05-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Mapenzi Yetu Kwa Ahlul-Bayt

 

Mapenzi yetu kwa Ahlul Bayt

 

 1-   Watu wa Ukoo

 

Ahlus Sunnah wanawapenda na kuwaheshimu watu wa ukoo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wamewaweka katika daraja ya juu wanayoistahiki.

Hawa ni binti zake wote, pamoja na Bibi Faatwimah na wanawe Al-Hasan na Al-Husayn na watu wa ukoo wake tuliotangulia kuwataja kuwa ni katika Ahlul Bayt wakiwemo ‘Aliy bin Abi Twaalib na watu wa nyumba yake, na Al-‘Abbaas bin Abdil-Muttwalib na watu wa nyumba yake, na ‘Aqiyl bin Abi Twaalib na watu wa nyumba yake na Ja’afar bin Abi Twaalib na watu wa nyumba yake (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Allaah Amewaondolea uchafu na kuwasafisha barabara watu hawa na Akatuamrisha katika kitabu chake kitukufu kuwapenda, na pia Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametuamrisha tuwapende.

Katika Sahih Muslim imeelezwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipowahutubia watu mahali panapoitwa Ghadiyr aliwaambia:

 

{ وأهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي }.

 

«Na watu wa nyumba yangu. Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu, Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu.» Muslim

 

Allaah Anasema:

 

((إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا))

 

«Hakika Allaah na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu» Al-Ahzaab -56

 

Ilipoteremshwa aya hii Masahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

«Vipi tukuswalie?»

Akawaambia:

«Semeni:

 

{اللهم صل على محمد وعلى آل محمد، كما صليت على إبراهيم وعلى آل إبراهيم إنك حميد مجيد، وبارك على محمد وعلى محمد، كما باركت على إبراهيم وعلى آل إبراهيم إنك حميد مجيد}.

 

Mola wangu Mswalie Muhammad na Aali ya Muhammad, kama ulivyomswalia Ibraahiym na aali ya Ibraahiym hakika Wewe ni Msifiwa na Mwenye kutukuzwa. Na umbariki Muhammad kama ulivyombariki Ibraahiym na aali ya Ibraahiym hakika Wewe ni Msifiwa na Mwenyeye kutukuzwa.”

 

Anasema Ibnul Qayyim katika kuisherehesha hadithi hii:

Kuwaswalia Aali zake ni katika kukamilisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa sababu kufanya hivyo ni katika kumfurahisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na Allaah Anamuongezea daraja na heshima (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Imepokelewa kuwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu anhu) alisema:

 

[[ارقبوا محمداً في آل بيته]].

 

“Mpeni heshima Muhammad kwa (kuwaheshimu) watu wa nyumba yake.”

 

Na alisema pia:

 

[[والله لأن أَصِلَ قرابة رسول الله صلى الله عليه وسلم أحب إلي من أصل قرابتي]]

 

“WaAllaahi, kuwasiliana na jamaa zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni bora kwangu kuliko kuwasiliana na jamaa zangu.” Al-Bukhaariy

 

Na ile hadithi isemayo: « Faatwimah ni Bibi wa wanawake wa Peponi.»

Imepokelewa kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Imepokelewa pia kuwa siku ile Abu Sufyaan alipokuja kusilimu mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

«Huyu hapa Abu Sufyaan amekuja mwenyewe kwa miguu yake, niruhusu nimkate kichwa chake».

Al-‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

«Ewe Mtume wa Allaah mimi namuingiza Abu Sufyaan katika himaya yangu.»

Al-‘Abbaas akakaa karibu na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na alipomuona ‘Umar (Radhiya Allaahu anhu) anashikilia kutaka kumkata kichwa Abu Sufyaan, Al-‘Abbaas akamuambia:

«Taratibu ewe Umar angelikuwa huyu ni katika watu wa kabila lako la Bani ‘Uday bin Ka’ab usingelishikilia namna hii, lakini kwa vile huyu ni mtu (wa kabila langu) anayetokana na ukoo wa Abdu Manaf.»

Umar akasema kumuambia Al-‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhum):

«Taratibu ewe ‘Abbaas, kwani WaAllaahi naapa kuwa siku uliyosilimu wewe ilikuwa bora kwangu kuliko angelisimu baba yangu Al-Khattaab, kwa sababu naelewa kuwa kusilimu kwako kulimfurahisha sana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).» At-Twabaraaniy, Al-Bidaayah wan- Nihaayah- Ibni Kathiyr na Siyrat Ibn Hishaam

 

Hadithi hizi na nyingi nyingine zinatufundisha namna gani watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) walivyokuwa wakiwapenda Masahaba, na pia Masahaba walivyokuwa wakiwapenda watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na zinatufundisha pia namna gani Ahlus Sunnah walivyojishughulisha kuzitafuta na kuziandika hadithi zinazowahusu watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Masahaba na pia ‘Tabi’iyna’ (waliokuja baada yao) walijishughulisha sana kutafuta na kuziandika fadhila za watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ili watakaokuja baada yao wazijuwe na kuzichunga na kuzifuata. Na hii ndiyo sababu utakaposoma kitabu chochote katika vitabu vya Ahlus Sunnah hukosi kuona ndani yake mlango maalum uliohusishwa kwa ajili ya sifa za Ahlul Bayt. Utayakuta haya katika vitabu vya Hadiyth na vitabu vya ‘Aqiydah na hata katika vitabu vya Tariykh ‘historia’.

Imam Al-Bukhaariy kwa mfano, amehusisha mlango maalum juu ya fadhila za Imam ‘Aliy (Radhiya Allaahu anhu), na amehusisha mlango wa fadhila za Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) n.k.

 

Imam Muslim katika mlango wa Fadhila za Masahaba ameandika juu ya fadhila za Maimaam Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Imam At-Tirmidhy na Ibni Maajah na Imam Ahmad bin Hanbal na Ibni Kathiyr na At-Twabariy na Ibni Taymiyah na Adh-Dhahabiy na wengine, wote hawa katika vitabu vyao wameandika kwa mapana na marefu juu ya fadhila za Maimam hawa wawili ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amewaita ‘Mabwana wa vijana wa Peponi.’

Hizi zote ni dalili wazi juu ya heshima tunayowapa watu wa nyumba hii tukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Share