Zingatio: Kila Mtu Ataingia Peponi Isipokuwa Anayekataa

 

Naaswir Haamid

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amewaumba majini na watu kwa lengo la kumuabudu Yeye Pekee. Wala Hakuwaleta duniani kuja kufanya masikhara na kuumaliza muda wao bila ya mambo ya msingi.

Kwa hakika ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Waislamu walio wengi kabisa hawaelewi lengo hilo. Ndio maana wamekosa muelekeo na kumalizia muda wao mwingi kwenye shughuli zilizo nje ya mwenendo sahihi wa Uislamu.

Bado Waislamu wamevumbikwa na ujinga; ilhali elimu, majarida, mitandao na madrasa za Kiislamu zipo chungu nzima. Asilimia kubwa ya wenye kuupuuza Uislamu ni wale waliofumbua macho wakiwaona wazee wao ni Waislamu. Kwa upande mwengine, tunashuhudia Waislamu ambao wazee wao sio Waislamu ni wenye himma zaidi. Ule msemo wa asiyekujua hakuthamini ndio tumejibebesha sisi. Kwani hao Waislamu wepya walioingia kwenye Uislamu wanauthamini zaidi Uislamu wao. Wao wameusoma, wakauelewa na wakauthamini.

Enyi Waislamu tunatarajia nini kwa Mola wetu hali ya kuwa tunatupa muda wetu bila ya kumuabudu Yeye? Swala ya Alfajiri yatukuta kitandani, adhuhuri tukiwa makazini, alaasiri tukiwa wachovu, magharibi yakimiwa tukiwa tumeganda kwenye kioo cha runinga na Swala ya Ishaa inatupita tukiwa matembezini. Tumesahau ya kwamba wenye kutupwa motoni wanatokana na kuacha kusimamisha Swalah? Qur-aan Tukufu yatueleza (tafsiri):

{{"Ni kipi kilichokupelekeni Motoni?" Waseme: "Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakiswali…"}} [al-Muddaththir: 42-43]

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha ya kwamba Umma wake wote utaingia Peponi isipokuwa kwa anayekataa. Hadiyth ifuatayo inafafanua zaidi (tafsiri):

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu): hakika amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Umma wangu wote utaingia Peponi isipokuwa kwa atakayekataa)) Pakasemwa: na ni nani huyo atakayekataa ewe Mjumbe wa Allaah? Akasema: ((Mwenye kunitii mimi ataingia Peponi, na atakayeniasi basi huyo amekataa)). [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, Buluughul-Maraami, Hadiyth ya 157]

Ila yahitajika juhudi na kuonesha moyo wa kumukhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Tusitegemee tulale tuu halafu tushushiwe riziki kama alivyofanyiwa bibi Maryam '(Radhiya Allaahu ‘Anha). Wahenga wanatwambia kwamba "Kazi mwanamandanda, kulala njaa kupenda".

 

Ummah huu alioulilia Nabii Muusa (‘Alayhi swalaatu was-salaam) kwa kuomba angalau kuwa ni mfuasi tu. Alikuwa tayari kuuacha Utume wake ili awemo tu ndani ya Ummah huu. Lakini wapi?! Rejista la wafuasi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) limeshajaa zamani. Sisi tuliozipata, tunazichezea fursa hizi.

Kwa ufupi, hali ngumu ya maisha na mitihani ya kuvamiwa ardhi zetu yanatukuta kwa sababu ya ujinga wetu. Haya yametokana na kupuuza amri za Mola Mlezi. Ndio maana tumezungukwa na wanafiki pamoja na rafiki zao makafiri walio wengi. Wanatutesa na kutuacha tukiteseka huku wao wakifurahi kabisa - Zimwi likujualo halikuli likakwisha..

 

 

 

Share