, na ajiepushe na sababu zinazopelekea hilo na ajue ukubwa wa undugu apupie sababu za kuunga achunge adabu zinazopasa kuchunga pamoja na Ndugu.

 

Ni nini kuunga undugu?

 

Na kwa vitu gani inakuwa?

 

Na ni nini fadhila zake?

 

Na ni njia zipi na sababu zinazosaidia hilo?

 

Na ni adabu zipi zinapasa kuzichunga pamoja na Ndugu wa karibu?

 

 

NI NINI KUUNGA UNDUGU?

 

Kuunga undugu ni kinyume cha kuhamana.

 

Kuunga undugu ni kuwafanyia wema ndugu wa karibu kwa nasaba au kwa ukwe kuwafanyia huruma upole na kuchunga hali zao hata wakiwa mbali na wakafanya vibaya au wakakukata.

 

 

NI KWA LIPI INAKUWA KUUNGA UNDUGU?

 

Kuunga undugu kwa mambo mengi inakuwa kwa kuwatembelea kuwajulia hali kuwaulizia kuwapa zawadi na kuwaweka kuendana na daraja zao na kuwapa sadaka mafakiri wao kuwafanyia upole matajiri wao kuwaheshimu wakubwa kuwaonea huruma wadogo na madhaifu pia kuwasiliana nao kwa barua simu kuwafanyia ziara kuwakaribisha kuwapokea vizuri kuwatukuza kuwanyanyua katika mambo yao na kumuunga anayekukata.

 

Inakuwa pia kushirikiana nao katika furaha kuwaliwaza katika matatizo kuwaombea dua kuwasafishia vifua kuwapatanisha waliogombana kuwa na pupa ya kuthibitisha mahusiano kuwatembelea wagonjwa wao kuwaitikia wito.

 

Na kubwa katika kuunga undugu, apupie mtu kuwalingania katika uongofu kuwaamrisha mema kuwakataza maovu.

 

Na undugu huu utaendelea ukiwa mwema wenye kutengamaa.

 

Ama ikiwa ndugu kafiri au muovu inakuwa kumuunga kwa kuwapa mawaidha na kuwakumbusha na kujitolea kwa juhudi katika hilo.

 

Ukiona wanakupinga au kukufanyia makusudi au ukijiogopea kupotea nao basi wahame vizuri bila kuwafanyia maudhi na uzidishe kuwaombea du’aa huenda Allaah Akawaongoza kwa baraka ya du’aa zako. Na ukipata fursa ya kuwalingania mara kwa mara itumie.

 

Na inapendezeshwa katika kuwalingania ndugu na kuwapa nasaha ufanye wema katika kuamiliana nao utumie upole hikma na mawaidha mazuri wala usiingie nao katika mjadala ila kwa uchache na kwa wema kwani walinganiaji wengi athari yao katika familia na kabila ni ndogo. Na hili linatokea kwa walinganiaji hawafanyi upande huu kuwa ni muhimu kuwalingania ndugu wangetafuta njia wangefaulu na kuwaathiri, mfano kuwanyenyekea, kuwajali, kuwaunga, kujipendezesha kwao.

 

Na ni juu ya familia au kabila wawaheshimu wenye elimu katika familia kuwasikiliza na kutowadharau.

 

Ikitokea hili katika familia watakuwa huru katika kupanda kufikia ukamilifu na fadhila.

 

Share